Friday, November 30, 2018

TAWLA YAWAKUTANISHA WADAU KUJADILI MASUALA MBALIMBALI YA KISHERIA ZINAYOMHUSU WATOTO

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

CHAMA cha Wanasheria Wanawake(TAWLA) kimewakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili , kuchambua na kuweka mikakati ya namna ya kuwasaidia watoto  ambao wapo kwenye ukinzani wa kisheria hasa kipindi hiki ambacho mmomonyo wa maadili kwenye jamii umekuwa mkubwa na kusababisha watoto wengi kujikuta wakiingia kwenye ukinzani huo wa kisheria.

Baadhi ya wadau ambao wamekutanishwa na TAWLA ni polisi, maofisa ustawi wa jami, wanasheria wenyewe, mahakimu, masheikh na wachungaji pamoja na wadau wengine wanaojihusisha na masuala ya watoto nchini  Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania(TAWLA)Tike Mwambipile amesema wameamua kukaa pamoja na kisha kutazama nini wafanye katika kuwasaidia watoto walioko kwenye ushindani wa kisheria na kwamba wakati wa najadiliana kwenye hilo watatumia nafasi hiyo kuulizana maswali ya msingi ya kisheria likiwamo la wapi wamekosea.

Amefafanua sheria inasema kesi ya mtoto isikilizwe ndani ya siku mmoja na hiyo ni changamoto kwani ni ngumu kutumia siku moja kusikiliza kesi ambapo utahitaji pia mashahidi na mambo mengine ya kisheria na hivyo wadau hao wataangalia nini kifanyike angalau kutoa nafasi ya kutosha ya kusikiliza kesi za watoto kwenye makosa ya haki jinai.

" Tumekutana wadau mbalimbali leo hii kwa lengo la kukaa pamoja na kutazama kitu gani hasa tufanye hasa kwa kuzingatia kwenye jamii yetu kunachangamoto ya maadili ambayo inachangia watoto wengi kuingia kwenye sheria kinzani.Hivyo tutaka na majibu ambayo angalau yatatuongoza ili tuweze kumsaidia mtoto ambaye atakuwa na kosa jinai,"amesema.

Amefafanua kuna milolongo mingi kwenye sheria zinazohusu mtoto na hivyo ni wakati sahihi wa kuangalia nini kifanyike kuwaisaida watoto wenye makosa mbalimbali na wamefikishwa mbele ya sheria."TAWLA tunaamini kupitia kikao hicho wadau watajadiliana na kutoka na majibu ya wapi tunatakiwa kwenda na wapi tulikosea katika sheria zinazohusu watoto,"amesema Mwambipile.

Kwa upande wake Wakili Barnabas Kaniki amefafanua kwa kina kuhusu masuala ya kisheria hasa zinazohusu watoto na kwamba sheria inazungumzia kuanzishwa kwa mahakama za watoto wilayani lakini kinachotokea haziko nchi nzima.

Amesema japo sheria inataka ianzishwe mahakama maalumu ya watoto na sheria imeeleza namna ambavyo kesi za watoto zinavyotakiwa kuendeshwa na kwamba kuna hatua nzuri ambayo imefikia kwenye eneo hilo.

Wakili Kaniki amesema pamoja na kwamba kuna taratibu maalum za kuendesha kesi za watoto changamoto iliyopo ni kwamba bado watoto wanapelekwa kwenye mahakama za wakubwa. "Ukweli ni kwamba wakati wadau tumekutana kujadili kwa kina kuhusu haki jina kwa mtoto , wenzetu wa mahakama wamekwenda mbele zaidi kwa kuzipa mamlaka mahakama za wilaya kusikiliza kesi za watoto."

Amesisitiza sheria ya mtoto ya mwaka 2009 imeleta mapinduzi makubwa kwenye suala zima la ulinzi wa mtoto nchini Tanzania na kufafanua sheria imetaka kuanzishwa kwa mahakama hizo za watoto.

Alipoulizwa ni makosa gani ambayo watoto wengi wanashitakiwa nayo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, amejibu kuwa watoto wengi wanafikishwa mahakamani kwa makosa ya wizi ambao aidha wa kusingiziwa au wa kweli , makosa ya ubakaji na makosa mengine mbalimbali ambayo yanakuja kwa mtindo tofauti.

Amesema sheria ya Tanzania inamtambua mtu mwenye umri wa miaka chini ya 18 ni mtoto na hivyo anapofanya kosa na akafikishwa mahakamani hata akiwa na miaka 17 au 18 maana yake kwa mujibu wa sheria lazima suala lake  lishughulikiwe kwa kuangalia sheria ya mtoto inavyotaka.

Wadau wengine ambao wamekutana kujadili sheria za mtoto nchini wameimbia Michuzi Blog kuwa wanaipongeza TAWLA kutokana na kutambua na kuona umuhimu wa kuwanisha wadau hao ili kuangalia namna gani bora katika kuwasaidia watoto wenye matatizo ya kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile akizungumza na Michuzi TV pamoja na Michuzi Blog leo jijini Dar es Salaam wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na chama hicho kujadili haki za Watoto wenye matatizo ambao wanahitaji msaada wa kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile akisoma moja ya Kitabu kinachohusu masuala ya kisheria wakati wa semina ya kujadili namna ya kumsaidia mtoto ambaye ameingia kwenye ukinzani wa kisheria.Semina hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Wakili Barnabas Kaniki akizungumzia mjadala ulioandaliwa na Chama hicho, uliokuwa unajadili haki za watoto wenye matatizo ambao wanahitaji masaada wakisheria.
Baadhi ya washiriki wa mjadala huo wakiwa kwenye semina maalum iliyoandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake(TAWLA) walipokutaa leo jijini Dar es Salaam.

JAMII YAASWA KUACHA FIKIRA POTOFU JUU YA UGONJWA WA KIFAFA


Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja akiwasilisha utafiti wake juu ya Ugojwa wa Kifafa katika muhadhara wa Kiprofesa uliofanyika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Profesa Matuja alifanya utafiti wa Ugonjwa wa Kifafa kwa muda wa miaka minne katika Wilaya ya Mahenge, Morogoro. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mwenyekiti wa Muhadhara huo, Prof. Gadi Kilonzo akifungua majadiliano ya kuulizana maswali juu somo la ugonjwa wa kifafa alilolitoa Profesa William Matuja (kushoto).
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja akiwasilisha utafiti wake juu ya Ugojwa wa Kifafa katika muhadhara uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Profesa Matuja alifanya utafiti wa Ugonjwa wa Kifafa kwa miaka minne katika Wilaya ya Mahenge, Morogoro.

Wageni waalikwa wakifuatilia muhadhara huo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja (kushoto) akikabidhiwa zawadi ya cheti shukrani na Mhadhiri mwandamizi idara. Dkt. Tumaini Nagu mara baada ya kumaliza kuwasilisha utafiti wake juu ya ugonjwa wa kifafa. Katikati ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani Dkt. Patricia Munseri.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja (kulia) akikabidhiwa zawadi na Mhadhiri mwandamizi idara ya Magonjwa ya Ndani Dkt. Tumaini Nagu mara baada ya kumaliza kuwasilisha utafiti wake juu ya ugonjwa wa kifafa.
Dkt Pilly Chillo akikabidhi zawadi ya ua.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja (kulia) akikabidhiwa zawadi na Kaimu Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani Dr. Patricia Munseri mara baada ya kumaliza kuwasilisha utafiti wake juu ya ugonjwa wa kifafa.
Afisa Uhusiano wa MUHAS, Hellen Mtui akitoa shukrani kwa wageni waliofika katika muhadhara huo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja akiwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na wanafamilia.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja akiwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na wafanyakazi wa kitengo chake.


Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Imani potofu ndiyo inayopelekea kuongezeka wa Ugonjwa wa Kifafa katika maeneo mbali mbali ya nchi ya Tanzania hasa Wilaya ya Mahenge, Morogoro.
 

Hayo ameyasema Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa William Matuja wakati akiwasilisha ufatifi wake katika muhadhara uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ili kuweza kutoa mapendekezo yake njia za kuweza kusaidia jamii.

Profesa Matuja amesema Jamii inahitaji kuondokana na imani potofu maana watu wengi wamekuwa wakijua kuwa ugonjwa unasambabishwa na ushirikina.Ameongeza kuwa jamii ni bora kujitokeza kupima mara kwa mara ili kuweza kupatiwa tiba mahususi ili kuweza kuondokana na tatizo hilo.

"Nimefanya utafiti katika wilaya ya Mahenge, Morogoro ila tulichogundua mwanzo ni jamii haikuwa na ueleza zaidi kuhusiana na ugonjwa wa kifafa na hivyo kupelekea watu wengi sana kuugua ugonjwa huo, lakini wengi wao wanafikiria imani potofu hasa haya mambo ya ushirikina," ameongeza Prof Matuja.

Aidha ameongeza kuwa ni vyema serikali na wadau wote wa afya kujitokeza kuipa elimu ya kutosha jamii ili kuweza kutambua jinsi ugonjwa wa kifafa unavyopatikana na tiba yake.

Profesa Matuja amesema kwa sasa kuna aina mpya ya kifafa ambayo ni Kifafa cha Kichwa kuanguka kifuani (Nodding Syndrome) ambao ulionekana kwa mara ya kwanza 1960 katika wilaya ya Mahenge na kwa nchi nyingine Kifafa hichi kimeonekana miaka ya 1980 Liberia, Cameroon, Sudan Kusini na Uganda Magharibi miaka ya 2000.

Amesema njia kuu za kujikinga na kifafa Tanzania ni:-


1. Kujikinga na visababishi vinavyozuilika kama kumjali mama mjamzito kipindi cha ujauzito kwa kumshauri kuhudhuria kliniki pamoja na kumpatia vipimo mara kwa mara, ugunduzi na matibabu ya haraka kwa watoto wanaopata homa, matumizi ya choo, kunawa mikono na kula nyama ya nguruwe iliyoiva vizuri.

2. Kuwepo na muendelezo wa kutoa elimu vjijini ili kutonyanyapaa na kuwabagua kwa makundi kutokana na matatizo yao; mfano mashuleni kwa ngazi zote ikiwemo walimu.

3. Kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya juu ya chanzo, jinsi ya kujikinga na matibabu sahihi kwa watu wenye kifafa.

4. Kutoa elimu maalum inayohitajika kwa watoto wenye kifafa na uwezo wa kusoma.

5. Serikali ihakikishe kuwepo na utoaji wdawa za kutosha.

BURUNDI YAKWAMISHA MKUTANO 20 WA WAKUU WA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Na. Vero Ignatus, Arusha

Mkutano wa 20 wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika ya mashariki uliokuwa ufanyike leo Mkoani Arusha umeaihirishwa.

Akitaja sababu za kuahirishwa kwa mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika ya mashariki kutoka Uganda Kirunda Kivejinja amesema nchi ya Burundi imekwamisha mkutano huo kwa kitokutuma muwakilishi

Waziri wa mambo ya nje ya nchi ya Tanzania Mhe. Augustino Mahiga amesema marais wawili wa Sudan ya Kusini na Rwanda wametuma wawakilishi lakini Rais wa Burudi hakutuma muwakilishi yeyote kwenye vikao vyote

'' Kwenye mikutano kama hii kuna kuwa na maandalizi ya ngazi tatu kwanza ni maafisa wataalam,makatibu wakuu na mwisho ya mawaziri na hatimaye inakuwa mkutano wawakuu lakini Burundi haikuleta wawakilishi kabisa na hawakutoa maelezo hivyo hatujui ninini kiewapata''alisema Mahiga

Hivyo kutokana na sheria za mkataba wa Afrika ya Mashariki kikao cha mawaziri kilishindwa kuchukua maamuzi, kwani hata kikao cha maamuzi lazima kiwe na wawakilishi kutoka nchi zote sita ."Hivyo kikao cha mawaziri hakikutoa maamuzi yeyote, tulijadiliana tu hayo ni kutokana na kilichopo katika mkataba wetu"

Amesema kuwa Marais na mawaziri walipokuja walikuwa na matumaini kuwa pengine Burundi wangetuma taarifa ama wawakilishi lakini toka walipoanza mkutano asubuhi kulikuwa hakuna taarifa yeyote hivyo wakuu wa nchi walipokutana wakaona haitawezekana kuendelea na mkutano huo

"Na hata kama wangekuwa wanazungumza mazungumzo yao yasimgelikuwa na mashiko kisheria na maamuzi ya kisheria kwahiyo wakaamua huu mkutano uhairishwe ndiyo maana huo mkutano ukaahirishwa" alisema Mahiga. Hata hivyo Mahiga amesema itawalazimu kufanya mkutano mkuu wa Wakuu wa nchi zote sita na ni lazima iwe ndani ya mwaka huu, na ndani ya mwezi disemba 2018 kikatiba

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi sita ikiwemo Tanzani, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.Mkutano huo wa 20 wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliokuwa umebeba kauli mbiu isemayo kuhuisha utengamano wa kijamii, kisiasa na kiuchumi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki


Mkutano wa 20 wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika ya mashariki uliokuwa ufanyike leo Mkoani Arusha umeairishwa.

Akitaja sababu za kuahirishwa kwa mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza la  Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika ya mashariki kutoka Uganda Kirunda Kivejinja amesema nchi ya Burundi imekwamisha mkutano huo kwa kitokutuma muwakilishi

Waziri wa mambo ya nje ya nchi ya Tanzania Mhe. Augustino Mahiga amesema marais wawili wa Sudan ya Kusini na Rwanda wametuma wawakilishi lakini Rais wa Burudi hakutuma muwakilishi yeyote kwenye vikao vyote

'' Kwenye mikutano kama hii kuna kuwa na maandalizi ya ngazi tatu kwanza ni maafisa wataalam,makatibu wakuu na mwisho ya mawaziri na hatimaye inakuwa mkutano wawakuu lakini Burundi haikuleta wawakilishi kabisa na hawakutoa maelezo hivyo hatujui ninini kiewapata''alisema Mahiga

Hivyo kutokana na sheria za mkataba wa Afrika ya Mashariki kikao cha mawaziri kilishindwa kuchukua maamuzi, kwani hata kikao cha maamuzi lazima kiwe na wawakilishi kutoka nchi zote sita . "Hivyo kikao cha mawaziri hakikutoa maamuzi yeyote, tulijadiliana tu hayo ni kutokana na kilichopo katika mkataba wetu"

Amesema kuwa Marais na mawaziri walipokuja walikuwa na matumaini kuwa pengine Burundi wangetuma taarifa ama wawakilishi lakini toka walipoanza mkutano asubuhi kulikuwa hakuna taarifa yeyote hivyo wakuu wa nchi walipokutana wakaona haitawezekana kuendelea na mkutano huo

"Na hata kama wangekuwa wanazungumza mazungumzo yao yasimgelikuwa na mashiko kisheria na maamuzi ya kisheria kwahiyo wakaamua huu mkutano uhairishwe ndiyo maana huo mkutano ukaahirishwa" alisema Mahiga

Hata hivyo Mahiga amesema itawalazimu kufanya mkutano mkuu wa Wakuu wa nchi zote sita na ni lazima iwe ndani ya mwaka huu, na ndani ya mwezi disemba 2018 kikatiba.Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi sita ikiwemo Tanzani, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini

Mkutano huo wa 20 wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliokuwa umebeba kauli mbiu isemayo kuhuisha utengamano wa kijamii, kisiasa na kiuchumi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

WAZIRI MBARAWA ASIKITISHWA NA UTENDAJI KAZI WA BOHARI KUU YA MAJI ( MAJI CENTRAL STORES)

 Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii. 

 WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa amesema lengo la serikali ni kuona bohari kuu ya maji inasaidia katika kupunguza gharama za madawa.

 Ameyasema hayo baada ya kutembelea bohari kuu ya maji (Maji Central Stores) na kusisitiza uongozi uliopo hauridhishi kutokana na namna wanavyoendesha taasisi hiyo.

 Akizungumza na waandishi wa habari, Prof Mbarawa amesema nia ya serikali ni kuona mamlaka zinafaidika na bohari kuu na muda mwingine wanatakiwa kusambaza vifaa vyake kwa mamlaka za maji kote nchini.

 Mbarawa amesema, kuna mita zaidi ya 10,000 zimefungiwa tu ndani hawazisambazi kwa mamlaka za maji, kuna miradi mingi imesimama kutokana na kukosa vifaa ila bohari kuu imeviweka na havifanyi kazi yoyote.

 Amewaagiza bohari kuu ndani ya wiki mbili wawe wamesambaza mita hizo kwa mamlaka za maji nchini ikiwemo Mkoa wa Lindi ambao wana uhitaji wa mita za maji karibia 3,000 na mikoa mingine pia.

 "Mimi hii ni mara yangu ya kwanza kufika hapa na nilikuja ili niweze kufahamu na kujifunza namna bohari kuu inavyofanya kazi ila nimefika hapa nimekuta vifaa vingi sana ambavyo vinahitajika kwenye miradi inayoendelea na mingine imesimama na hili suala linaonesha utendaji wa watu hawa hauko makini na hauridhishi,"amesema Mbarawa.

 "Lengo ni kuona bohari kuu ni kujipanga katika upande wa madawa na bohari wanatakiwa kuuza madawa kwa mamlaka na wao wakinunua kutoka kiwandani kabisa na sio kwa watu au makampuni," amesema.

