Friday, November 30, 2018

WASSIRA ATUMIA MAHAFALI CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE KUTOA UJUMBE KWA WASOMI

Na Said Mwishehe, Blogu ya jamii

CHUO cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam  kimefanya mahafali yake ya 13 ya chuo hicho ambapo jumla ya wahitimu 1578 wamehitimu ngazi mbalimbali za mafunzo huku 
Mwenyekiti wa Bodi chuoni hapo Steven Wassira akishauri somo la maadili na uzalendo liwe la lazima kwa wanafunzi wote.

Mahafali ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yamefanyika leo Novemba 30 mwaka 2018 ambapo pamoja na mambo mengine wahitimu ambao wamefanya vizuri kwenye masomo wamepewa zawadi na vyeti vya kuwatambua.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Shadrack Mwakaluka , wahadhiri wa chuo hicho, wahitimu, wanafunzi na wageni waalikwa Wassira ambaye ndiyo alikuwa mgeni rasmi amesema elimu ndio kila kitu kwenye maisha ya mwanadamu amapo pamoja na faida nyingine nyingi faida nyingine ya elimu ni kurahisisha utendaji kazi wa majukumu ya mhusika.

"Elimu ni mfano wa shamba ambalo unapanda mbegu bora na unavuna mazao bora.Hivyo nitumie nafasi hii kuwapongeza wote waliohitimu mafunzo yao chuoni hapa kwa ngazi mbalimbali.Hata hivyo niwakumbushe Watanzania elimu haina mwisho, hivyo ninyi mliomaliza ni vema mkaendelea na hatua nyingine za kielimu kwa maslahi yenu na Taifa kwa ujumla.

"Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha watu wake wanapata elimu iliyobora na imeamua kutoa elimu bure kwa ngazi ya elimu ya msingi na 
sekondari.Yote hiyo ni sehemu ya kuonesha namna inavyothamini na kutambua umuhimu wa elimu nchini.Taarifa za chuoni hapa idadi ya wanafunzi imeongezeka na hii ni dalili ya jamii nayo kutambua faida ya elimu na juhudi zinazofanywa na Serikali,"amesema Wassira.

Wakati huo huo Wassira ameshauri umuhimu wa somo la maadili na uzalendo ambalo linafundishwa chuoni hapo liwe la lazima kwa wanafunzi wote kulisoma kwani hiyo itasaidia kujenga Watanzania 
wenye uzalendo wa kuipenda nchi yao na hata wanapokuwa watumishi kufanya kazi kwa maadili mema.Pia ameshauri viongozi wa ngazi mbalimbali kufika kwenye chuo hicho kwa ajili ya kupata mafunzo ya maadili na uzalendo hasa kwa kutambua somo hilo linasaidia kujenga uelewa.

Ametoa rai kwa wasomi nchini wakiwamo wahitimu wa chuo hicho kuhakikisha wanatumia elimu ambayo wameipata kujenga hoja wakati wa kuchambua hoja kwa kuielewa na kwamba uchambuzi na uelewa ni muhimu kwa wasomi."Wasomi ni lazima wawe na uelewa pindi wanapotaka kujenga hoja kwenye jambo lolote."Kwa upande wake Profesa Mwakaluka amesema idadi ya wanafunzi katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inaongezeka mwaka hadi mwaka na hiyo inaonesha namna ambavyo chuo hicho kimeendelea kuaminiwa kutokana na elimu bora ambayo wanaitoa.

"Chuo chetu kimeendelea kuaminiwa na idadi ya wanafunzi na wahitimu inaongezeka mwaka hadi mwaka.Pia nitoe ushauri kwa Watanzania ambao wanataka kwenda kusoma nje ya nchi , kabla ya kuondoka waje chuoni kwetu kujifunza lugha ya Kingereza ambayo inatolewa na walimu waliyobobea na cheti ambacho atakipata kitamsaidia huko anakokwenda maana tunatambulika vema kwenye eneo hilo,"amesema Profesa Mwakaluka.

Wakati huo huo amesema pamoja na mafanikio makubwa , changamoto kubwa ambayo inawakabili chuoni hapo ni ufinyu wa bajeti ya fedha na uhaba wa watumishi.Hata hivyo amesema licha ya uhaba wa watumishi wameendelea kutekeleza majukumu yao vizuri.
 Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Shadrack Mwakaluka akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika leo chuoni hapo
 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Steven Wassira ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 13 ya Chuo hicho ageni rasmi (kulia) akiwa na Mkuu wa Chuo Profesa Shadrack Mwakaluka wakipitia kwa umakini majina ya wahitimu.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya chuo hicho pamoja na viongozi wengine wa chuo wakiwa pamoja na wahitimu waliofanya vizuri kwenye masomo(waliosimama nyuma).
 Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye picha wakati wa mahafali ya 13 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika leo chuoni hapo.

No comments: