Thursday, September 20, 2018

TatuMzuka yazindua ‘jackpots’ mbili kubwa za kubadili maisha kila wiki

Wiki hii TatuMzuka imezindua jackpot ya Jumatano ikiwa ni jackpot ya pili ndani ya wiki moja. Watanzania sasa watapata fursa ya kuwa washindi wa jackpots mara mbili na hivyo kutengeneza washindi wengi zaidi kupitia jackpots.Jackpot ya jumatano ambayo itahusisha wachezaji wote waliocheza tangu jumapili itakuwa inaonyeshwa saa 3 usiku kupitia Clouds TV na EATV.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni hiyo, Bwana Sebastian Maganga alisema kampuni ya The Network ambao ni wamiliki wa mchezo wa namba wa TatuMzuka imekuwa ikiangalia namna ya kuongeza nafasi za Watanzania kushinda kwa wingi na kwa kiasi ambacho kinabadilisha maisha yao.

“Tangu tulipoanza mwaka mmoja uliopita tumetoa jackpot ya kihistoria ya milioni 300, na sasa kwa kuongeza jackpot ya jumatano watanzania hawatahitaji kusubiri wiki nzima kushinda, itakuwa sasa jumatano na jumapili” Alisisitiza Maganga

Baada ya uzinduzi huu, Tatumzuka sasa itaondoa jackpot ya kila siku ya Mzuka Deile na kuibadilisha na droo za vipindi maalumu ndani ya siku moja. Droo hizi zitatengeneza mamilionea wengi kwa haraka na kuufanya TatuMzuka kuwa mchezo unaotengeneza mamilionea wengi zaidi kuliko mchezo mwingine katika soko.

Akiongea wakati wa uzinduzi, balozi wa TatuMzuka Mussa Hussein (pichani) alisema hii ni fursa kubwa kwa watanzania kubadili maisha yao kupitia jackpots mbili kubwa kila wiki.

“Kwa tiketi moja ya shilingi 500 sasa Watanzania watakuwa wanasubiri kwa siku 3 tu kushinda kupitia jackpot za jumatano na jumapili. Hii itakata kiu ya wachezaji wetu wapendwa ya kusubiri muda mrefu kushinda kiasi kikubwa” Aliongeza Hussein

Ili kuongeza nafasi ya watanzania wengi kutazama shoo za jackpots Bwana Maganga alisisitiza kwamba The Network imeiongeza TBC1 kati ya vituo vitakavyokuwa vinaonyesha mubashara shoo ya jackpot ya jumapili.

AMANI CENTRE WAOKOA WATOTO 1200 WALIOKUWA WAKIISHI KATIKA MAZINGIRA HATARISHI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kituocha Amani (Amani Center for Street Children ) Meindert Schaap akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya wanafunzi wa Darasa la Saba waliokolewa na kituo hicho kutoka mitaani.


Mgeni rasmi katika Mahafali hayo ,Mratibu wa Elimu kata ya Karanga,Mercy Mandia akikabidhi zawadi kwa baadhi ya Wanafunzi walihitimu Darasa la Saba waliooklewa kutoka Mitaani na kupata msaada wa Elimu kutoka katika kituo hicho.
Mzazi Mwakilishi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho ,Editha Cyril akitoa neon la shukrani kwa msaada mkubwa uliotolewa kwa watoto hao.
Mtoto Getrude Salutary ,mmoja wa Wahitimu wa Darasa la Saba waliokuwa wakilelewa katika kituo hicho akisoma Risalambele ya mgeni rasmi,kushoto kwake ni mwanafunzi mwenzake ,Michael Salutary.

Kikundi cha Vijana wa Sarakasi wakionyesha umahiri katika mahafali hayo.
Watoto wanaolelewa katika kituo hicho wakionesha vipaji vyao katika uchezaji wa Muziki.
Watato hao wakionesha umahiri katika uchezaji wa ngoma za Asili.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.

WATOTO 1,200 waliokuwa wakiishi katika mazingra hatarishi mitaani wameokolewa na shirika lisilo la kiserikali la Amani (Amani Center for street Children) na kusaidia upatikanaji wa elimu kwa watoto hao na baadae kuwaunganisha na familia zao.

Watoto waliookolewa wakiwa katika umri tofati tofauti ,walichukuliwa na kituo cha Amani kutoka katika mitaa ya mikoa ya Singida,Moshi na Arusha ambapo mwaka huu watoto 31 kati ya kundi hilo wamehitimu elimu ya msingi baada ya kupata msaada wa kituo hicho.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya kuwaaga wanafunzi hao ,Mratibu wa Elimu wa kituo cha Amani Brenda Mzava alisema licha ya kuwaunganisha familia zao baada ya kuwalea watoto hao kwa muda mrefu, kituo bado kinaendelea kuwafuatilia na kuwasaidia hadi hapo watakapoweza kujiendeleza.

