Friday, November 30, 2018

TAWLA YAWAKUTANISHA WADAU KUJADILI MASUALA MBALIMBALI YA KISHERIA ZINAYOMHUSU WATOTO

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

CHAMA cha Wanasheria Wanawake(TAWLA) kimewakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili , kuchambua na kuweka mikakati ya namna ya kuwasaidia watoto  ambao wapo kwenye ukinzani wa kisheria hasa kipindi hiki ambacho mmomonyo wa maadili kwenye jamii umekuwa mkubwa na kusababisha watoto wengi kujikuta wakiingia kwenye ukinzani huo wa kisheria.

Baadhi ya wadau ambao wamekutanishwa na TAWLA ni polisi, maofisa ustawi wa jami, wanasheria wenyewe, mahakimu, masheikh na wachungaji pamoja na wadau wengine wanaojihusisha na masuala ya watoto nchini  Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania(TAWLA)Tike Mwambipile amesema wameamua kukaa pamoja na kisha kutazama nini wafanye katika kuwasaidia watoto walioko kwenye ushindani wa kisheria na kwamba wakati wa najadiliana kwenye hilo watatumia nafasi hiyo kuulizana maswali ya msingi ya kisheria likiwamo la wapi wamekosea.

Amefafanua sheria inasema kesi ya mtoto isikilizwe ndani ya siku mmoja na hiyo ni changamoto kwani ni ngumu kutumia siku moja kusikiliza kesi ambapo utahitaji pia mashahidi na mambo mengine ya kisheria na hivyo wadau hao wataangalia nini kifanyike angalau kutoa nafasi ya kutosha ya kusikiliza kesi za watoto kwenye makosa ya haki jinai.

" Tumekutana wadau mbalimbali leo hii kwa lengo la kukaa pamoja na kutazama kitu gani hasa tufanye hasa kwa kuzingatia kwenye jamii yetu kunachangamoto ya maadili ambayo inachangia watoto wengi kuingia kwenye sheria kinzani.Hivyo tutaka na majibu ambayo angalau yatatuongoza ili tuweze kumsaidia mtoto ambaye atakuwa na kosa jinai,"amesema.

Amefafanua kuna milolongo mingi kwenye sheria zinazohusu mtoto na hivyo ni wakati sahihi wa kuangalia nini kifanyike kuwaisaida watoto wenye makosa mbalimbali na wamefikishwa mbele ya sheria."TAWLA tunaamini kupitia kikao hicho wadau watajadiliana na kutoka na majibu ya wapi tunatakiwa kwenda na wapi tulikosea katika sheria zinazohusu watoto,"amesema Mwambipile.

Kwa upande wake Wakili Barnabas Kaniki amefafanua kwa kina kuhusu masuala ya kisheria hasa zinazohusu watoto na kwamba sheria inazungumzia kuanzishwa kwa mahakama za watoto wilayani lakini kinachotokea haziko nchi nzima.

Amesema japo sheria inataka ianzishwe mahakama maalumu ya watoto na sheria imeeleza namna ambavyo kesi za watoto zinavyotakiwa kuendeshwa na kwamba kuna hatua nzuri ambayo imefikia kwenye eneo hilo.

Wakili Kaniki amesema pamoja na kwamba kuna taratibu maalum za kuendesha kesi za watoto changamoto iliyopo ni kwamba bado watoto wanapelekwa kwenye mahakama za wakubwa. "Ukweli ni kwamba wakati wadau tumekutana kujadili kwa kina kuhusu haki jina kwa mtoto , wenzetu wa mahakama wamekwenda mbele zaidi kwa kuzipa mamlaka mahakama za wilaya kusikiliza kesi za watoto."

Amesisitiza sheria ya mtoto ya mwaka 2009 imeleta mapinduzi makubwa kwenye suala zima la ulinzi wa mtoto nchini Tanzania na kufafanua sheria imetaka kuanzishwa kwa mahakama hizo za watoto.

Alipoulizwa ni makosa gani ambayo watoto wengi wanashitakiwa nayo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, amejibu kuwa watoto wengi wanafikishwa mahakamani kwa makosa ya wizi ambao aidha wa kusingiziwa au wa kweli , makosa ya ubakaji na makosa mengine mbalimbali ambayo yanakuja kwa mtindo tofauti.

Amesema sheria ya Tanzania inamtambua mtu mwenye umri wa miaka chini ya 18 ni mtoto na hivyo anapofanya kosa na akafikishwa mahakamani hata akiwa na miaka 17 au 18 maana yake kwa mujibu wa sheria lazima suala lake  lishughulikiwe kwa kuangalia sheria ya mtoto inavyotaka.

Wadau wengine ambao wamekutana kujadili sheria za mtoto nchini wameimbia Michuzi Blog kuwa wanaipongeza TAWLA kutokana na kutambua na kuona umuhimu wa kuwanisha wadau hao ili kuangalia namna gani bora katika kuwasaidia watoto wenye matatizo ya kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile akizungumza na Michuzi TV pamoja na Michuzi Blog leo jijini Dar es Salaam wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na chama hicho kujadili haki za Watoto wenye matatizo ambao wanahitaji msaada wa kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile akisoma moja ya Kitabu kinachohusu masuala ya kisheria wakati wa semina ya kujadili namna ya kumsaidia mtoto ambaye ameingia kwenye ukinzani wa kisheria.Semina hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Wakili Barnabas Kaniki akizungumzia mjadala ulioandaliwa na Chama hicho, uliokuwa unajadili haki za watoto wenye matatizo ambao wanahitaji masaada wakisheria.
Baadhi ya washiriki wa mjadala huo wakiwa kwenye semina maalum iliyoandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake(TAWLA) walipokutaa leo jijini Dar es Salaam.

No comments: