Sunday, September 30, 2018

SIKU YA MOYO DUNIANI YAADHIMISHWA KWA KUTOA ELIMU NA UPIMAJI WA AFYA

SIKU ya moyo duniani imeadhimishwa leo Septemba 29 ikiwa lengo mahususi kwa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujua na kupima magonjwa mbalimbali ya moyo, pamoja na kuelimisha jamii juu ya athari mbalimbali zinazotokana na magonjwa ya moyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa afya, wazee, jinsia na watoto Faustine Ndugulile amesema kuwa  maadhimisho ya Siku ya Magonjwa ya Moyo Duniani mwaka yamekuja na kauli mbiu ya ‘MOYO WANGU, MOYO WAKO’ kwa lugha ya kiingereza  My heart, Your heart, ikiwa na lengo la kusisitiza juu ya kila mmoja wetu kufanya uchunguzi wa moyo ili kujua hali yake.

Aidha amesema; "Magonjwa ya moyo yanaongoza kwa kusababisha vifo duniani. Inakadiriwa kuwa watu 17,500,000 hufa kila mwaka duniani kote kutokana na magonjwa ya moyo na kiharusi. Ugonjwa wa moyo ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote; watoto, watu wazima, wake kwa waume. Aidha, Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kwamba asilimia 40% ya vifo vyote vinavyotokea duniani vinasababishwa na magonjwa ya moyo. Pia nusu ya vifo ambavyo vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza vinatokana na magonjwa ya moyo na vilevile asilimia 80% ya vifo hivi hutokea kwenye nchi zenye uchumi wa kati na wa kiwango cha chini" amesema Ndugulile.

Aidha imeelezwa kuwa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake yanakadiriwa kusababisha vifo vya watu 6,000,000 duniani kila mwaka na pia huchangia kusababisha asilimia 10% ya wagonjwa wenye magonjwa ya moyo. Vilevile moshi wa sigara kwa watu wasiovuta sigara (second hand smoking) husababisha vifo vya watu laki sita (600,000) na kati ya hao 28% ni watoto. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani (WHO).

Pia amesema kuwa kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la Moyo ifikapo mwaka 2035 litaongezeka na kufikia makadirio ya wagonjwa wapya milioni 131,978,870 (sawa na ongezeko la 45% kutoka hali ilivyo kwa sasa), huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa moja wapo.

Pia ameeleza kuhusu tafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mwaka 2012, ulionyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 15.9% ya wananchi wanavuta sigara, asilimia 29.3% wanakunywa pombe, asilimia 97.2% wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa wiki.

 Aidha utafiti ulionyesha asilimia 26% ya wananchi ni wanene kupita kiasi, asilimia 26% wana lehemu nyingi mwilini, asilimia 33.8% wana mafuta mengi mwilini, asilimia 9.1% wana kisukari na asilimia 25.9% wana shinikizo kubwa la damu. Utafiti pia ulionyesha 25% ya wananchi waliohojiwa hawajishughulishi na kazi zinazotumia nguvu na hawafanyi mazoezi yeyote. Viashiria hivi ndivyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Moja wapo ya sababu kubwa za magonjwa ya shinikizo la damu ni kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye misuli ya moyo. Kuziba kunaweza kusababishwa na mafuta yaliyomo kwenye chakula ambayo huenda huganda katika kuta za mishipa hiyo, hali ambayo hutokea pole pole na huchukua muda mrefu hadi mishipa kuziba kabisa. Matumizi ya tumbaku, uzito uliozidi na kutofanya mazoezi huchangia sana uwezekano wa kupata ugonjwa wa shinikizo la damu na  hii hupelekea mtu kupata matatizo hayo. 

Imeelezwa kuwa ugonjwa wa Moyo umekuwa na vyanzo mbalimbali vinavyosababisha tatizo hili kukua kwa kasi hapa nchini na Duniani kote. vyanzo hivyo vikubwa ni pamoja na: Mtindo wa kimaisha (Life Style), Ulaji usiofaa, Kutofanya Mazoezi, Matumizi ya pombe, Uvutaji wa Sigara na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku  

Ili kuzuia ugonjwa wa Moyo na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata maradhi ya Moyo . 

Na ametoa rai kwa wananchi wote nchini watoe ahadi kwa ajili ya moyo wangu, moyo wako na mioyo ya watu wengine, na tuchukue hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya magonjwa ya moyo na kuweka ahadi ya mtu binafsi ya kupika na kula chakula kinachokidhi viwango vya afya,

Ahadi ya kujitahidi kufanya mazoezi na kuwafundisha na kuwahimiza watoto wetu kufanya mazoezi,ahadi ya kutovuta sigara na kutumia bidhaa za tumbaku, na kuwahimiza wapendwa wetu ambao wanavuta sigara na kutumia bidhaa za tumbaku kuacha kabisa, ahadi kwa watoa huduma za afya, kujitahidi kutoa huduma bora ya kuelimisha, kukinga na kuokoa maisha, 

ahadi ya viongozi wa kitaifa kufanikisha mpango mkakati wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na amewakaribisha wananchi wote kwenye zoezi la uchunguzi linaloendelea katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.Kwa upande wake Rais wa Chama cha madaktari wa moyo nchini Dkt. Robert Mvungi amesema kuwa tatizo la moyo ni kubwa na gharama ni kubwa na kinga ni sisi wenyewe kubadili mifumo ya maisha. 

Na amesema kuwa kuna tishio kwa ugonjwa wa moyo kwani watu wenye umri mdogo hupata ugonjwa wa moyo na amesema baadhi ya visababishi ni pamoja na presha ambapo zaidi ya asilimia 20 ya watu wa chini ya miaka 25 wana presha.Sigara, mfumo wa maisha na matumizi ya pombe.

Amewaasa wananchi kubadili mifumo ya maisha,kufanya mazoezi  na kuepuka matumizi ya sigara na pombe.
 Matembezi ya Siku ya Moyo Duniani yakiendelea, ambayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya 'Moyo wangu, Moyo wako"
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile  akiongoza mazowezi siku ya Moyo Duniani yaliyoanzia viwanja vya Leaders Club na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es sala, matembezi hayo yamebeba kauli mbiu ya "Moyo wangu Moyo Wako". Wakwanza Julia ni Mkurugenzi wa kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akikagua moja kati ya mabanda yaliyokuwepo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani. Kushoto kwake ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Robert Mvungi, kulia kwake ni Mkurugenzi wa kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya Dkt. Amalberga Kasangala



Madakitari wakitoa elimu na kipima afaya za wananchi walijitokeza katika maadhimisho ya siku ya Moyo Duniani.(picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)

MAZISHI YA IGP MSTAAFU PUNDUGU YAFANYIKA DAR

1
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa IGP Mstaafu marehemu Samwel Pundugu Mji Mwema Kigamboni ambapo alizikwa jana katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
2
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akiwa na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wastaafu,(kulia) na kushoto kwake ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye wakati wa mazishi ya IGP mstaafu marehemu Samwel Pundugu katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
3
Maofisa wa Polisi wakiwa wamebeba jeneza la mwili wa IGP Mstaafu marehemu Samwel Pundugu wakati wa mazishi yake katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
4
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akitoa heshima baada ya kuweka shada la maua katika kaburi la IGP Mstaafu marehemu Samwel Pundugu katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
5
Askari Polisi wakishiriki kushusha mwili wa IGP Mstaafu marehemu Samwel Pundugu kaburini wakati wa mazishi yake katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
6
Viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na familia ya IGP Mstaafu marehemu Samwel Pundugu baada ya mazishi yake katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.Picha na Jeshi la Polisi)

“TAA KUIFUNGUA TANZANIA KWA ULIMWENGU”

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kushoto) akiongea na waandishi kuhusiana na viwanja vya ndege kuchagiza uingiaji wa watalii nchini. Kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax Mabula.



Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imejipanga kupitia kaulimbiu yake kuifungua Tanzania kwa ulimwengu kupitia sekta ya Utalii nchini, kwa kuimarisha usafiri wa anga ili kuhakikisha watalii wote wanafikia vivutio vyote vya utalii kwa haraka zaidi.

Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alipokuwa akizumgumza na waandishi wa habari siku ya ushiriki wa Mamlaka katika Tamasha la Urithi Wetu linaloanza leo Jumatatu (Oktoba Mosi, 2018) kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Viwanja vyetu vya ndege ndio milango mikuu wa watalii kupita, hivyo tupo hapa kuwaambia wananchi, wadau pamoja na Jumuiya za Kimataifa kwamba sasa kuna fursa ya kutanganza vivutio vya kitalii kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa kuwa vinatumika kwa usafiri wa anga lakini pia tunaweza kuvitumia kibiashara kwa kutangaza vivutio vyetu” alisema Bw. Mayongela.

Bw Mayongela pia amewapa wito Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza vivutio vilivyopo kupitia Viwanja vya ndege lakini pia kuwaeleza wadau kwa njia mbalimbali zilizopo Tanzania ili watalii wanapowasili waweze kupata picha halisi ya maeneo ya kutembelea akiwa nchini.

Aidha Bw. Mayongela ameongeza kwamba Mamlaka ina mtandao mkubwa na inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali, ambavyo vipo kila sehemu penye vivutio vya utalii na wamejiimarisha kuhakikisha huduma bora ya usafiri wa anga.

“Sehemu ya Kaskazini mwa nchi yetu ambapo ndio kuna vivutio vingi, vipo viwanja vya ndege vya kutosha, tuna Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), Kiwanja cha Lake Manyara ambacho kimejengwa kwa mkakati wa kutumika kwa watalii na kinafanya vizuri sana kwa kuingiza watalii wengi, vilevile tuna mpango wa kujenga kiwanja kipya katika Mkoa wa Manyara,” alibainisha Bw. Mayongela.

Akizungumzia miundombinu ya Viwanja vya Ndege kwa Kanda ya Kusini ameeleza kwamba serikali imejitoa kufanya maboresho ya kiwanja cha Mtwara kwa lengo moja kuu la kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo maeneo hayo.

“Serikali inaboresha kwa kufanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa Kiwanja Cha Ndege cha Mtwara, pamoja na sababu za kiuchumi lakini pia lengo ni kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vilivyopo, sio hivyo tu lakini pia Kilwa masoko tuna kiwanja, Lindi tuna kiwanja, Nachingwea mpaka Masasi kote tuna viwanja” Alisema Bw. Mayongela.

Akizungumzia upande wa nyanda za juu Kusini Bw. Mayongela amebainisha kwamba baada ya ukarabati mkubwa kukamilika kutakuwa na kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe, Njombe mpaka Iringa kutakuwa na viwanja vizuri vya ndege ili kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo Tanzania vinafikika kwa urahisi.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabula ameeleza kwamba Tamasha la Urithi Wetu lililobuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lina madhumuni makuu mawili ikiwemo ya kuwezesha kuonyesha fursa zote zinazoizunguka tasnia hii.

“Madhumuni makuu ni kuendeleza, kutambua na kuhifadhi urithi wetu wa utamaduni kwa ajili ya kizazi kilichopo na kinacho kuja lakini pili ni kubadili urithi wetu wa utamaduni kuwa zao la utalii hayo ndio malengo makuu mawili” alisema Prof Mabula.

TAA wametoa msaada wa fulana 100 kwa ajili ya washiriki wa tamasha la Urithi Wetu, ambalo litafikia tamati Oktoba 6, 2018 kwa kufungwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
a Iringa wakati akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani humo inayokwenda kwa jina la "Iringa Mpya" ambapo watedaji kutoka wilaya zote na wataalam walijumuika pamoja katika mkutano huo.

MKUU WA WILAYA ARUMERU AWAHIMIZA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI KWA WAKATI


Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wafanyabiashara iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi. Semina hiyo imefanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu, Diana Masalla akiwaelimisha wafanyabiashara kuhusu mabadiliko ya Sheria za Kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Afisa Kodi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Shaban Makumlo akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu, Adelaida Rweikiza akiwaelimisha wafanyabiashara kuhusu Mfumo wa Maadili kwa Watumishi wa TRA wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wakifurahia hotuba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry Muro wakati wa ufunguzi wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya Mabadiliko ya Sheria za Kodi, Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi na Mfumo wa Maadili kwa watumishi wa TRA. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO)


……………………….


Na Veronica Kazimoto,Arumeru

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amewahimiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati ili kufikia azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza wakati akifungua semina ya wafanyabiashara hao iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkuu wa Wilaya huyo amesema kuwa, maendeleo yanayopatikana kutokana na kodi, hayawanufaishi walipakodi pekee bali taifa zima kwa ujumla.