“Kama baadhi yetu tunavyojua watoto hawa walikuwa kwenye mazingira hatarishi na magumu ya mtaani kabla ya kuokoloewa na shirika la Amani, kwa kuwatoa mtaani,kuwapatia huduma na haki za msingi ikiwemo huduma za afya na elimu bora, siyo kazi rahisi hususani kwa motto aliyekuwa mtaani kwa muda mrefu.”alisema Mzava.

“Kazi hii haikuwa rahisi lakini kwa ushirikiano wa jamii pamoja na serikali hususani Manispaa ya Moshi kupitia shule ya Msingi Shirmatunda na Magereza jambo hili limewezekana hatimaye watoto 31 waliokuwa mtaani wamefanikiwa kuhitimu elimu ya msingi.”aliongeza Mzava.

Alisema kama shirika wanajivunia watoto hao kwa kuweza kuhitimu elimu yao ya msingi na kuwa ni mafanikio makubwa kwa shirika naTaifa kwa ujumla na kwamba ushirikiano uliopo kati ya shirika la Amani ,jamii na taasisi za Serikali ni wa pekee kwani unaogozwa na uwito pamoja na kujitolea.

“Kwa namna moja au nyingine tumewawezasha watoto hawa waliohitimu darasa la saba na wale tunaondelea kuwalea katika kituochetu kujenga msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye kielimu.”alisema Mzava.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mratibu wa Elimu kata ya Karanga Mercy Mandia alilipongeza Shirika la Amani kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwaokoa watoto toka kwenye mazingira hatarishi ya mtaani kisha kuwaweka sehemu salama na kuwapatia huduma za msingi ikiwemo Elimu.

”Niwapongeze shirika la Amani kwa kazi nzuri kwa kufanya watoto tunaoita wa mitaani kuwa watoto tena hasa kwa kuwapatia huduma za msingi kama malazi ,Chakula ,huduma za Afya,Elimu pamoja na mchakato mzima wa kuwarudisha kwenye jamii,”alisema Mandia.

“Nijitihada nzuri naomba kuahidi serikali kuanzia ngazi ya Mtaa,Kata,Manispaa pamoja na Mkoa kwa ujumla tutafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha kazi hii inafanikiwa kwa kiasi kikubwa”aliongeza Mandia.

Mandia alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa kituo hicho ,Meindert Schaap pamoja na wafanayakazi wote kwa kazi nzuri wanaoifanya yakufundisha ,kutunza,na kulea kiroho na kimwili watoto hao na kwamba Mungu ataibariki kazi hiyo na kukumbuka jitihada za kituo hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Amani ,Meindert Schaap alisema ni faraja kubwa kuona idadi kubwa ya watoto waliotoka mitaani wanaelekea kwenye mafanikio makubwa hasa baada ya baadhi yao kuhitimu elimu ya Msingi.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake , Joyce Faustine Ngada aliyekuwa akisoma shule ya msingi Magereza alikishukuru kituo cha Amani kwa kuwaokoa kutoka mazingira hatarishi ya mtaani na kuwaleta kituoni ambapo wamefanikiwa kupata huduma mbalimbali za msingi ikiwemo Elimu.

“Mimi nilichukuliwa nyumbani Bukoba na kuja kufanya kazi za ndani Moshi,baada ya kufika Moshi nilijikuta nafanya kazi tofauti ya ile niliyo ahidiwa wakati natoka nyumbani kwani nilijikuta nafanya kazi ya Baa”alisema Joyce.

Alisema kupitia muelimishaji mtaani wa Amani (Street Educator) alifanya nae mahojiano na kwamba awali alikuwa akimdanganya lakini nilipogundua anania njema ya kutaka kumuokoa alitoa ushirikiano na kuweza kutoka kwenye kazi ya kuuza Baa na kupelekwa katika kituo cha Shirika la Amani .

Amani Centre for Street Children ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 2001 na kusajiliwa baada ya kupewa namba NGO/0766 likifanya kazi ya kuwaokoa watoto wanaoishi mtaani kwa muda wote,katika miji ya Moshi,Arusha na Singida.

MAZISHI YA JOHN GUNINITA IFAKARA WILAYANI KOLOMBELO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala akimpa pole mdogo wa marehemu John Guninita Ndg Gerald John Guninita alipowasili nyumbani kwao Ifakara Wilaya ya kilombero.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala wakati akiwasili nyumbani kwao marehemu pamoja na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Ndg Innocent Karogelesi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala akizungumza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Ndg Innocent Karogelesi
Waombolezaji wakiandamana kutangulia mbele wakati mwili wa Marehemu John Guninita ulipokuwa ukipelekwa eneo la kusaliwa wakati wa mazishi hayo.
Muombolezaji Wakilia kwa uchungu wakati wa mazishi ya marehemu John Guninita.
Vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM wakibeba jeneza lenye mwili wa marehemu John Guninita kulipeleka kwenye eneo la kusaliwa wakati wa mazishi hayo.
Mwili wa Marehemu ukiwa umepakizwa kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa eneo la ibada 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl Raymond Mwangwala akitoa mkono wa pole kwa mdogo wa marehemu John Guninita Ndg Gerald John Guninita alipowasili nyumbani kwao Ifakara Wilaya ya kilombero.

Jeneza Lililobeba Mwili wa Marehemu Ndg John Guninita likiwekwa ndani ya Kaburi na Waombolezaji |(Picha Zote Na Fahadi Siraji Wa UVCCM)

VIJANA 4200 NCHINI KUNUFAIKA MRADI WA KILIMO KUPITIA KITALU NYUMBA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde akimwagilia bustani ya kijana Matogolo Samwel wa Kijiji cha Mwamanyili wilayani Busega, wakati wa Ziara ya kukagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vitalu nyumba mkoani Simiyu.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Vijana takribani 4200 hapa nchini wanatarajia kunuafaika na kilimo kupitia mradi wa kitalu nyumba(green house), ambao utaanza kutekelezwa katika mikoa sita ambayo imekuwa kinara kwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana, ukiwemo mkoa wa Simiyu na Halmashauri zake zote sita. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu,  Sera, Bunge,  Kazi ,Vijana Ajira  na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu yenye lengo la kukagua maeneo ya ujenzi wa vitalu nyumba na uwepo wa maji yatakayotumika katika  kilimo cha umwagiliaji.

Mvunde amesema katika kutekeleza mradi huo vijana watawezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili iwe sehemu ya ajira yao, ambapo vijana watafundishwa kulima kwa tija kupitia kitalu nyumba na kujua namna ya kutengeneza vitalu nyumba na wananchi wengine wanapohitaji kujifunza namna ya kutengeneza vitalu nyumba wajifunze kwao.

“Tutaleta green house (Kitalu nyumba) ambayo itafungwa hapa na vijana wataelekezwa kulima kupitia huko, lakini pia tutawaunganisha na chama cha Wauza mboga Tanzania kwa ajili ya kutengeneza masoko ya uhakika ili green house (kitalu nyumba) hizo ziwe na tija” alisema Naibu Waziri Mavunde
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde akikagua eneo litakalotumika kujenga vitalu nyumba Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Viwanja vya Nanenane Nyakabindi, wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo hayo mkoani Simiyu.

Akiwa katika ziara yake Naibu Waziri huyo amekutana na baadhi ya vijana ambao watatekeleza mradi huo na kuwapongeza kwa uamuzi waliochukua na akatoa rai kwa vijana wote nchini kuachana kukaa vijiweni na badala yake wajishughulishe na teknolojia hiyo ili waondokane na umasikini. Akiwa wilayani Busega, Bariadi na Itilima Mavunde ameeleza kuridhishwa kwake na maeneo yaliyotengwa na akatoa wito kwa viongozi wote kuwalea vijana wote watakaoanza kutekeleza mradi huo ili mradi huo uweze kuwa endelevu na uweze kuwaletea tija.

Mkuu wa Mkoa wa Mhe. Anthony Mtaka  ameishukuru Serikali kwa mpango huo ambao utawasaidia vijana kujiajiri kupitia vitalu nyumba na akamhakikishia Naibu Waziri kuwa mkoa wa Simiyu utahakikisha vijana wanafanya vizuri katika mradi huo

Mkuu wa wilaya ya Itilima amesema pamoja na vijana wilayani humo kujiandaa na mradi wa kilimo kwa kutumia kitalu nyumba Wilaya hiyo pia imeweka mpango wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na ufundi stadi yatakayowawezesha kupata maarifa ya namna ya kufanya shughuli za ujasiriamali na ufundi kama ajira zao.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhandisi. Mohammed Ali akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde(mwenye miwani) juu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kitalu nyumba lililopo Mwamanyili, wakati akiwa katika zi ara ya kukagua maeneo hayo mkoani Simiyu.