 Naye Boharia Mkuu Crepin Bilamu amesema, ni kweli kuna vifaa vipo hapo ila sio kama havina ubora ila atafanya maagizo kama aliyooelekezwa na Waziri husika ya kuanza kusambaza vifaa hivyo kwa mamlaka za maji nchini.

 Bilamu ameagizwa kuteketeza dawa zote zilizoisha muda wake zisije kwenda kwa mamlaka kwa ajili ya matumizi ambao yanaweza kuleta athari kwa binadamu.
 Boharia Mkuu Crepin Bilamu akisoma taarifa kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa wakati alipotembelea bohari ya maji (Maji Central Stores) kwa ajili ya kufahamu mambo mbalimbali.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akieleza jambo kwa Boharia Mkuu Crepin Bilamu baada ya kutembelea ghala la vifaa na madawa leo Jijini Dar es Saalla
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akikagua baadhi ya vifaa vilivyopo ndani ya ghala ndani ya bohari kuu ya maji Jijini Dar es Salaam.
Vifaa mbalimbali vilivyopo ndani ya Bohari kuu ya maji ambapo vina  muda mrefu bila kutumika.

WAHITIMU CHUO CHA USTAWI WA JAMII WASHAURIWA KUTUMIA UJUZI ,UWEZO WALIOUPATA KUSAIDIA JAMII

Na Khadija Seif, Globu ya jami
            
TAASISI  ya Ustawi wa Jamii imewatunuku vyeti wahitimu 1,387 katika mahafali ya 42 ya chuo hicho katika ngazi ya astashahada,stashahada, katika fani ya Kazi za jamii kwa Watoto na vijana,Mahusiano kazini na Menejimenti ya sekta ya Umma( Industrial Relations and Public Management).

Akizungumzana leo jijini Dar es Salaam katika mahafali hayo, Katibu Mkuu - Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii -Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dk.John Jingu amesema wahitimu wote wamekula kiapo kwa ajili ya kulitumikia Taifa na ujuzi waliopatiwa ni rasilimali kwa ajili ya Taifa kwa ujumla.

Dk.Jingu ameeleza fani ya ustawi wa jamii ni nyeti na muhimu katika jamii na wanapaswa kuwa katika sekta mbalimbali kwani wamefundishwa kujiajiri na kuajiri watu kwenye kazi. Aidha katika nchi zilizoendelea kuna hitajika kuwa na Ofisa Ustawi na chuo kwa sasa kinatakiwa kuweka wigo mpana kwa ajili ya kuendelea kuzalisha wataalam kwa lengo la kusaidia jamii na manufaa ya nchi kwa ujumla.

Akizungumza na wanahabari Kaimu Mkuu wa  Taasisi, Mipango,fedha na utawala wa tasisi ya ustawi wa jamii Dk.Saliel Kanza ameeleza kuwa taasisi hiyo  ina changamoto kadhaa katika kutekeleza majukumu yake makuu matatu ambayo ni mafunzo,utafiti na kutoa ushauri wa weledi na changamoto hizo ni upungufu wa vifaa vya  Tehama katika kufundishia na kujifunza, uchakavu na upungufu wa Miundombinu ya kujifunza na kufundishia ikiwemo ofisi za walimu,vyumba vya semina,vyumba vya mihadhara(lecture theatre) na zahanati.

Dk.Kanza pia amesema pamoja na ufinyu wa mapato,Taasisi imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha mazingira bora ya kusomea kwa kubadilisha matumizi kwa baadhi ya Majengo na kuwa vyumba vya mihadhara.Pia ununuzi wa samani za ofisini na kompyuta ili kusaidia wanafunzi na wahadhiri kujifunza na kufundishia,Kufanya ukarabati wa miundombinu ya taasisi kama vile vyumba vya mihadhara kulingana na uwezo wa kifedha uliopo.

Hata hivyo,mbali na kufanya hayo bado Taasisi Haina uwezo wa kutosha kifedha ili kutatua changamoto tajwa.Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana Sophia Simba amewapongeza wahitimu hao na kuwataka watumie elimu yao na ujuzi ili kusaidia jamii katika usuluhishi wa Migogoro mbalimbali katika jamii zetu.

Simba amewahusia wahitimu katika fani zote kuwa ni kila nyanja katika jamii inauhitaji wa Ofisa ustawi kwani ni watu wenye ufanisi mkubwa sana katika kutatua,kusuluhisha,kusaidia maeneo yote kwa walemavu,makazini hata Mashuleni.
 Wahitimu wa chuo cha Ustawi wa jamii waliotunukiwa tuzo ya uzamili na Dkt John Jingu wakati wa mahafali hayo leo Jijini Dar es Salaam

BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA DK.YOUQING


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BALOZI wa China nchini Dk. Lu Youqing na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Geoffrey Mwambe wamekutana na kufanya kikao cha kazi ambapo wametumia kikao hicho pia kuzungumzia masuala yanayohusu uwekezaji hasa kwa kampuni za kutoka nchini China.

Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za TIC jijini Dar es Salaam ambapo Mwambe ametoa ufafanuzi pia kuhusu sheria ya kutoa vivutio vya uwekezaji hasa vinavyohusu msamaha wa kodi kwa wawekezaji huku akiendelea kutoa ufafanuzi zaidi kuwa kampuni za Kichina ziache kutumia taarifa za madalali na badala yake wafike TIC kupata taarifa mbalimbali za nchi kuhusu uwekezaji.

