Friday, November 30, 2018

KUSIMAMISHWA SOKO LA JUMLA LA FEDHA ZA KIGENI (IFEM) HAKUHUSU HUDUMA ZINGINE-BoT

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) imesema soko la jumla la fedha za kigeni kati ya benki za biashara (IFEM) ni muhimu katika soko la fedha za kigeni huku ikifafanua hilo ni soko linaloziwezesha benki za biashara na taasisi za fedha kuuza na kununua (kubadilishana) dola za Kimarekani na Shilingi kati yao. 

Taarifa ya BoT iliyotolewa Novemba 30,2018 na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki imesema kuwa soko hilo husaidia kuamua kiwango 
rasmi cha kubadilisha dola dhidi ya shilingi kwa siku husika. Benki Kuu ya Tanzania pia hushiriki kuuza na kununua fedha za kigeni pale ambapo inalazimu. 

Imesema wakati mwingine huingilia soko ili kuhakikisha hakuna mabadiliko makubwa sana ya kiwango cha kubadilisha fedha.Soko la fedha za kigeni kati ya mabenki (IFEM) lina kanuni na taratibu zake, ambazo zinaeleza kinagaubaga namna washiriki wote wanavyotakiwa kufanya biashara hiyo. 

Aidha, washiriki wote katika soko hilo wanatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu ya Tanzania kuhusu miamala waliyofanya kwa siku.Washiriki wa IFEM ambao wanavunja kanuni na taratibu za soko hilo hufungiwa kushiriki katika kuuza na kununua kwenye soko hilo kwa kipindi maalum. 

Taarifa hiyo imefafanua kufungiwa huko kunahusu tu ushiriki katika soko la fedha za kigeni kati ya mabenki na si vinginevyo. Kwa hiyo, kusimamishwa kwa benki tano za Barclays, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania kunahusu ushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki tu, yaani IFEM na si vinginevyo. 

"Benki hizo zinaruhusiwa kushiriki katika soko la reja reja la fedha za kigeni,  kwa mfano kuuza fedha za kigeni kwa wateja wake au kununua kutoka kwao,"imeeleza taarifa hiyo.

No comments: