Na.WAMJW, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya amewataka Madaktari wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kutimiza wajibu wao katika kuwahudumia wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kila siku na kumuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Uhakiki na Ubora kutoka Wizarani kwake kufuatilia.
Dkt.Mpoki ametoa agizo hilo alipotembelea taasisi hiyo ili kujionea hali ya utoaji huduma pamoja na kusikiliza wagonjwa wanaofika kupata huduma kwenye taasisi hiyo kutokana na kulalamikiwa kwa baadhi madaktari na wauguzi “Taasisi hii ni ya faraja lazima mtengeneza mazingira mazuri yakuwahudumia wagonjwa,kwani ndugu wanafuatilia hali za wagonjwa wao hivyo jamii inapolalamika tusiseme moja kwa moja ni waongo bali tushughulikie malalamiko yao ,kama huna jibu muelekeze kwa mtu ambaye anaweza kumpa jibu ili aweze kupata faraja”.Alisisitiza Dkt.Mpoki.
Aidha, aliwataka watumishi wa taasisi hiyo kuvaa vitambulisho ambavyo vinaweka wazi utambulisho wao ili ndugu na wagonjwa waweze kuwatambua na kutaja ni nani ambaye hajatimiza wajibu wake ipasavyo.
“watakaoshindwa kwenda nasi tutawapeleka kwingine,hatutaki maumivu yawe sehemu ya uzoefu wa wagonjwa wanaolazwa Ocean Road,nyinyi kazi yenu ni kuwahudumia wagonjwa”.
Hata hivyo aliwataka madaktari wabobezi (Mabingwa) kutimiza wajibu wao na sio kuwaachia jukumu la kuwahudumia wagonjwa madaktari waliopo mafunzo kwa vitendo”kuanzia sasa tukigundua mgonjwa ameachiwa daktari wa mafunzo kwa vitendo tutawaondoa wasifanye mazoezi hapa lazima tuishi kwa kutii na kufuata miiko ya taaluma zetu”alisema dkt.Mpoki
Aliagiza kufanyika mikutano ya ndani mara kwa mara ya kufuatilia utendaji kazi wa taasisi na kujibu malalamiko yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na masanduku ya maoni ili kupata mrejesho kutoka kwa wananchi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwenye taasisi.
Kuhusu adha ya umbali wa kufuata huduma kwenye taasisi hiyo Dkt. Mpoki aliwathibitishia wagonjwa na ndugu waliopo hospitalini hapo kuwa Serikali kupitia wizara ya afya iko mbioni kupeleka huduma za saratani kanda ya kusini mara tu itakapokamilika hospitali ya Rufaa ya kanda,pia huduma kama hizo zipo mbioni kupelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya Tabora pamoja na hospitali maalum ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma kwani ni wajibu wao kuhakikisha huduma hizo karibu na wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akiongea na wagonjwa kwenye dirisha la dawa lililopo hospitalini hapo ambapo wagonjwa walisema wanapata dawa hizo bila malipo
Dkt.Mpoki akimjulia hali mmoja wa wagonjwa kwenye wodi ya wanaume hospitalini hapo na kuahidi wizara yake ipo mbioni kusogeza huduma za saratani kwenye baadhi za hospitali za rufaa za kanda na mkoa ili kuondoa adha ya kusafiri kwenda ocean road.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akisisitiza wananchi (hawapo pichani) kuandika maoni na kuweka kwenye Kisanduku kuhusiana na huduma zinatolewa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili uongozi uweze kusoma na kuyafanyia kazi maoni hayo.
Katibu Mkuu akisikiliza wagonjwa waliofika kupata huduma kwenye hospitali hiyo.Dkt. Mpoki aliutaka Uongozi wa hospitali hiyo kufanyia kazi malalamiko ya ndugu wa wagonjwa kama mrejesho wa utoaji huduma
No comments:
Post a Comment