"Kituo hakipo hapa kukwamisha mwekezaji, tupo kwa ajili ya kusaidia kuanzisha uwekezaji wake nchini kwa kuwa tunatambua umuhimu wa uwekezaji huo kwa nchi,"amesema Mwambe.Baada ya maelezo hayo Balozi ameridhishwa na amepongeza Serikali kwa kusimamia uwekezaji kwa uwazi na kufuata sheria na China inafurahia jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha mazinga ya biashara na uwekezaji nchini."Mazingira ya biashara na uwekezaji yanaboreshwa na ndiyo sababu kubwa ya makampuni mengi ya China kuendelea kuonesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania,"amesema Balozi

Pia Balozi amemtaarifu Mwambe kuwa Desemba 1 mwaka 2018 msafara wa wafanyabiashara wapatao 50 unaojumuisha kampuni 26 kutoka China utafika nchini ikiwa ni mojawapo ya mpango wao wa kutembelea nchi tatu za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda. "Lengo la ziara ya wafanyabiashara hao Afrika Mashariki ni kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali. Hata hivyo kwa kutambua uwepo wa mahusianao mazuri tena ya muda mrefu yaliyopo kati ya Tanzania na China msafara ulikubaliana uanzie Tanzania kabla ya kwenda nchi nyingine. Msafara unaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Kukuza Uhusiano kati ya Nchi zinazoendelea Bw. Lyu Xinhua.


Kampuni zinazokuja nchini zipo katika sekta za viwanda, ujenzi, afya, maji, tehama, fedha, elimu, miundo mbinu, kilimo na biashara ya maduka makubwa,"amesema.Katika kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanznaia (TPSF), Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI),Ubalozi wa China nchini na Ubalozi wa Tanznaia nchini China wanaratibu Kongamano la Biashara na Uwekezaji Kati ya Tanzania na China litakalofanyika Desemba 3,2018 katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.

Balozi amewaomba Watanzania kutumia kongamno hilo kama chombo muhimu cha kutolea taarifa za kuhamasisha na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka China kwa kuzingatia kwamba wafanyabiashara wanaokuja ni wale wenye nia ya kuwekeza Afrika; na watatembelea pia nchi nyingine kwa madhumuni ya kujionea mazingira na fursa za uwekezaji. Hivyo matarajio ya Balozi ni kwamba Tanzania kama nchi itatumia fursa hiyo kueleza kinagaubaga fursa za uwekezaji na sababu za kuwekeza Tanzania na sio nchi nyingine.

Wakati huo huo Mwambe, amemshukuru Balozi kwa kukitembelea Kituo kwa lengo la kufanya mazungumzo yaliyoweka bayana utayari wa Ubalozi wa China kuisaidia TIC katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kuboresha huduma kwa wawekezaji. Pia imeelezwa kwa wafanyabiashara wenye nia ya kushiriki kongamano kati ya Tanzania na China wanaweza kuwasiliana na Bi. Diana

Ladislaus 0719 653 079 kwa maswali au Bi. Lilian Ndossi 0784323068

kwa usajili.
Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanya mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam

Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing akifafanua jambo wakati wa kikao chake na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe kilichofanyika kwenye ofisi za Kituo hicho jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe (kushoto) akifafanua jambo kwa Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing (kulia) walipokutana jijini Dar es Salaam

Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Geoffrey Mwambe (wa pili kushoto)

Madaktari Ocean Road timizeni wajibu wenu Dkt.Mpoki

Na.WAMJW, Dar es Salaam 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya amewataka Madaktari wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kutimiza wajibu wao katika kuwahudumia wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kila siku na kumuagiza  Mkurugenzi wa Huduma za Uhakiki na Ubora kutoka Wizarani kwake kufuatilia. 

Dkt.Mpoki ametoa agizo hilo alipotembelea taasisi hiyo ili kujionea hali ya utoaji huduma pamoja na kusikiliza wagonjwa wanaofika kupata huduma kwenye taasisi hiyo kutokana na kulalamikiwa kwa baadhi madaktari na wauguzi “Taasisi hii ni ya faraja lazima mtengeneza mazingira mazuri yakuwahudumia wagonjwa,kwani ndugu wanafuatilia hali za wagonjwa wao hivyo jamii inapolalamika tusiseme moja kwa moja ni waongo bali tushughulikie malalamiko yao ,kama huna jibu muelekeze kwa mtu ambaye anaweza kumpa jibu ili aweze kupata faraja”.Alisisitiza Dkt.Mpoki. 

Aidha, aliwataka watumishi wa taasisi hiyo kuvaa vitambulisho ambavyo vinaweka wazi utambulisho wao ili ndugu na wagonjwa waweze kuwatambua na kutaja ni nani ambaye hajatimiza wajibu wake ipasavyo.
“watakaoshindwa kwenda nasi tutawapeleka kwingine,hatutaki maumivu yawe sehemu ya uzoefu wa wagonjwa wanaolazwa Ocean Road,nyinyi kazi yenu ni kuwahudumia wagonjwa”. 

Hata hivyo aliwataka madaktari wabobezi (Mabingwa) kutimiza wajibu wao na sio kuwaachia jukumu la kuwahudumia wagonjwa madaktari waliopo mafunzo kwa vitendo”kuanzia sasa tukigundua mgonjwa ameachiwa daktari wa mafunzo kwa vitendo tutawaondoa wasifanye mazoezi hapa lazima tuishi kwa kutii na kufuata miiko ya taaluma zetu”alisema dkt.Mpoki 

Aliagiza kufanyika mikutano ya ndani mara kwa mara ya kufuatilia utendaji kazi wa taasisi na kujibu malalamiko yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na masanduku ya maoni ili kupata mrejesho kutoka kwa wananchi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwenye taasisi. 


