Sunday, December 31, 2017

SALAMU ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA Dkt. Faustine Ndugulile

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya 2018. Hii ni neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu  ametujaalia  kwani kuna wengi walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni nyote kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa huduma za afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu na uadilifu licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.  Nami nawatia shime na hamasa ili muendelee na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua kuwa  Sera yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi pamoja na yale ya Taifa.  Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha na kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara yangu. Jambo hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la minong’ono, manung’uniko na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya  watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au miiko ya kazi zao na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo yatakayoweza kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya kupitia Watoa Huduma za Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo linatokea.
  • Wanataaluma wa Afya:
Nawakumbusha Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi, Wakunga, Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na Wafiziotherapia,  kwamba taaluma hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza yamejengwa  katika  misingi ya kuaminiwa (Trust) na Jamii, na kwamba  kuaminiwa  huko ndio kiini cha heshima ya taaluma hizi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma kutekeleza majukumu yake akiongozwa na msingi huu mkuu, pamoja na misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI, UAMINIFU, USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha, naendelea kuwakumbusha kuwa, utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama. Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika  utekelezaji wa wajibu wenu kama wanataaluma ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote wanaokuja mbele yenu kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa siku zote mnao wajibu wa kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa kuzingatia Sheria nyingine za nchi,  Kanuni, Sera, pamoja na  Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko  ya Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha, nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya Afya kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma wote walio chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi (Professionalism) pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na kuchukua hatua stahiki za nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana wajibu wa kuhakikisha kuwa Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao kwa misingi hii iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi iharibiwe na wakorofi wachache miongoni mwenu.
  • Mabaraza ya Taaluma
Natumia fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya Wizara yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria zinazosimamia Wanataaluma wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa  mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu na ujuzi  unaokubalika, na atambulike kwa kupewa usajili na leseni ya kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona kuwa jamii inapata huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika. Hivyo, Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.
  • Wanajamii
Napenda kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya zilizo salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na zinazozingatia heshima na utu wa binadamu.  Pia, mnayo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri au tiba kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa misingi ya Sheria za Nchi.  Kati ya vitendo visivyo kubalika ni pamoja na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi, dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya simu za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.
Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
  • Wanataaluma na Watoa Huduma,
  1. Kila Mwanataaluma na mtoa huduma anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili  wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
  2. Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa kazi ipasavyo.
  3. Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.
  1. Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au malalamiko.
  2. Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).
  • Mabaraza ya Taaluma
Kila Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika Wilaya, Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu dhidi ya wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na anuani za barua pepe (e-mails).
  • Wanajamii kwa ujumla:
    1. Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
  • Nawasihi wanajamii wote kutoa taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
  • Uongozi wa kituo husika,
  • Mganga Mkuu wa Wilaya,
  • Mganga Mkuu wa Mkoa,
  • Ofisa wa TAKUKURU,
  • Baraza la Taaluma Husika,
  • Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
  • Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
  • Kiongozi yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.
Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.
Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO.
31/12/2017.

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) MKOA WA SINGIDA CHAZINDUA KAMPENI ZA UCHAGUZI MDOGO



Baadhi ya wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida kaskazini wakiwa kwenye viwanja vya mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mtinko,singida vijijini juzi.
Baadhi ya wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida kaskazini wakiwa kwenye viwanja vya mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mtinko,singida vijijini juzi.
Naibu katibu Mkuu wa CCM Tanzania bara,Rodrick Mpogolo akizindua kampeni za uchaguzi mdogo wa CCM katika jimbo la Singida kaskazini zilizofanyika juzi katika Kijiji cha Mtinko,singida vijijini. 
Mgombea wa kiti cha ubunge wa jimbo la Singida kaskazini,Justine Monko akiwa tayari amepokea ilani ya chama kwa ajili ya kutekeleza yaliyoainishwa ndani ya ilani hiyo.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)



Na,Jumbe Ismailly SINGIDA 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimezindua kampeni zake za uchaguzi mdogo katika jimbo la Singida Kaskazini na kusisitiza juu ya kudumisha amani,utulivu na mshikamano uliopo hapa nchini.

Akizindua kampeni hizo zilizofanyika katika Kijiji cha Mtinko,Singida Vijijini,kwa niaba ya Katibu mkuu wa CCM taifa,Naibu katibu mkuu wa CCM,Tanzania bara,Rodrick Mpogolo alisema idadi kubwa ya wananchi wameendelea kukichagua chama cha mapinduzi kutokana na kuwa na mipango mizuri ya maendeleo.

Alizitaja sababu zingine kuwa ni chama chenye historian a pia kina awamu tano za uongozi na kwamba ni chama kilichokomaa na endapo kitakabidhiwa nchi au ukikabidhi madaraka,watakuwa na uhakika kwamba madaraka hayo yameshikwa na watu waliokomaa.

Kwa mujibu wa Naibu katibu mkuu huyo wakati wote CCM imekuwa ikishughulikia kero za watu na kwa hivi sasa inayo matumaini makubwa ya kubadilisha maendeleo ya nchi na kwamba hivi sasa rais wan chi amekwisha hamisha makao makuu ya serikali yake Mkoani Dodoma,jirani kabisa na Mkoa wa Singida.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi pamoja na kuwashawishi wananchi wa jimbo la Singida kaskazini kumchagua mgombe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini hakusita pia kutaja utekelezaji unaofanya na serikali ya chama hicho kwa hivi sasa.

Dk.Nchimbi ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa wa Singida aliweka bayana kwamba mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya pili nay a tatu umeshaanza na tayari zaidi ya shilingi bilioni 71.3 zinatarajiwa kutumika kusambaza nishati hiyo katika vijiji vyote.

“Kwa hivyo nawaombeni wananchi wa jimbo la Singida kaskazini mchagueni mgombea wa CCM kwani mkimleta mtu mwingine haijui ataanza kwanza kujifunzafunza atatuchelewesha,kwa hiyo mleteni Monko ili aendeleze utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)”alisisitiza Dk.Nchimbi.

Akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa CCM,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,Juma Hassani Kilimba alisema kutokana na wingi wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo,unadhihirisha wazi kwamba wao tayari kumchagua mgombea huyo wa CCM ifikapo jan,13,mwaka ujao.

Hata hivyo Kilimba alisisitiza huku akijinasibu kwamba chama hicho hakina wasiwasi juu ya kushinda katika uchaguzi huo mdogo kutokana na serikali ya chama hicho kujishusha kwa wananchi wa ngazi za chini.Naye mgombea wa chama hicho Justine Monko kwa upande wake amewahakikishia wakazi wa jimbo hilo kwamba hataweza kuwaangusha endapo watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao kwa kumchagua kwa kura za kutosha na za kishindo na hatasita kuwatumikia kwa weledi wa hali ya juu.

“Namshukuru sana Rais wetu Dk.John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Liwale,kanipa nafasi hiyo nimejifunza mengi sana pamoja na namna bora ya kuwatumikia wananchi”alisisitiza Monko.

Rais wa Zanzibar Dk. Shein, Ashiriki Katika Zoezi La Usafi Wa Mazingira Katika Nyumba Za Wazee Sebleni Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akishiriki katika zoezi la Usafi wa Mazingira katika eneo la Nyumba za Wazee Sebleni na kujumuika na Wananchi katika zoezi hilo, kulia Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, akishiriki katika zoezi la kufanya usafi katika Nyumba za Wazee Sebleni Unguja, kulia Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee Vijana Wanawake na Watoto Zanzibar, Mhe. Maudline Cyrus Castico.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Wazee wanaoishi Nyumba za Wazee Sebleni alipofika katika viwanja hivyo kwa ajili ya Uzinduzi wa Usafi wa Mazingira katika eneo hilo
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akimkabidhi Vifaa vya Usafi Katibu wa Baraza la Vijana Wilaya ya Magharibi A Unguja Farida Juma, kwa ajili ya zoezi la Usafi katika Wilaya yao, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Nyumba za Wazee Sebleni wakati wa Uzinduzi wa Zoezi la Usafi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na Viongozi wa meza kuu wakiwa wamesimama kwa dakika moja kuwakumbuka Wazee waliotangulia mbele ya haki.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Usafi wa Mazingira katika viwanja vya Sebleni Unguja
BAADHI ya Vijana wanaoshiriki katika zoezi la Usafi wa Mazingira katika eneo la Sebleni Nyumba za Wazee wakifanya usafi
WAZEE wa Sebleni wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi wa usafi wa mazingira katika maeneo ya nyumba za wazee sebleni Unguja.
VIJANA wa Mabaraza ya Vijana ya Mkoa wa Mjini Magharibi na Wananchi wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa usafi wa mazingira katika eneo la Nyumba za Wazee Sebleni, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla hiyo
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Hamida Mussa Khamis akisoma risala ya Mkoa wakati wa Uzinduzi wa Usafi wa Mazingira katika viwanja vya Nyumba za Wazee Sebleni Unguja.
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, akizungumza na Wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kabla ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuzungumza na Wananchi walioshiriki kazi ya Usafi wa Mazingira katika viwanja vya Nyumba za Wazee Sebleni.
Picha na Ikulu

MKOA WA PWANI UMEUZA TANI 19,815 ZA KOROSHO NA KUPATA BIL.39-RC NDIKILO

MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, ambae pia ni mkuu wa Mkoa huo, mhandisi Evarist Ndikilo , akizungumza na baadhi ya wakulima wa korosho wakati alipotembelea ghala moja lililopo wilayani Mkuranga.Picha na Mwamvua Mwinyi



Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga

MKOA wa Pwani ,tayari umeuza tani 19,815 ambazo zimeingiza zaidi ya bilioni 39 tofauti na msimu uliopita ambapo uliuza tani 13,000 na kupata bilioni 33.##

Mkoa huo umejiwekea lengo la kuuza tani 25,000 hadi 30,000 kwa msimu huu ambao minada yake ya korosho ikiwa bado inaendelea .Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,aliyasema hayo Mkuranga ,wakati akizungumzia changamoto na mafanikio waliyoyapata msimu wa korosho 2017/2018 .

Alieleza ,mbali ya hayo wakulima wa korosho mkoani Pwani wakiwa bado wanadai zaidi ya bilioni tano.Mhandisi Ndikilo alisema ,kuuza tani 19,815 hadi sasa ni mwanzo mzuri wa kufikia malengo yao waliyojiwekea msimu huu.Alisema ,hatua hiyo imetokana na serikali kutoa pembejeo bure katika msimu huu na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Alibainisha ,licha ya mafanikio hayo lakini kuna changamoto zimejitokeza tangu kuanza kwa minada mwaka huu ikiwemo uhaba wa magunia .Kero nyingine ni ile iliyojitokeza sasa ya kuchakachua ubora wa korosho unaofanywa na baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).

“Changamoto ya magunia inaweza kuwa historia endapo tutakubaliana kwa kukaa na mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha wawekezaji waje wawekeze kiwanda cha magunia lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo hili” alifafanua .Akizungumzia kuhusu tatizo la ubora wa korosho, mhandisi Ndikilo ,alisema baadhi ya Amcos zimejiingiza kwenye kuhujumu minada hiyo kwani baadhi yao wameweka michanga na mawe kwenye magunia ya korosho .

Alisema huo ni wizi,uhujumu uchumi na kuaibisha sifa ya nchi ya Tanzania nje ya nchi kwani magunia hayo yangefika India na nchi nyingine ingekuwa aibu na fedheha.Kutokana na upuuzi huo ndio maana nimeamua kutoa maagizo kuwa Amcos 10 zilizojihusisha na ubabaishaji huo viongozi wake wakamatwe na kuhojiwa.

Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo ,kuwepo kwa maghala makubwa itainua soko la korosho msimu ujao na kuondoa ubabaishaji wa maghala ya vichochoroni yanayoleta dosari .Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mkombozi kwa wakulima hivyo anawashangaa wale wanaobeza na kuyumbisha mfumo huo.

Mhandisi Ndikilo ,aliwataka wakulima wa korosho kuacha kukubali kurubuniwa na madalali ama wanunuzi wachache hali inayosababisha kukosa mapato kulingana na korosho zao.Serikali mkoani humo imewatoa shaka wakulima wa korosho ambao bado hawajalipwa fedha zao na kudai itasimamia makampuni na wanunuzi kulipa kwa wakati na changamoto zinazojitokeza

NAIBU WAZIRI ULEGA AAGIZA WATENDAJI WA VIJIJI NA WENYEVITI KUWASOMEA MAPATO NA MATUMIZI WANANCHI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akizingumza na wananchi wa kijiji cha Kiziko alipofanya ziara katika jimbo la Mkuranga.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mkuranga, Juma Abeid akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiziko juu ya mikakati ya Halmashauri katika uboreshaji wa sekta mbalimbali.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwasili katika kijiji cha cha Kitonga katika ziara ya vijiji jimbo la Mkuranga. 


Na Chalila Kibuda,Globu ya jamii.

NAIBU waziri wa Mifugo na Uvuvi (Mbunge) wa Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani Abdalla Ulega ametoa agizo kwa Watendaji wa vijiji na Wenyeviti kuwasomea mapato na matumizi wananchi wao ili kuepuka kurudisha nyumba uchangiaji wa shughili za maendeleo.