Kwa upande wao vijana watakaofaidika na mradi wa kitalu nyumba wamesema wanaupokea mradi huo kwa mikono miwili na wakaomba Serikali iwasaidie kupata mikopo ili waweze kununua vifaa vya kisasa hususani mashine na zana za kilimo zitakazowawezesha kutekeleza mradi huo.

“Mradi huu sisi vijana tunaupokea kwa mikono miwili ombi letu kwa serikali tusaidiwe mikopo itakayotuwezesha kupata mtaji utakatufanya vijana tunufaike na kilimo, tupate vifaa bora kama mashine za kumwagilia na zana nyingine za kilimo ili tuweze kulima kisasa” alisema Matogolo Samwel kutoka Mwanyili wilayani Busega.

Katika ziara hiyo Mavunde ametembelea Halmashauri ya wilaya ya Busega, Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika  viwanja vya nane nane Nyakabindi na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima makao makuu ya Wilaya Lagangabilili.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde( wa pili kulia mbele) akizungumza na viongozi na baadhi ya Vijana wa Itilima, alipotembelea eneo la ujenzi wa Vitalu Nyumba Lagangabilili akiwa katika ziara ya kukagua maeneo hayo mkoani Simiyu.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu(baadhi hawapo pichani) mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara ya kukagua maeneo yaliyotengwa kujenga vitalu nyumba mkoani humo, (kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza wakati ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde, aliyofanya mkoani humo kwa ajili ya kukagua maeneo ya kujenga vitalu nyumba.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde(mwenye miwani), Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga(katikati) na Mkuu wa Wilaya ya  Itilima, Mhe. Benson Kilangi(kulia) wakifurahia pamoja na wanafunzi wa Shule ya sekondari Kanadi na baadhi ya viongozi wa Mkoani Simiyu wakati Naibu Waziri Mavunde akiwa katika ziara ya kukagua maeneo ya kujenga vitalu nyumba mkoani Simiyu.

MAGAZETI YA LEO ALHAMISI SEPTEMBA 20, 2018
Wednesday, September 19, 2018

Dkt. Gwajima azindua ziara ya kitabibu Wilayani Kondoa

Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akihutubia kwenye uzinduzi wa ziara ya Madaktari Wauguzi kutoka taasisi binafsi ya Health Education Development (HEAD INC) ya watanzania waishio nchini Marekani ya kutoa huduma za kitabibu kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa. Dkt. Gwajima alitumia fursa hiyo kuwapongeza taasisi hiyo kwakuona umuhimu wa kuja nyumbani kutoa huduma za afya kwa watanzania wenzao. Dkt. Gwajima hakusita kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Diaspora kwa kuwezesha kufanikisha Ziara ya Madaktari na Wauguzi hao kutoka Nchini Marekani ambapo inaonyesha namna mwitikio wa Watanzania waishio nje ya nchi katika kuchangia maendeleo nchini. Madaktari na Wauguzi hao watakuwa kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa siku nne (4) wakitoa huduma za Afya kwa wagonjwa mbalimbali. 
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta (wa kwanza kushoto), na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Anisa Mbega wakimsikiliza kwa makini Dkt. Gwajima alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa ziara ya Madaktari na Wauguzi kutoka (Head Inc).
Sehemu ya Watumishi kutoka wilaya ya Kondoa wakimsikiliza kwa makini Dkt. Gwajima alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa Ziara ya Madaktari na wauguzi.
Sehemu ya Wananchi waliojitokeza kwenye Ufunguzi huo wakimikiliza kwa makini Dkt. Gwajima 
Mkuu wa Wilaya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta naye alipata fursa ya kuwakaribisha Madaktari na Wauguzi hao kwenye Wilaya ya Kondoa na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa kipindi chote cha siku nne watakachokuwa wanatoa huduma za Afya katika Hospitali hiyo. 
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Anisa Mbega naye alipata Fursa ya kuwasalimia wananchi wa Wilaya ya Kondoa walio jitokeza kwenye Uzinduzi wa Ziara hiyo ya Madaktari na Wauguzi, pia alitumia fursa hiyo Kuwashukuru wanadiaspora kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya nchini kwa namna mbali mbali ikiwemo kuleta ujuzi wao, kuwekeza kwenye sekta mbalimbali. Pia aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Kondoa kupitia Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta kwa maandalizi na mapokezi mazuri ya ziara hiyo. 

Juu na chini sehemu ya wananchi wakiendelea kusikiliza hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye uzinduzi huo.

Juu na chini sehemu ya wananchi wakianza kupata huduma za kiafya mara baada ya kufanyika kwa uzinduzi huo.

Picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi.
Balozi Anisa Mbega akiagana na Dkt. Gwajima mara baada ya kumaliza ufunguzi wa Ziara ya Madaktari na Wauguzi.