Kuhusu adha ya umbali wa kufuata huduma kwenye taasisi hiyo Dkt. Mpoki aliwathibitishia wagonjwa na ndugu waliopo hospitalini hapo kuwa Serikali kupitia wizara ya afya iko mbioni kupeleka huduma za saratani kanda ya kusini mara tu itakapokamilika hospitali ya Rufaa ya kanda,pia huduma kama hizo zipo mbioni kupelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya Tabora pamoja na hospitali maalum ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma kwani ni wajibu wao kuhakikisha huduma hizo karibu na wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akiongea na wagonjwa kwenye dirisha la dawa lililopo hospitalini hapo ambapo wagonjwa walisema wanapata dawa hizo bila malipo

Dkt.Mpoki akimjulia hali mmoja wa wagonjwa kwenye wodi ya wanaume hospitalini hapo na kuahidi wizara yake ipo mbioni kusogeza huduma za saratani kwenye baadhi za hospitali za rufaa za kanda na mkoa ili kuondoa adha ya kusafiri kwenda ocean road. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akisisitiza wananchi (hawapo pichani) kuandika maoni na kuweka kwenye Kisanduku kuhusiana na huduma zinatolewa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili uongozi uweze kusoma na kuyafanyia kazi maoni hayo. 
Katibu Mkuu akisikiliza wagonjwa waliofika kupata huduma kwenye hospitali hiyo.Dkt. Mpoki aliutaka Uongozi wa hospitali hiyo kufanyia kazi malalamiko ya ndugu wa wagonjwa kama mrejesho wa utoaji huduma 

RAIS WA ZANZIBAR AZUNGUMZA NA UJUMBE WA WASHIRIKA WA MAENDELEO SEKTA YA KILIMO TANZANIA

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Meneja Mkaazi wa Growing Africa’s Agriculture (AGRA) wakati wa mazungumzo na Ujumbe wa Washirika wa Sekta ya Kilimo Tanzania, ukiongozwa na Mwakilishi wa FAO Tanzania na Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo Sekta ya Kilimo Tanzania  Mr. Fred  Kafeero, ulipofika Ikulu leo 30/11/2018 kwa mazungumzo.
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza Mwakilishi  wa FAO Nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo Sekta ya Kilimo Tanzania Mr. Fred Kafeero, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kungozana na Ujumbe wake.
  Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Ujumbe wa Washiriki wa Maendeleo Sekta ya Kilimo Tanzania kushoto Mwakilishi wa FAO Nchini Tanzania pia ni Mwenyekiti wa Washiriki wa Maendeleo Sekta ya Kilimo Tanzania Mr, Fred Kafeero akiwa na Mwakilishi wa UNIDO Tanzania,Mauritius na EAC.Mr. Stephen Bainous Kargbo, 30/11/2018.
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mwakilishi wa FAO Nchini Tanzania Mr.Fed Kafeero, alipofika Ikulu Zanzibar na Ujumbe wake wa Washirika wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Tanzania, kwa mazungumzo leo 30/11/2018. 
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiongozana na mgeni wake Mwakilishi wa FAO Nchini Tanzania pia ni Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo Sekta ya Kilimo Tanzania Mr. Fed Kafeero, wakitoka katika ukumbi wa mkutano  baada ya kumaliza mazungumzo yao  yaliofanyika Ikulu Zanzibar leo 30/11/2018.
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na Mwakilishi wa FAO Nchini Tanzania Mr. Fred Kafeero kushoto na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujumbe wa Washirika wa Maendeleo Sekta ya Kilimo Tanzania, baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Zanzibar.30/11/2018.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiagana na mgeni wake Mwakilishi wa FAO Nchini Tanzania Mr. Fred Kafeero, alipofika Ikulu Zanzibar na Ujumbe wake wa Washirika wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Tanzania, kwa mazungumzo na Rais wa Zanzibar. (Picha na Ikulu) 

KUSIMAMISHWA SOKO LA JUMLA LA FEDHA ZA KIGENI (IFEM) HAKUHUSU HUDUMA ZINGINE-BoT

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) imesema soko la jumla la fedha za kigeni kati ya benki za biashara (IFEM) ni muhimu katika soko la fedha za kigeni huku ikifafanua hilo ni soko linaloziwezesha benki za biashara na taasisi za fedha kuuza na kununua (kubadilishana) dola za Kimarekani na Shilingi kati yao. 

Taarifa ya BoT iliyotolewa Novemba 30,2018 na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki imesema kuwa soko hilo husaidia kuamua kiwango 
rasmi cha kubadilisha dola dhidi ya shilingi kwa siku husika. Benki Kuu ya Tanzania pia hushiriki kuuza na kununua fedha za kigeni pale ambapo inalazimu. 

Imesema wakati mwingine huingilia soko ili kuhakikisha hakuna mabadiliko makubwa sana ya kiwango cha kubadilisha fedha.Soko la fedha za kigeni kati ya mabenki (IFEM) lina kanuni na taratibu zake, ambazo zinaeleza kinagaubaga namna washiriki wote wanavyotakiwa kufanya biashara hiyo. 

Aidha, washiriki wote katika soko hilo wanatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu ya Tanzania kuhusu miamala waliyofanya kwa siku.Washiriki wa IFEM ambao wanavunja kanuni na taratibu za soko hilo hufungiwa kushiriki katika kuuza na kununua kwenye soko hilo kwa kipindi maalum. 

Taarifa hiyo imefafanua kufungiwa huko kunahusu tu ushiriki katika soko la fedha za kigeni kati ya mabenki na si vinginevyo. Kwa hiyo, kusimamishwa kwa benki tano za Barclays, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania kunahusu ushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki tu, yaani IFEM na si vinginevyo. 

"Benki hizo zinaruhusiwa kushiriki katika soko la reja reja la fedha za kigeni,  kwa mfano kuuza fedha za kigeni kwa wateja wake au kununua kutoka kwao,"imeeleza taarifa hiyo.

WASSIRA ATUMIA MAHAFALI CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE KUTOA UJUMBE KWA WASOMI

Na Said Mwishehe, Blogu ya jamii

CHUO cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam  kimefanya mahafali yake ya 13 ya chuo hicho ambapo jumla ya wahitimu 1578 wamehitimu ngazi mbalimbali za mafunzo huku 
Mwenyekiti wa Bodi chuoni hapo Steven Wassira akishauri somo la maadili na uzalendo liwe la lazima kwa wanafunzi wote.