Naibu waziri huyo ametoa agizo hilo wilayani humo akiwa katika mwendelezo wa ziara za vijijini ambapo akiwa katika kijiji cha Kiziko, kilichopo Kata ya Mwarusembe baada ya kupokea malalamiko ya wananchi juu ya viongozi wao ngazi ya kijiji kushindwa kusoma taarifa ya mapato na matumizi.

Alisema kushindwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kunachangia kwa asilimia kubwa wananchi kushindwa kuchangia maendeleo katika maeneo hayo hivyo lazima wananchi wajulishe kinachoingia na kinavyotumika.

"Natoa agizo hili kwa watendaji na wenyeviti kusoma mapato na mapato na matumizi na hapa naagizi mtendaji wa Kata ya Mwarusembe kuhakikisha hadi kufika Januari 2 ,2018 niwe nimepata taarifa za kushindwa kusoma mapato na matumizi katika kijiji hiki cha kiziko. "alisema Ulega

Alisema wananchi wanatamani kujitolea kwa lengo la kuchangia maendeleo lakni wanavunjwa moyo viongozi hao huku akisisitiza kupewa ifika January 2 awe amepata taarifa nakuhaidi kulifuatilia jambo hilo kwa ukaribu zaidi.

Pia akiwa katika kijiji hicho cha alitoa mifuko 50 ya saruji pamoja na shilingi laki tano kwa ajili kuchangia ujenzi ya serikali ya kijiji hicho ikiwa pamoja na matundu ya vyoo katika shule ya msingi kiziko huku akitoa ahadi ya shilingi tisa. Kwa ajili ya kuchangia vikundi tisa vya Vikoba.

Awali wakitoa kero zao kwa Mbunge huyo walisama wamakerwa sana na kukithiri kwa mifugo aina ya ng'ombe hali inayosababisha umasikini na njaa kwa wananchi hao kutokana na mazao yao.Pia walilalamikia kukosekana kwa barabara, inayounganisha kijiji hicho cha kiziko na vijiji vingine pamoja na Daraja linalounganisha vitongoji vya Gwanzo, Chakande vyenye wakazi wengi zaidi.

"kwakweli tuna kero nyingi mno hapa kijijini kwetu kwani mbali na barabara na Daraja lakini pia tunakero ya kukosa Daktari kwenye Zahanati hii yetu hali inayosababisha wananchi kukosa kupatiwa huduma stahiki. "alisisitiza Mojamed Ally mjumbe wa serikali ya kijiji.

Naye Ofisa Kilimo wa Kijiji hicho... Alisema wananchi hao ambao waliowengi ni wakulima lakini wanakosa dhana za kisasa za kilimo pamoja na ukosefu wa gereta ili kusikuma maji kwenye kisima cha maji kilichopo shule ya msingi kiziko ili wanafunzi na raia wengine wapate maji.

Mbali na kijiji hicho pia Naibu waziri Ulega aliendelea na ziara katika kijiji cha Kitonga kata hiyo ya Mwarusembe ambapo pia alipokea kero ya kuvamiwa na ng'ombe kwenye mashamba ya wananchi huku wakimtaka kumaliza kero hiyo.

Wakati huohuo wananchi hao walilalamika kwa Kiongozi wao huyo juu ya kutoridhishwa na huduma zinazotolewa katika Hospitali ya wilaya hiyo nakudai kwamba wakinana mama wanapohitaji kujifungua kuambiwa wabebe vifaa vya uzazi mbali Serikali kusema huduma hiyo bure.

"Naibu waziri kwakweli wananchi wako sisi tunaumia. Pale Hospitali ya Wilaya ya mkuranga ni tatizo bado panafigisu na kona kona nyingi tunaomba tusaidie. "alisema mmoja wa wananchi katika mkutano huo.

WAZIRI NDALICHAKO ATEMBELEA SHULE YA SEKONDARI MAGUFULI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA LIPA KWA MATOKEO (P4R)

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Pro.Joyce Ndalichako amefanya ziara fupi Wilayani Chato kwa kuitembelea Shule ya Sekondari Magufuli na kukagua utekelezaji wa miradi ya lipa kulingana na matokeo(P4R) shuleni hapo.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa mabweni, Bwalo, vyoo na vyumba vya madarasa Profesa Joyce Ndalichako ameupongeza Uongozi wa Mkoa, Halmashauri ya Chato na Shule ya Sekondari Magufuli kwa kusimamia vizuri fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kwa ubora na kiwango kinachotakiwa.''Nafurahi kuona fedha za P4R zinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa kama tulivyokagua na kujionea kiwango kilichojengwa ndio haswa kinachotakiwa ambacho darasa lazima liwe na silling bodi, umeme lakini pia liwe na madirisha tofauti na madarasa tuliyokuwa tunajenga zamani hivyo nawapongeza kwa dhati kabisa viongozi mmefanya kazi kubwa thamani ya fedha inaonekana''.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondari Magufuli.

Profesa Ndalichako amesema Serikali ya awamu ya tano inajukumu kubwa la kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora katika utoaji wa elimu hivyo miradi ya namna hii inatekelezwa katika Halmashauri nchi nzima. Amesema mwezi desemba 2017 serikali imetoa kwa halmashauri zote shilingi bilioni 15 na milioni 900 za kuendeleza jitihda za kuimarisha miundombinu ya sekta ya elimu ili kuongeza na kuimarisha majengo kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa darasa la kwanza ambapo zitajenga jumla ya madarasa 415, mabweni 46, matundu ya vyoo 814 na mabwalo 7.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amempongeza Waziri wa elimu kwa kutembelea shule hiyo ili kujionea kazi nzuri iliyofanyika licha ya kuwa na majukumu mengi ya kitaifa. Amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Geita kwa jitihada zao za kushiriki katika ujenzi wa nyumba vya madarasa 8000 kwa shule za msingi na Sekondari ambapo tangu mkoa uzindue kampeni ya ujenzi huo zaidi ya vyumba 900 vya shule za msingi na zaidi ya 130 vya Sekondari vipo katika hatua tofauti. Amesisitiza kuendelea kuunga mkono jitihada zao kwa kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika michango inayotolewa na wananchi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akiwa na viongozi wa Mkoa wa Geita wakati wa kukagua vyumba vya madarasa.

Mhandisi Robert Gabriel amemhakikishia Waziri wa Elimu kuwa pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi walioandikishwa kujiunda na elimu ya awali, darasa la kwanza na Sekondari hakutakuwa na mwanafunzi atakaye kaa nje ya darasa kwa kuwa jitihada za zinafanyika kwa haraka ili kukabiliana na hali hiyo.

Akiwa katika shule hiyo Mheshimiwa Waziri wa elimu alikagua ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa, matundu 20 ya vyoo, mabweni 2 ya kulala wanafunzi na bwalo miradi yote hii imetekelezwa na Serikali kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo kwa gharama ya shilingi 570,500,000/=.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bwanga wakati wa Ziara yake katika shule ya Magufuli Sekondari.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi akizungumza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Magufuli Sekondari.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mheshimiwa Shaban Ntarambe akizungumza na wananchi (awapo kwenye picha) wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu Wilayani Chato.
Muoenako wa Jengo hilo.

NIDA YATAJA MIKOA INAYOFANYA VIZURI ZOEZI LA USAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA

Mhe.Dkt Mwigulu L.Nchemba akikagua baadhi ya Vitambulisho 3470 ambavyo watagawiwa wananchi wa Kata ya Songea ambao Usajili wao umekamilika kufuatia zoezi la Usajili Vitambulisho kuwa kufanyika katika Kata za karibu kabla ya kuanza Usajili wa Umma. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida Ndugu Andrew W. Massawe.

Mhe Waziri akimkabidhi Kitambulisho chake mmoja wa wananchi wa Kata ya Songea Bwana Hassan Ally Shomari wakati wa zoezi la ugawaji Vitambulisho kwenye sherehe za uzinduzi wa zoezi la Usajili kwa mkoa wa Ruvuma. Jumla ya Vitambulisho 3470 viligawanywa kwa wanachi wakati wa sherehe hizo.






kikundi cha burudani za asili maarufu kama wana Lizombe wakitumbuiza wakati wa sherehe za uzinduzi wa zoezi la Usajili kwa mkoa wa Ruvuma.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt Mwigulu L.Nchemba akiwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Ndugu Andrew W. Massawe wakiwasili kwenye viwanja vya Lisaboni –Songea kushiriki sherehe za uzinduzi wa zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa mkoa wa Ruvuma.

……………………………………………………………………………………

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Ndg Andrew W. Massawe ameitaja mikoa ya Mara, Arusha, Iringa, Geita, Lindi, Simiyu, Mbeya na Songwe kuwa mikoa inayoongoza katika zoezi la kuwasajili wananchi kupata Vitambulisho vya Taifa; huku mikoa mingine ikiwa nyuma kiusajili kulinganisha na malengo waliyowekewa.

Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa zoezi la usajili kwa mkoa wa Ruvuma lilofanyika katika viwanja vya Lisaboni-Songea, Ndugu Massawe amemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Nchemba kusaidia kuweka msukumo kwa viongozi na wananchi kwenye mikoa ambayo haifanyi vizuri ili iongeze kasi ya usajili kwa lengo la kukamilisha usajili kwenye mikoa yao kwa muda uliopangwa.

Akihutubia wananchi wa Ruvuma waliofurika kwenye viwanja vya Lisaboni vilivyopo nje kidogo ya mji wa Songea, Waziri wa Mambo wa Ndani ya Nchi Mhe.Dkt Mwigulu Lameck Nchemba amewasisitizia wananchi kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kwani kuwa na kitambulisho cha Taifa siyo suala la hiyari ni wajibu kwa kila Mtanzania mwenye sifa kuwa nacho.

“ Mhe. Rais wetu ametoa hela za kuwasajili, zoezi ni bure bado kujisajiliwa kwenda kupigwa picha na kuchuliwa alama za vidole ikushinde?” aliuliza Waziri huyo mwenye dhamana kubwa katika kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo.

Aidha amewataka viongozi wa Mikoa na wote wenye dhamana katika kusimamia zoezi hili kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika kuhakikisha wananchi wenye sifa wanasajiliwa na kamwe pasiwepo wageni watakaojipenyeza kusajiliwa Vitambulisho vya Taifa kama raia.

“Kwakuwa NIDA inatoa vitambulisho vya aina tatu, cha Raia, Mgeni na Mkimbizi basi niwaombe wageni badala ya kufanya udanganyifu wajisajili kwa hadhi yao kwani siyo dhamira ya Serikali kumfukuza yeyote lakini kuwatambua Raia wake kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani” alisema

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme amemhakikishia Mhe. Waziri mkoa wake uko tayari kusimamia na kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanasajiliwa na kupata Vitambulisho ndani ya muda uliopangwa na kwamba kamwe hata mvumilia mtu yeyote ambaye atakuwa kikwazo katika utekelezaji wa zoezi hilo kwa wananchi; akiwakemea wanasiasa kuingiza siasa kwenye zoezi la Usajili wananchi vitambulisho vya Taifa.

Mkoa wa Ruvuma wenye Wilaya 5 unakisiwa utawasajili zaidi ya wananchi 900,000 katika zoezi lililopangwa kumalizika ndani ya miezi mitatu. Tayari NIDA imekamilisha usambazaji wa vifaa na kutoa mafunzo kwa maafisa ambao watatumika kuwasajili wananchi wa Ruvuma na viunga vyake.

Mikoa mingine inayoendelea na Usajili kwa sasa ni Iringa, Mbeya, Njombe, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara, Songwe, Lindi na Mtwara.

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA AMEHUTUBIA BARAZA LA KUFUNGA MWAKA 2017 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2018 JIJINI MBEYA

Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akiongoza Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018. Baraza hilo limehudhuriwa na Maafisa na Askari kutoka vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani Mbeya, Chuo cha Magereza Kiwira na Chuo cha Ufundi Mbeya ambapo Baraza hilo limefanyika leo Desemba 31, 2017 katika Viwanja vya Magereza Mkoani Mbeya.
Baadhi ya Askari wa kike wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali vya Magereza ya Mkoa wa Mbeya wakisikiliza hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(hayupo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018.
Wakuu wa Magereza yaliyopo Mkoani Mbeya wakifuatilia kwa umakini mkubwa maelekezo ya Kamishna Jenerali wa Magereza aliyoyatoa katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018.
Mkuu wa Magereza Mkoani Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Kijida Mwakingi akitoa taarifa fupi ya Mkoa wake katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018.
Naibu Kamishna wa Magereza, Tusekile Mwaisabila akitoa ufafanuzi wa masuala yahusuyo Divisheni ya Huduma za Urekebishaji mbele ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa pili kulia) katika Baraza la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018 (wa kwanza kushoto) ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Mbaraka Semwanza. Baraza hilo limefanyika katika Viwanja vya Magereza Mkoani Mbeya.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu katika Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Chacha Binna akitolea ufafanuzi kuhusiana na masuala ya madeni ya watumishi yaliyoulizwa na Maafisa na Askari wa Jeshi hilo Mkoani Mbeya(hawapo pichani) katika Baraza hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akipokea salaam ya heshima kutoka kwa gwaride maalum alipowasili katika Viwanja vya Magereza Mkoani Mbeya kabla ya kuhutubia Baraza la Maalum la Maafisa na Askari kutoka vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani Mbeya, Chuo cha Magereza Kiwira na Chuo cha Ufundi Mbeya ambapo Baraza hilo limefanyika Desemba 31, 2017.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akikagua gwaride la Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kabla ya kuhutubia Baraza Maalum la Maafisa na Askari wa Jeshi hilo lililofanyika katika Viwanja vya Magereza Mkoani Mbeya leo Desemba 31, 2017(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