“Ndugu zangu wafanyabiashara kodi mnazolipa ndio zinaiwezesha serikali kujenga nchi na kutoa huduma mbalimbali za jamii kama vile elimu, afya, miundombinu ya usafirishaji, maji, umeme na mengine mengi,” alisema Muro.

Aliongeza kuwa, nchi nyingi zilizoendelea duniani, wananchi wake hulipa kodi kwa wakati na hiari, hivyo ili Tanzania ifikie uchumi wa kati na wa viwanda ni lazima wananchi wajenge tabia ya kulipa kodi kwa wakati.Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo, amewasisitiza wafanyabiashara hao kutumia Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) na kuhakikisha wanatoa risiti kila wanapouza bidhaa au huduma mbalimbali kwani mashine hizo huwasaidia kutunza kumbukumbu na kujua mwenendo wa biashara zao.

Kwa upande wake Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Diana Masalla alisema kuwa, lengo la semina hiyo ni kuongeza uelewa juu ya Mabadiliko ya Sheria za Kodi, Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi na Mfumo wa Maadili kwa watumishi wa TRA.

Semina za wafanyabiashara na watumishi wa TRA katika Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimemalizika ambapo watumishi wamesisitizwa kuzingatia maadili wakati wafanyabiashara wametakiwa kuchangamkia msamaha wa riba na adhabu na kutoa taarifa pale ambapo mtumishi yeyote wa TRA atajiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwa ni pamoja na kuomba au kupokea rushwa.

Saturday, September 29, 2018

MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA MADINI YAZIDI KUONGEZA MAPATO


Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi.



Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi.



Na Mwandishi wetu, Geita.

Mageuzi makubwa katika sekta ya madini nchini yameifanya sekta hiyo kuendelea kuongeza mapato ya Serikali kutoka bilioni 194.6 ilizopanga kukusanya mwaka 2017/18 hadi kufikia shilingi bilioni 301.6 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 55.

Hayo yameelezwa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi mkoani Geita wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Serikali.

Dkt. Abbasi ameeleza kuwa ongezeko hilo la mapato katika sekta ya madini limechagizwa na mabadilikomkatika sheria za madini, kujengwa kwa ukuta wa Mirerani na kuzuia kwa usafirishaji wa mabaki (kaboni) ya dhahabu nje ya mkoa yanapochimbwa madini.

“Mheshimiwa Rais aliagiza kujengwa ukuta eneo la wachimbaji wadogo la Mirerani na April mwaka huu ukuta huo ulikamilika na kuwezesha kuongezeka kutoka kilo 164.6 za madini ya Tanzanite yenye thamani yas milioni 71.8 mwaka 2016 hadi kufikia kilo 449.6 zenye thamani ya shilingi milioni 893.8 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018”, ameeleza Msemaji Mkuu wa Serikali.

Ameeleza kuwa kutokana na usimamizi mzuri, makampuni ya uchimbaji madini yameendelea kutoa mchango wake kwa jamii ambapo Geita Gold Mine imetoa shilingi bilioni 9.2 kwa mkoa wa Geita kama mchango wa kampuni hiyo kwa maendeleo ya mkoa huo.

Aidha, Msemaji Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa zuio la kaboni zenye dhahabu kusafirishwa na kuchakatwa nje ya mkoa zinakozalishwa limesaidia kuongeza pato kwa Serikali kufikia shilingi milioni 850 kwa mwezi Agosti mwaka huu kutoka shilingi milioni 400 kwa mwezi April.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali, Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kufanya mageuzi mbalimbali ikiwemo kujenga vituo saba vya umahiri vitakavyokamilika Disemba mwaka huu kwa thamani ya shikingi 11.9 kuwapatia wachimbaji wadogo mafunzo na utaalamu zaidi wa uchimbaji. Aidha, vituo vinne vya mfano pia vitajengwa kwa thamani ya shilingi tono kuwasaidia wachimbaji kupata teknolojia rahisi ya uchenjuaji wa madini na kuyaongezea thamani.

Kwa upande wa sekta ya afya, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa uwekezaji mkubwa wa vifaa, wataalamu na majengo umefanyika katika hospitali za Muhimbili, Mloganzila, MOI, Bugando, Benjamin Mkapa na ambapo hivi sasa Tanzania inapokea wagonjwa kutoka Komoro, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia kwa ajili ya kupata matibabu ya kibingwa ya moyo, figo, mifupa na kuongeza uwezo wa kusikia.