Mahafali ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yamefanyika leo Novemba 30 mwaka 2018 ambapo pamoja na mambo mengine wahitimu ambao wamefanya vizuri kwenye masomo wamepewa zawadi na vyeti vya kuwatambua.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Shadrack Mwakaluka , wahadhiri wa chuo hicho, wahitimu, wanafunzi na wageni waalikwa Wassira ambaye ndiyo alikuwa mgeni rasmi amesema elimu ndio kila kitu kwenye maisha ya mwanadamu amapo pamoja na faida nyingine nyingi faida nyingine ya elimu ni kurahisisha utendaji kazi wa majukumu ya mhusika.

"Elimu ni mfano wa shamba ambalo unapanda mbegu bora na unavuna mazao bora.Hivyo nitumie nafasi hii kuwapongeza wote waliohitimu mafunzo yao chuoni hapa kwa ngazi mbalimbali.Hata hivyo niwakumbushe Watanzania elimu haina mwisho, hivyo ninyi mliomaliza ni vema mkaendelea na hatua nyingine za kielimu kwa maslahi yenu na Taifa kwa ujumla.

"Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha watu wake wanapata elimu iliyobora na imeamua kutoa elimu bure kwa ngazi ya elimu ya msingi na 
sekondari.Yote hiyo ni sehemu ya kuonesha namna inavyothamini na kutambua umuhimu wa elimu nchini.Taarifa za chuoni hapa idadi ya wanafunzi imeongezeka na hii ni dalili ya jamii nayo kutambua faida ya elimu na juhudi zinazofanywa na Serikali,"amesema Wassira.

Wakati huo huo Wassira ameshauri umuhimu wa somo la maadili na uzalendo ambalo linafundishwa chuoni hapo liwe la lazima kwa wanafunzi wote kulisoma kwani hiyo itasaidia kujenga Watanzania 
wenye uzalendo wa kuipenda nchi yao na hata wanapokuwa watumishi kufanya kazi kwa maadili mema.Pia ameshauri viongozi wa ngazi mbalimbali kufika kwenye chuo hicho kwa ajili ya kupata mafunzo ya maadili na uzalendo hasa kwa kutambua somo hilo linasaidia kujenga uelewa.

Ametoa rai kwa wasomi nchini wakiwamo wahitimu wa chuo hicho kuhakikisha wanatumia elimu ambayo wameipata kujenga hoja wakati wa kuchambua hoja kwa kuielewa na kwamba uchambuzi na uelewa ni muhimu kwa wasomi."Wasomi ni lazima wawe na uelewa pindi wanapotaka kujenga hoja kwenye jambo lolote."Kwa upande wake Profesa Mwakaluka amesema idadi ya wanafunzi katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inaongezeka mwaka hadi mwaka na hiyo inaonesha namna ambavyo chuo hicho kimeendelea kuaminiwa kutokana na elimu bora ambayo wanaitoa.

"Chuo chetu kimeendelea kuaminiwa na idadi ya wanafunzi na wahitimu inaongezeka mwaka hadi mwaka.Pia nitoe ushauri kwa Watanzania ambao wanataka kwenda kusoma nje ya nchi , kabla ya kuondoka waje chuoni kwetu kujifunza lugha ya Kingereza ambayo inatolewa na walimu waliyobobea na cheti ambacho atakipata kitamsaidia huko anakokwenda maana tunatambulika vema kwenye eneo hilo,"amesema Profesa Mwakaluka.

Wakati huo huo amesema pamoja na mafanikio makubwa , changamoto kubwa ambayo inawakabili chuoni hapo ni ufinyu wa bajeti ya fedha na uhaba wa watumishi.Hata hivyo amesema licha ya uhaba wa watumishi wameendelea kutekeleza majukumu yao vizuri.
 Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Shadrack Mwakaluka akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika leo chuoni hapo
 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Steven Wassira ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 13 ya Chuo hicho ageni rasmi (kulia) akiwa na Mkuu wa Chuo Profesa Shadrack Mwakaluka wakipitia kwa umakini majina ya wahitimu.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya chuo hicho pamoja na viongozi wengine wa chuo wakiwa pamoja na wahitimu waliofanya vizuri kwenye masomo(waliosimama nyuma).
 Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye picha wakati wa mahafali ya 13 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika leo chuoni hapo.

SERIKALI INAFANYA MAPITIO YA LESENI ZA UCHIMBAJI-MAJALIWA

*Zitakazobainika kutofanya kazi kwa muda mrefu itazichukua 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inafanya mapitio ya leseni zote za uchimbaji wa madini na zile ambazo zitabainika kuwa hazijafanya kazi kwa muda mrefu zitachukuliwa na kisha maeneo hayo hayo yatagawiwa kwa wachimbaji wadogo. Amesema Wizara ya madini imeimarishwa  na sasa inatengeneza fursa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mji Mdogo wa Katoro.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika Mji Mdogo wa Katoro uliopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Geita, akiwa kwenye siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Geita.

Waziri Mkuu amewaambia wananchi hao ambao wengi wao ni wachimbaji wadogo kuwa waendelee kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuhakikisha wachimbaji hao wanafanya shughuli zao bila ya kubugudhiwa.“Jipangeni kwa kufanya kazi maeneo yapo na Serikali itawapa. Nawashauri mjiunge katika vikundi vitakavyosajiriwa na kutambilika kisheria ili muende kwenye mabenki mbalimbali na kukopa fedha za kununulia mitambo ya kisasa itakayowawezesha kuchimba kwa kutumia teknolojia ya kisasa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Geita ihakikishe kila kijiji kinakuwa na kisima cha maji ili kuwapunguzia wananchi kutumia muda mwingi kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji katika maeneo yasiyojulikana. Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama inayowakabili wanachi kwenye Mji Mdogo wa Katoro, Waziri Mkuu amewataka waendelee kuwa na subira kwani Serikali imepanga kuwafikishia maji kutoka ziwa Victoria. 

Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao. Waziri Mkuu amesema mbali na kuimarisha huduma za maji  kwenye Mji Mdogo wa Katoro, pia Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya na kikuwezesha Kituo cha Afya cha Katoro kiweze kuwa na maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, chumba cha kujifungulia, wodi za wanawake na wanaume.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Serikali imeendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo na wa Mji Mdogo wa Katoro ili waendelee kufanya shughuli zao bila ya usumbufu wa aina yoyote. Amesema katika kuhakikisha wachimbaji hao wafanya shughuli za uchimbaji kwa weledi, Serikali imeamua kujenga vituo vya mfano vyenye lengo la kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu namba bora ya uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa

Amesema Mji Mdogo wa Katoro ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali imejenga kituo hicho katika eneo la Lwamgasa. Pia amesema wachimbaji wadogo kwa sasa wanaendelea na shughuli zao katika maeneo mbalimbali kwa uhuru na Amani yakiwemo ya Bingwa, Musasa, Nyamalimbe, Nyarugusu, Lwamgasa. Naibu Waziri huyo ametaja maeneo mengine nchini ambayo Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi wa vituo hivyo kuwa ni pamoja na Lindi, Chunya, Mpanda, Tanga na   Buhemba mkoani Mara.

Naye, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewahakikishia wakazi wa Mji mdogo wa Katoro na Buselesele kuwa maeneo yao yote ambayo hajaunganishiwa umeme wasiwe na wasiwasi umeme utawaka kabla ya sikukuu ya X-Mass. Amesema mkandarasi tayari ameshafika kwenye maeneo hayo na kuanza  kazi. Dkt. Kalemani amesemaSerikali maeneo hayo yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.” Awali, Mbunge wa Busanda, Lolencia Bukwimba alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya kwa kuwa kituo chilichopo hakitoshelezi mahitaji kwani watu wengi. Ameomba Serikali iwajengee hospitali na kuimarisha huduma za mama na mtoto kwa kuwa kwa mwezi wanazaliwa watoto 700.

ASILIMIA 85 YA WANAWAKE MKOANI MARA WANAJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA.

Na WAMJW - MARA.

Asilimia 85 ya Wanawake Mkoani Mara wanajifungua kwenye vituo vya Afya, hali iliyosaidia kupunguza idadi kubwa ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Hospitali ya Mkoa wa Mara kukagua hali ya utoaji Huduma.

"Mko Asilimia 85, kitaifa tupo Asilimia 51, kwahiyo niwapongeze kwa hilo, lengo letu ilikuwa ifikapo 2020 tunataka angalau Asilimia 80 ya wanawake wajawazito wajifungulie kwenye vituo vya Afya" Alisema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy ameitaka Mikoa mingine nchini kuiga jitihada zinazofanywa na mkoa wa Mara za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuhakikisha wanawake wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

"Sitaielewa mikoa mingine kwa kushindwa kuhamasisha na kuweka Mazingira mazuri kwa wanawake kwenda kujifungulia katika vituo vya kutoa huduma za Afya" alisema Waziri Ummy

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara kuhamasisha jamii hususan wanawake katika maeneo mbali mbali kuhudhuria kliniki angalau Mara 4 katika kipindi cha ujauzito.

"Wanawake ambao wanahudhuria Kliniki angalau mara 4 ni Asilimia 45 hivyo hamjafanya vizuri kwasababu kitaifa ni Asilimia 51, mjenge tabia ya kuwahamasisha wanawake kuhudhuria kliniki angalau Mara 4, kama watoa huduma za Afya wanavyotushauri" alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Francis Mwanisi Kuhakikisha ifikapo Disemba 30 mwaka huu angalau kaya zote mkoani Mara ziwe na vyoo bora, na kumtaka kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo bora kiafya na kiuchumi kwa mwanadamu.

"Kaya zilizo na vyoo bora kwa Mkoa wa Mara naona ni Asilimia 40, Kwahiyo tunahitaji kuongeza elimu na kutoa mwamko kwa jamii kuhusu kujenga vyoo bora na kuvitumia" alisema Waziri Ummy

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za Afya Mkoani Mara kupitia kuboresha Vituo vya Afya 14, na kujenga Hospitali 3 za Wilaya ambazo ni Lorya, Musoma DC na Bunda, jambo ambalo litalopunguza mzigo kwa Hospitali ya Mkoa ili iweze kujikita katika kutoa huduma za rufaa.

Sambamba na hilo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma Bora kwa wananchi kwa kupeleka jumla ya Watumishi 25 katika Hospitali ya Mkoa wa Mara huku akiwahasa Viongozi mkoani hapo kujenga Mazingira mazuri yakuwavutia Watumishi ili wafanye kazi kwa bidii na wabaki katika vituo vya kazi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Dkt. Hosea Bisanda alisema kuwa Hospitali ya Mkoa imeweza kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 23 mwaka 2015, vifo 14 mwaka 2016, vifo 10 mwaka 2017, na vifo 6 hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

Dkt. Bisanda amesema kuwa licha ya Serikali kuwaletea Watumishi 25 Hospitali ya Mkoa wa Mara inatakiwa kuwa na Watumishi 684, lakini Watumishi waliopo sasa ni 305, hivyo kupelekea kuwa na upungufu wa Watumishi 379 sawa na Asilimia 55.

"Hospitali ya Mkoa wa Mara ina uhaba wa Watumishi hasa Madaktari Bingwa, Madaktari wasaidizi, Wauguzi, wateknolojia, Maabara pamoja na wateknolojia madawa" alisema Dkt. Hosea Bisanda

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya mmoja kati ya wagonjwa waliofika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akihoji juu ya gharama za huduma za Afya zinazotolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara, pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma na miundombinu katika Hospitali hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya mmoja kati ya wagonjwa waliofika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akitoa maoni juu ya namba za mawasiliano zilizopo kwenye ubao mdogo wa matangazo katika Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Mara, pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Watumishi wa sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara(hawapo kwenye picha) pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma katika.
Watumishi wa Kada mbali mbali za Afya wakimsikiliza mgani rasmi Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na uboreshaji wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.