WATALII WA NJE NA NDANI WAENDELEA KUMIMINIKA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI

Watalii wakiwasili uwanja mdogo wa ndege wa Seronera wilayani Serengeti mkoa wa Mara uliopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Senapa) kwaajili ya kutembelea vivutio vya kitalii wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Watalii wakiwasili uwanja mdogo wa ndege wa Seronera wilayani Serengeti mkoa wa Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,kukamilika kwa jengo la wageni wanaowasili na wanaondoka kumerahisisha huduma za usafiri ndani ya hifadhi hiyo.
Afisa Utalii Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti mkoa
wa Mara,Susuma Kusekwa akizungumza na watalii waliotembelea hifadhi hiyo.
Watalii wakimsikiliza Zacharia Mathayo ambaye ni mwongoza watalii wakati akitoa maelezo kuhusu uhamaji wa wanayamapori aina ya Nyumbu kutoka Kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti hadi Kusini.
Watalii hufurahia kuona wanyama wakubwa wakiwemo Tembo na wengine wanaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Tembo ni mojawapo ya kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.
Wanyama wadogo aina ya Pimbi ni sehemu ya vivutio utakavyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Wanyama wadogo aina ya Pimbi ni sehemu ya vivutio utakavyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imefanikiwa kutangaza vivutio vyake kikamilifu sio kwa watalii wanaotoka mataifa ya Ulaya,Asia na Amerika pekee bali pia watalii wa ndani ni sehemu ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.
Makundi makubwa ya Simba kama hili utayaona ndani ya hifadhi hiyo.

Serengeti.Idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa
ya Serengeti(Senapa) imeongezeka katika siku za hivi karibuni kutokana na sekta ya utalii kukua huku miundombinu ya barabara na viwanja vidogo vya ndege vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo kufanya kazi vizuri.

Afisa Utalii wa Senapa,Evance Magomba alisema kuwa
baada ya kujengwa jengo dogo la wageni wanaowasili na wanaoondoka katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera idadi ya wageni imeongezeka huku wakala wa makampuni ya ndege wakiweka wawakilishi wao katika uwanja huo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa katika kipindi cha
Januari hadi Septemba mwaka huu kumekua na safari za ndege 3,724 katika uwanja  wa Seronera huku uwanja wa Lobo katika kipindi hicho ni safari 349 na uwanja wa Kogatende safari 564.

Alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna viwanja vidogo vya ndege saba kikiwemo cha Seronera ambacho ni kikubwa zaidi chenye uwezo wa kupokea ndege
kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 60 ikiwemo ya shirika la Precision
Air inayofanya kazi mara nne kwa wiki.

“Miaka miwili iliyopita hatukua na jengo hili la abiria naamini pamoja na sababu nyingine limekua kishawishi  kwa wageni kuongezeka kwani linawawezesha kuwa na sehemu nzuri ya kupumzika kabla ya kuanza safari zao,”alisema Magomba

Alisema kutokana na ukubwa wa hifadhi hiyo wanavyo viwanja vingine vilivyosambaa maeneo mbalimbali ili kutoa huduma kwa urahisi na
kuwawezesha watalii kupata muda mzuri wa kutembelea vivutio zaidi.

Magomba alivitaja viwanja vingine kuwa ni  ogatenda,Lobo,Ndutu,Kirawira ,Fort Ikoma na Lamai ambavyo hutumika kwa malengo ya kurahisisha kufika eneo husika na kulingana na watalii wanapenda kuona
vivutio maalumu.

“Hifadhi ya Serengeti ina uwezo wa kupokea wageni wa aina
zote na zipo huduma za malazi zikiwemo hoteli saba,makambi ya kudumu sita na makambi ya muda zaidi 140 yaliyosambaa na kipekee tuwakaribishe wananchi kutembelea hifadhi zetu kwasababu zipo bei maalumu kwaajili yao,”alisema Magomba

Dereva wa kampuni ya kitalii ya Micato Safaris,Emmanuel Lema alisema huduma za kitaalii nchi zimekua kwa kasi baada ya serikali kupitia Bodi ya Utalii(TTB),shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa) na wadau wengine wa utalii kutangaza kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii.

Alishauri Tanapa kuongeza ukubwa wa jengo la wanaowasili
na kuondoka na huduma zingine muhimu ili kuwawezesha watumiaji wa jengo hilo kupata huduma za kiwango cha juu hasa wakati wa msimu wa utalii.