“Serikali imeendelea kusogeza huduma za afya karibu kwa wananchi kwa kujenga hospitali za rufaa katika mikoa saba, hospitali za Wilaya 67 zinajengwa mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 105 na tayari vituo vya afya 210 pamoja na nyumba za wahudumu wa afya vimejengwa” amesisitiza Dkt. Abbasi.

Katika hatua nyingine, Dkt Abbasi ameeleza kuwa hali ya uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara ukikua kwa takribani asilimia 7.0 mpaka 7.1 kwa mwaka na kwamba kwa mujibu wa ripoti mbalimbali ikiwemo ya World Economic Forum, Tanzania ni ya tisa duniani kwa ukuaji wa uchumi na kwa Afrika inashika nafasi ya tano kwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi.

Ameeleza kuwa hali nzuri ya ukuaji wa uchumi unaifanya Serikali kuendeleza mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, miundombinu, afya na nishati ili kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Miongoni mwa mageuzi makubwa yanayoendelea nchini ni pamoja na uchezi wa miundombunu kama reli ya kisasa ya Standard Gauge, ujenzi wa bwala kubwa la kuzalisha umeme wa megawati 2100 kutoka bonde la mto Rufiji na hivi karibuni ambapo Rais alizindua barabara ya Juu (Flyover) iliyopo TAZARA jijini Dar es Salaam.

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani utakaofanyika katika jimbo la Liwale na kwenye kata 37 leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani utakaofanyika katika jimbo la Liwale na kwenye kata 37.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria wakati wa mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Oktoba 13 mwaka huu.
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo, jijini Dodoma.
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi washiriki wa Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo, jijini Dodoma leo.





Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Oktoba 13 mwaka huu katika jimbo la Liwale na kwenye Kata 37 za Tanzania Bara wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni za uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi.


Jaji Mbarouk amewataka Wasimamizi hao kufanya kazi kwa ufanisi, uhuru, uwazi na bila kuegemea upande wowote ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.Amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.

“ Tunakutana hapa ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi, natumaini mtatumia fursa hii kubadilishana uzoefu katika kutekeleza jukumu hili lililo mbele yenu” Amesema Jaji Mbarouk.

Jaji Mbarouk ametoa wito Wasimamizi hao waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi akisisitiza kwamba katika kipindi hiki chaguzi zinafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya Kisiasa, kutoaminiana na wakati mwingine kutawaliwa na mihemko ambayo imekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.

Aidha, amewaeleza Wasimamizi hao kuwa wameaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo kwa kuwa wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi hivyo wajiamini na kujitambua.

Ametoa wito kwa Wasimamizi hao kuhakikisha kwamba wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi na wanawatumia vyema wasaidizi walio nao katika maeneo yao ya kazi kwa matokeo bora.“Naomba mjue mna jukumu la kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wote wa uchaguzi kwa Tume. Hivyo mfanye kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, bila kuegemea upande wowote.Kufanya kazi kwa uhuru na kwa uwazi kutasaidia kudumisha amani katika maeneo yenu ya Uchaguzi” Amesema.

Kuhusu kufanyika kwa Uchaguzi huo mdogo Oktoba 13 mwaka huu, Jaji Mbarouk amesema kuwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura 292, ni jukumu la Tume kusimamia, kuendesha na kuratibu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi.

Amesema kwa nyakati tofauti Tume imepokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika jimbo la Liwale.

Pia amefafanua kuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa, Sura, 292 alitoa taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 37 kutoka katika Halmashauri 27 zilizopo katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara.

Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mbarouk Salim Mbarouk ameeleza kuwa jumla ya wagombea 6 waliteuliwa kugombea ubunge katika jimbo la liwale ambapo mgombea mmoja alijitoa baada ya uteuzi huo kukamilika.Ameongeza kuwa katika Kata 37 za Tanzania Bara jumla ya wagombea 56 waliteuliwa kugombea udiwani katika Kata hizo.

WADAU WATAKIWA KUENDELEA KUFANYA TATHMINI YA ELIMU NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR –TAMISEMI), Selemani Jafo akifunga Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akitoa neno la Utangulizi wakati wa ufungaji wa Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.
Baadhi ya wadau wa elimu walioshiriki katika Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.

Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi walioshiriki kama Wadau wa Elimu katika Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Lydia Wilberd akitoa salamu za asasi hiyo kabla ya kufungwa kwa Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.



Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Wadau wa Elimu wametakiwa kuendelea kufanya tathmini ya elimu kwa kujadili mafanikio na changamoto za sekta hiyo ili kuboresha na kukuza elimu nchini.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Elimu.

Waziri Jafo amesema kuwa nchi nyingi ambazo hazina rasilimali za madini wala vivutio vya utalii zinaendelea kuwekeza katika rasilimali elimu ambapo baadae nchi hizo huwa tajiri na kutoa misaada kwa nchi masikini.

“Taifa linalowekeza vizuri katika sekta ya elimu ndilo Taifa lenye nafasi kubwa ya kukomboa wananchi wake na taifa kiujumla hivyo kutathmini juu ya elimu inayotolewa nchini kwetu ni jambo la muhimu sana”, alisema Jafo.

Waziri Jafo amewasisitiza wadau wa elimu walioshiriki katika mafunzo hayo kutekeleza maazimio yote yaliyoazimiwa kwenye kikao hicho ili kuendelea kutoa matokeo chanya katika sekta hiyo.

Vile vile ametoa rai kwa wadau wa elimu kuendelea kutoa michango yao ya hali na mali katika kuinyanyua sekta ya elimu nchini ili kwa pamoja taifa la Tanzania liweze kujinasua katika umasikini kupitia elimu.

Aidha, amewataka wadau wa elimu kuwa huru katika kutoa mawazo yao bila kuogopa na kuwahakikishia kuwa milango ya ofisi hiyo iko wazi kukubali changamoto mbalimbali zinazopelekwa na inaendelea kuzitatua.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu amesema kuwa kwa pamoja mkutano huo umejadili juu ya uboreshaji wa elimu nchini hasa juu ya suala la uwazi katika mipango na utekelezaji wa bajeti za elimu.

“Ili kuboresha sekta ya elimu nchini uwazi ni jambo la msingi hivyo tunawaomba wenzetu wa mashirika na taasisi tunaosaidiana katika sekta hii wajitahidi kuweka bajeti zao wazi kama Serikali inavyofanya ili kuboresha zaidi sekta hii”, amesema Dkt. Ave Maria.

Mkutano huo umeshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakurugenzi, Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Taasisi zisizo za kiserikali.

LUGOLA ATANGAZA OPERESHENI KUWAONDOA WAHAMIAJI HARAMU MKOANI KIGOMA, AWATAKA UHAMIAJI, POLISI WASHIRIKIANE



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalinzi, Wilaya ya Kigoma Vijijini wakati Waziri huyo alipofanya ziara wilayani humo kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wilayani humo. Waziri Lugola alitangaza operesheni kuanza kwa operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu mkoani Kigoma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga. Kulia ni Mwanasheria wa Sekretaireti ya Mkoa wa huo, Said Kamugisha. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiyaangalia majina ya watuhumiwa waliopo mahabusu katika Kituo cha Polisi Manyovu, wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma, alipokua anaonyeshwa na Askari Polisi wa zamu kituoni hapo, Peter Charles. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati) akiwahoji watuhumiwa (hawapo pichani) ndani ya mahabusu ya kituo cha Polisi Manyovu wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma, alipofanya ziara katika kituo hicho kujua utendaji kazi wa Polisi wa kituo hicho kilichopo mpakani na nchi ya Burundi. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Luteni Kanali, Michael Ngayalina, na nyuma yake ni Mkuu wa Kituo hicho, Nickobay Mwakajinga. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Na Felix Mwagara, MOHA-Buhigwe

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameitaka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma ishirikiane na Jeshi la Polisi kufanya operesheni maalum ya kuwaondoa wahamiaji haramu mkoani humo.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika uwanja wa Mnanila mjini Manyovu wilayani Buhigwe, leo, Lugola alisema anataarifa za kutosha kuhusu wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani wapo mkoani humo, hivyo lazima waondolewe kwa mujibu wa sheria.

Lugola ambaye alikua akishangiliwa na wananchi baada ya kutoa agizo hilo, pia alikemea tabia ya baadhi ya watu wanaohifadhi raia hao wa kigeni ambao wameingia nchini kinyume cha sheria.

“Sasa natoa agizo hili na litekelezwe, Uhamiaji mkoa washirikiane na polisi kuwaondoa raia hawa wa kigeni ambao wameingia nchini kwa njia zisizo halali, nataka operesheni hii ianze mara moja,” alisema Lugola.

Lugola pia aliirudia kauli hiyo ya kuondolewa kwa wahamiaji hao haramu alipokua anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalinzi, Wilaya ya Kigoma Vijijini, na kuongeza kuwa anashangaa wahamiaji hao wanaendelea kuwepo mitaani huku maafisa uhamiaji wakiwepo mkoani humo.

“Hivi inakuaje, wananchi wanalalamika hapa kuhusu uwepo wa wahamiaji haramu, lakini Uhamiaji mpo, mnakaa kimya tu, mnataka mpaka mimi nije ndio nitoe maelekezo haya? Hii sitaki kusikia tena, nataka operesheni hii ianza mara moja na iwe endelevu,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola alisema katika operesheni hiyo lazima maafisa wa uhamiaji wawe makini wakati wanawaondoa wahamiaji haramu pekee na sio kuwasumbua wananchi wa Kigoma ambao ni raia halali wa nchi hiyo.

Lugola alifafanua kuwa operesheni hiyo itasaidia kupunguza matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali mkoani humo ambapo kwa kiasi kikubwa hutekelezwa na wahamiaji hao haramu.

Aidha, Waziri Lugola akiwa wilayani Buhigwe, pia ametembelea kituo cha Polisi cha Manyovu kilichopo mpakani na nchi ya Burundi na kukagua utendaji kazi wa askari Polisi wa kituo hicho pamoja na kuiwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu kujua makosa yaliyowafanya wawepo ndani ya kituo hicho.

RAIS DKT MAGUFULI AMUAPISHA DKT NDUMBARO KUWA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018.
a (2)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akimkambidhi nyenzo za kazi baada ya kumuapisha  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018.
a (3)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akimkambidhi nyenzo za kazi baada ya kumuapisha  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018.
a (4)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Jaji Mstaafu Harold Nsekela akimuongoza  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kula kiapo cha maadili ya viongozi baada ya kumuapisha kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018.
a (5)
a (6)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiongea baada ya kumuapisha  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018
a (7)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiongea baada ya kumuapisha  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018
a (8)
a (9)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika  wa Bunge la Jamhuri Mhe. Job Ndugai na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi katika picha ya pamoja baada ya Dkt. Damas Daniel Ndumbaro  kuapishwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018.
a (11)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akifurahia jambo na viongozi wa CCM Mkoa wa Ruvuma  baada ya kumuapisha  Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 29, 2018  

Dkt. Abbasi, TAGCO Watembelea Kituo cha Radio cha Storm Mkoani Geita



Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiongea na watumishi wa kituo cha Redio cha Storm FM Mkoani Geita ambapo aliwasisitiza umuhimu wa kufanya kazi ya uandishi wa Habari kwa kuzingatia weledi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akishiriki Kipindi cha Moja kwa moja katika kituo cha Redio cha Storm FM Mkoani Geita ambapo aliongelea masuala mbalimbali ikiwamo miradi mikubwa inayotekelezwa na iliyotekelezwa na Serikali katika kipindi cha Miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi na viongozi wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa kituo cha Redio cha Storm FM Mkoani Geita
Mwenyekiti Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Bw. Pascal Shelutete akishiriki Kipindi cha Moja kwa moja katika kituo cha Redio cha Storm FM Mkoani Geita ambapo alisistiza kuwa wataendelea kuwajengea uwezo Maafisa Mawasiliano Serikalini na kuendelea kurahisisha uhusiano kati ya waandishi wa habari na Maafisa Habari wa Serikalini.
Katibu wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Bw. Abdul Njaidi akiongea na watumishi wa kituo cha Redio cha Storm FM Mkoani Geita ambapo ambapo aliwasisitiza kuhusu umuhimu wa kushiriki katika shughuli za maendeleo katika mkoa wa Geita.

Watumishi wa kituo cha Redio cha Storm FM Mkoani Geita wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alipokutana nao.