Wednesday, October 31, 2012

Ligi kuu ya Vodacom sasa kwenye mtandao

Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom,Rene Meza
· Wateja kupata taarifa kupitia SMS, Facebook na Twitter.
·Yatoa pongezi kwa vyombo vya habari na timu.

Mdhamini Mkuu wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imewekeza katika kuwawezesha mashabiki wa soka kupata taarifa na matukio ya mechi zote za ligi hiyo kupitia njia ya simu za kiganjani na intanet.

 Kupitia mifumo mbalimbali ya kiteknolojia wateja wa Vodacom wataweza kupata matokeo ya mechi mbalimbali kupitia simu zao za kiganjani ukiwa na ujumbe mfupi wa maneno na mitandao ya kijamii. Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, amesema, Mtandao wa Vodacom una miundombinu ya kutosha na unaongoza katika masuala ya teknolojia.
 
Hivyo itatumika katika kuwawezesha mashabiki wa soka walioko ndani na nje ya nchi kujua matukio mbalimbali ya ligi kuu ya Vodacom. “Licha ya ligi yetu kuonekana katika kituo cha Televisheni cha Super Sport.

 Tumejipanga sasa kuhakikisha inakuwa katika mitandao mbalimbali muda wote kwa kila mchezo na kila tukio katika soka, Mashabiki watapata taarifa za ligi popote watakapokuwa,” alisema Meza na Kuongeza kuwa, “Kupitia intanet matukio haya yatapatikana kupitia Facebook na Twitter na mitandao mingine ya kijamii.” 

“Ili kupata matokeo na taarifa mbalimbali kupitia njia ya simu mteja wa Vodacom atatakiwa kupiga *149*01# kisha atachagua VODACOM FLAVA na akisha kujiunga na huduma hiyo itakayo muwezesha kupata taarifa na matokeo ya mechi mbalimbali” Aliongeza kuwa, 

“ Kwa wateja wanaotumia facebook na twitter kwao ni rahisi zaidi kwani huduma hizo zinatolewa bure na Vodacom, hivyo mashabiki wa soka watatembelea Ukurasa wetu wa facebook na Twitter na kupata taarifa mbalimbali kuhusu ligi na wengine kujishindia zawadi kwa kujibu maswali mbalimbali zikiwemo tiketi za mechi za ligi,” 

Aidha Mkurugenzi huyo alitoa Pongezi kwa Vyombo vya habari kwa kazi kubwa inayofanya katika kuwahabarisha watanzania kuhusu michezo mbalimbali hususani ligi kuu ya Vodacom kupitia Televisheni, Radio, Magazeti na Mitandao ya kijamii.

 “Vyombo vya habari ni wadau wakubwa na wanafanya kazi nzuri sana katika kutoa taarifa hizi wanastahili pongezi, nasi tunaangalia namna ya kuwaunga mkono kwa namna moja ama nyingine katika jitihada za kukuza soka la Tanzania na tunaamini tutafika mbali.” 

Mkurugenzi huyo alihitimisha kwa kutoa pongezi kwa timu mbalimbali zinazoshiriki katika ligi kwa kusema kuwa zimeonesha hamasa kubwa na kubainisha kuwa ni ishara ya ukuaji wa soka katika soka la Tanzania ambalo ndio lengo kuu la Vodacom. 

“Ligi sasa imekuwa na msisimko kila timu inajitahidi kushinda kila mechi,hadi sasa timu zote zimeonesha kiwango kikubwa na soka la kuvutia tunatarajia maendeleo haya yataleta tija hata kwa timu yetu ya Taifa kufanya vizuri. 

Vipaji vingi vinaonekana na ajira kwa vijana imeongezeka kupitia michezo,” alihitimisha Meza. Kampuni ya Vodacom katika kuongeza msisimko kwa mashabiki wa ligi imetoa ofa mbalimbali msimu huu kwa kuwawezesha wateja wake kupata SMS 50, Muda wa maongezi wa dakika 30 na MB 50 kwa shilingi 400 Ili kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki. 

Pamoja na mambo mengine kampuni hiyo inaangalia namna ya kutoa adha ya ukataji tiketi kwa wateja wake kutumia huduma ya M - pesa kununua tiketi za mechi mbalimbali.

JK katika msiba wa mama Lucy jijini Arusha leo

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na waombolezaji nyumbani kwa Marehemu Lucy Adam Samilah Mtaa wa Haile Selassie jijini Arusha leo  

Jeneza lenye mwili wa Marehemu Lucy Adam Samilah likiwasili katika makaburi ya Njiro kwa mazishi

 Baba Mchungaji akiongoza maombi ya mazishi
Jeneza likiteremshwa kaburini
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima zake za mwisho 
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitia saini kitabu vha maombolezo 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa watoto wa marehemu
Waombolezaji  
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka mchanga kaburini 
 Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda akiweka mchanga kaburini
  Mkuu wa Mkoa wa Arusha akiweka mchanga kaburini
 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akiweka mchanga kaburini
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha akiweka mchanga kaburini

Tuesday, October 30, 2012

MAMA PINDA AWAAMBIA VIJANA UJASIRIAMALI NI AJIRA RASMI INAYOTAMBULIKA DUNIANI.

Mke wa Waziri Mkuu Mana Tunu Pinda akitoa hotuba ya kufungua Maonyesho ya Wanawake Wajasiriamali (MOWE) katika Viwanja vya Mnazi Mmoja leo jijini Dar es Salaam ambapo amewahimiza wajasiriamali kujiunga katika ushirika ili iwe rahisi kusaidiwa kupata mikopo, kutafuta masoko, kupanga bei nzuri ya bidhaa zetu, kupata utaalam na teknolojia mpya. Kauli Mbiu ya ya Maonyesho hayo mwaka huu ni “Msichana Amka, Ujasiriamali ni Ajira”.
Mama Tunu Pinda akikata utepe kuzindua Mradi wa Uwezeshaji Kiuchumi wa Maendeleo ya Wanawake Wajasiriamali (WEDEE) Ulio chini ya Shirika la Kazi Duniani (WEDEE) wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Wanawake wajasiriamali ya MOWE yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Mama Pinda akipokea vitabu toka kwa Noreen Toroka (wa pili kulia) na Hopolang Phororo wa ILO.
Mama Tunu Pinda akisoma kwa furaha kitini cha mafunzo ya Wajasiriamali baada ya kufungua Maonyesho ya Wanawake Wajasiriamali (MOWE) katika Viwanja vya Mnazi Mmoja leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Bi. Hopolang Phororo na Noreen Toroka kutoka ILO.
Pichani Juu na Chini ni Mama Tunu Pinda akikagua baadhi ya mabanda na kujionea bidhaa mbalimbali katika maonyesho hayo.
Mama Tunu Pinda akipokea kipeperushi kutoka kwa Noreen Toroka wa ILO walioandaa maonyesho ya MOWE kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanawake na Maendele0 (WAMA) iliyochini ya Mama Salma Kikwete.
Mama Tunu Pinda (katikati) katika picha ya pamoja baada ya kufungua maonyesho ya MOWE 2012.

MAPATO UWANJA WA NDEGE PEMBA HAYAKIDHI MAHITAJI

Na Nafisa Madai 

Wafanyakazi wa kiwanja cha ndege Pemba wamesema mapatao yanayopatika kiwanjani hapo hayakidhi mahitaji ya kiwanja hivyo serikali kupitia wizara husika wanahitaji kutupia macho na nguvu zao kiwanjani hapo. 

Wamesema hayo wakati walipotembelea na waziri wa miundombinu na mawasiliano Mhe Rashid Seif ambapo wamesema kwa vile sasa wanatakiwa kubadilika kiutendaji tokea kuundwa kuwa mamlaka kamili serikali haina budi kuelekeza nguvu zao kiwanjani hapo ili kukifanya kiwanja hicho kuwa na hadhi na haiba nzuri kwa wenyeji na wageni wanaotumia kiwanja hicho. 

Aidha wamesema mpaka saivi bado hawajaona mabadiliko yoyote tokea kundwa mamlaka Jambo ambalo limekua likirudisha nyuma ufanisi wa kazi zao.

 Hata hivyo wamesema bado kama mamlaka wanafanya kazi katika mazingira magumu sana hasa pale wanapofanya upekuzi mizigo ya abiria hulazimika kutumia mikono na wala hawafahamu mizigo ile kama ipo salama ama laa. 

Wafanyakazi hao wamemuomba waziri huyo kufanya juhudi za makusudi kutafuta mashine alau moja ya kupimia mizigo ya abiria ili waweze kugundua ndani ya mizigo kuna kitu gani. 

Aidha wamemtaka waziri huyo kuchukua hatua maalumu kwa gari zinazoingia ndani ya kiwanja kwani wamesema kuna baadhi ya gari zinazokuja kuchukua viongozi huingia ndani ya uwanja jambo ambalo limekuwa likiharibu barabara za ndege yaani( apron). 

Kwa upande wake waziri Seif amesema lengo haswa la kufanya ziara katika taasisi mbali mbali za wizara yake ni kuangalia mapungufu yaliyopo ili kuhakikisha mapungufu hayo yanapatiwa ufumbuzi yakinifu. 

Aidha Waziri seif aliwatoa wasiwasi wafanyakazi hao kuwa hakuna tofauti katika ya kiwanja cha ndege unguja na cha pemba hivyo alimtaka meneja msaidizi kuhakikiksha kuwa hudma zinazotolewa unguja lazima Pemba ziwepo. 

Sambamba na hayo aliwataka wafanya kazi hao kubadilika katika utendaji wao na wawe wabunifu ili waweze kujitangaza ndani na nje ya nchi. Hata hivyo uwanja wa ndege ni sehemu nzito ya kufanya kazi ambapo alisema kila aliepewa dhamana ahakikishe anawajibika ipasavyo kwa vile kazi ni sehemu ya maisha yao. 

 Baada ya mazungumzo hayo mhe Waziri alitembelea jingo hilo kwa kukagua sehemu ya choo ambavyo vimefanyiwa matengenezo, sehemu ya zima moto na kuangalia mnara wa zantel ambao upo karibu na eneo la kiwanja hicho.

Waziri Membe akiwa ziarani Mkoa wa Mbeya

Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akisaini kitabu cha wageni jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, wakati akiwa katika ziara ya siku mbili Mkoani humo.
Mhe. Waziri Membe akifafanua kuhusu mgogoro wa Mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya Uenyekiti wa Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani Mbeya wakimsikiliza kwa makini Mhe. Waziri Membe (hayupo pichani).
Wilayani Kyela, Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. M. Malenga akimkaribisha Mhe. Waziri Membe (wa pili kulia), wakati alipotembelea Ofisi yake jana Wilayani Kyela.  Mhe. Membe yupo Mkoani Mbeya kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili, ambapo anatarajiwa kutembelea maeneo ya ufukwe wa Ziwa Nyasa. 


Wajumbe mbalimbali waliohudhuria Mkutano wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kyela (hayupo pichani).Balozi Irene Kasyanju (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dkt. Mohamed Maundi (kushoto), Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia - Kurasini wakisikiliza maelezo ya Mhe. Malenga kuhusu Wilaya ya Kyela.
Safari ya kuelekea kwenye mpaka wa Mto Songwe

Mkuu wa Wilaya ya Kyela akiuongoza msafara wa Waziri Membe kuelekea kwenye mpaka wa Mto Songwe uliopo kati ya Tanzania na Malawi.
Mhe. Waziri Membe na msafara wake wakiwa wamesimama kwenye mpaka wa Mto Songwe.
Waziri Membe akiangalia Mto Songwe, huku akitafakari mpaka kwa vile hapo aliposimama kwa ufupi ni nchini Malawi ambapo wananchi wa pande zote wanapishana kuendelea na shughuli zao za kawaida (angalia alama ya tundu lililoko chini ya fensi - kulia).
Mhe. Waziri Membe akiongea na Wajumbe wa msafara wake akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Kandoro (mwenye shati jeupe mbele ya Waziri), Balozi Irene Kasyanju (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dkt. Mohamed Maundi (kushoto), Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia - Kurasini.  (Picha hii na Mbaraka Islam)
Makazi ya wananchi wa Malawi kando ya Mto Songwe ambapo mmoja wa wananchi anaonekana akifua nguo (pichani - upande wa kushoto; ng'ando ya mpaka kwa upande wa Malawi) wakati wengine (kulia) wanaonekana wakiendelea na shughuli zao za kawaida huku wakiwa tayari wamevuka ng'ando ya mpaka kwa upande wa Tanzania.  Picha, maelezo na Tagie Daisy Mwakawago

Monday, October 29, 2012

Usafiri wa Treni Dar es Salaam Wanza Rasmi Leo

USAFIRI wa kutumia treni jijini Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Stesheni ya Treni) umeanza leo. Treni ya kwanza imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea katikati ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetumia wastani wa dakika 30 kufika katikati ya jiji. 

Treni ilioanza kazi leo iliyokuwa na injini mbili (vichwa vya traini) moja ikiwa imefungwa nyuma na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita, yaani matano ya abiria wa kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni maalumu kwa ajili ya kubeba wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu huku wanafunzi wakitakiwa kulipa sh. 100 kwa kila mmoja. 

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri wa leo ambao ni wamajaribio, akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli. 

Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni ya TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo la TAZARA kuelekea Mwakanga. Akizungumza mara baada ya ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni hiyo inaendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya usafiri hasa kwa foleni, ambapo utumia muda mrefu njiani kuingia na kutoka jijini. 

Alisema jumla ya mabehewa ya treni 14 pamoja na injini mbili zimekarabatiwa na mafundi wazalendo nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya kazi ya kusafirisha abiria kuingia na kutoka jijini kila asubuhi na jioni. Alisema kwa sasa inafanya treni moja kwa majaribio lakini baada ya uzinduzi mkubwa zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa zikipishana njiani moja ikirudi na nyingine ikienda. 

Akifafanua zaidi alisema kitendo cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa mabehewa na injini kimeokoa kiasi kikubwa cha fedha za umma kwani ukarabati wote umetumia sh. bilioni 2.1 tu, ilhali kama Serikali ingelazimika kukodi injini gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani bei ya kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku. 

Hata hivyoDk. Mwakyembe amewataka Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa upungufu utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado wanaendelea kufanya marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa. 

Mwandishi wa habari hizi alikuwa ni mmoja wa wasafiri walioizindua treni hiyo leo. Awali akizungumza mmoja wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni hiyo itafanya kazi kila siku isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu na itaanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa 9:00 za jioni, itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa nne usiku. 

Uchunguzi uliofanywa na muandishi wa habari hizi umebaini kuwa behewa moja la treni linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa, lina milango minne, feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia kwa abiria ambao watakuwa wamesimama. Aidha mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya kutosha. 

Treni ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama vituo vya eneo la Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani, Tazara, Kariakoo Gerezani (Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni kilichopo jirani na Kituo cha Polisi Kati (Katikati ya Jiji).
Abiria wa Usafiri wa Treni uliozinduliwa rasmi leo kwa ajili ya safari za ndani ya Jiji la Dar wakipanda usafiri huo.
Abiria Wakisubiri Treni Kituoni.
Treni ikiwa safarini.
Abiria wakiwa ndani ya Usafiri wa Treni huku wengine wakiendelea kupata nyuzz mbali mbali tena kwa utulivu kabisa kupitia magazeti.
Tangazo la Usafiri huo wa Treni.
Abiria ndani ya Treni
Abiria wakiwa wamejitokeza kwa wingi kupanda Treni zinazofanya usafiri wake ndani ya jiji la Dar mara baada ya kuzinduliwa rasmi leo na Waziri wa Uchukuzi,Dk. Harrison Mwakyembe.
Treni ikichanja mbuga.
Abiria wakiwa ndani ya Treni hiyo huku wakiwa ni wenye furaha na usafiri huo.
Wakaguzi wa tiketi za Treni wakiwajibika mchana wa leo wakati wa Uzinduzi wa Safari za Treni ndani ya jiji la Dar es Salaam mara baada ya kuzinduliwa rasmi leo na Waziri wa Uchukuzi,Dk. Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Uchukuzi,Dk. Harrison Mwakyembe akiongozana na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli wakati wa uzinduzi wa Safari za Treni ndani ya Jiji la Dar es Salaam mapema leo.
Waziri wa Uchukuzi,Dk. Harrison Mwakyembe akiwa nadni ya treni hiyo sambamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli wakati wa uzinduzi wa Safari za Treni ndani ya Jiji la Dar es Salaam mapema leo.