Imeandaliwa na www.rweyemamuinfo.blogspot.com

WATALII WA NJE NA NDANI WAENDELEA KUMIMINIKA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI

Watalii wakiwasili uwanja mdogo wa ndege wa Seronera wilayani Serengeti mkoa wa Mara uliopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Senapa) kwaajili ya kutembelea vivutio vya kitalii wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka.


Serengeti - Idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Senapa) imeongezeka katika siku za hivi karibuni kutokana na sekta ya utalii kukua huku miundombinu ya barabara na viwanja vidogo vya ndege vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo kufanya kazi vizuri.

Afisa Utalii wa Senapa,Evance Magomba alisema kuwa baada ya kujengwa jengo dogo la wageni wanaowasili na wanaoondoka katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera idadi ya wageni imeongezeka huku wakala wa makampuni ya ndege wakiweka wawakilishi wao katika uwanja huo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu kumekua na safari za ndege 3,724 katika uwanja wa Seronera huku uwanja wa Lobo katika kipindi hicho ni safari 349 na uwanja wa Kogatende safari 564.

Alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna viwanja vidogo vya ndege saba kikiwemo cha Seronera ambacho ni kikubwa zaidi chenye uwezo wa kupokea ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 60 ikiwemo ya shirika la Precision Air inayofanya kazi mara nne kwa wiki.

“Miaka miwili iliyopita hatukua na jengo hili la abiria naamini pamoja na sababu nyingine limekua kishawishi kwa wageni kuongezeka kwani linawawezesha kuwa na sehemu nzuri ya kupumzika kabla ya kuanza safari zao,”alisema Magomba

Alisema kutokana na ukubwa wa hifadhi hiyo wanavyo viwanja vingine vilivyosambaa maeneo mbalimbali ili kutoa huduma kwa urahisi na kuwawezesha watalii kupata muda mzuri wa kutembelea vivutio zaidi.

Magomba alivitaja viwanja vingine kuwa ni Kogatenda,Lobo,Ndutu,Kirawira ,Fort Ikoma na Lamai ambavyo hutumika kwa malengo ya kurahisisha kufika eneo husika na kulingana na watalii wanapenda kuona vivutio maalumu.

“Hifadhi ya Serengeti ina uwezo wa kupokea wageni wa aina zote na zipo huduma za malazi zikiwemo hoteli saba,makambi ya kudumu sita na makambi ya muda zaidi 140 yaliyosambaa na kipekee tuwakaribishe wananchi kutembelea hifadhi zetu kwasababu zipo bei maalumu kwaajili yao,”alisema Magomba

Dereva wa kampuni ya kitalii ya Micato Safaris,Emmanuel Lema alisema huduma za kitaalii nchi zimekua kwa kasi baada ya serikali kupitia Bodi ya Utalii(TTB),shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa) na wadau wengine wa utalii kutangaza kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii.

Alishauri Tanapa kuongeza ukubwa wa jengo la wanaowasili na kuondoka na huduma zingine muhimu ili kuwawezesha watumiaji wa jengo hilo kupata huduma za kiwango cha juu hasa wakati wa msimu wa utalii.

Watalii wakiwasili uwanja mdogo wa ndege wa Seronera wilayani Serengeti mkoa wa Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,kukamilika kwa jengo la wageni wanaowasili na wanaondoka kumerahisisha huduma za usafiri ndani ya hifadhi hiyo. 
Afisa Utalii Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti mkoa wa Mara,Susuma Kusekwa akizungumza na watalii waliotembelea hifadhi hiyo. 
Watalii wakimsikiliza Zacharia Mathayo ambaye ni mwongoza watalii wakati akitoa maelezo kuhusu uhamaji wa wanayamapori aina ya Nyumbu kutoka Kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti hadi Kusini. 
Watalii hufurahia kuona wanyama wakubwa wakiwemo Tembo na wengine wanaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Tembo ni mojawapo ya kivutio kikubwa kwa watalii wanaotemebela hifadhi hiyo. 
Wanyama wadogo aina ya Pimbi ni sehemu ya vivutio utakavyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 
Wanyama wadogo aina ya Pimbi ni sehemu ya vivutio utakavyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imefanikiwa kutangaza vivutio vyake kikamilifu sio kwa watalii wanaotoka mataifa ya Ulaya,Asia na Amerika pekee bali pia watalii wa ndani ni sehemu ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.
Makundi makubwa ya Simba kama hili utayaona ndani ya hifadhi hiyo.