Saturday, September 29, 2018

WADAU WATAKIWA KUENDELEA KUFANYA TATHMINI YA ELIMU NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR –TAMISEMI), Selemani Jafo akifunga Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akitoa neno la Utangulizi wakati wa ufungaji wa Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.
Baadhi ya wadau wa elimu walioshiriki katika Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.

Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi walioshiriki kama Wadau wa Elimu katika Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Lydia Wilberd akitoa salamu za asasi hiyo kabla ya kufungwa kwa Mkutano wa pamoja wa Wadau wa Elimu nchini uliofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma. Mkutano huo ulijadili kuhusu mafanikio na changamoto za sekta ya elimu.



Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Wadau wa Elimu wametakiwa kuendelea kufanya tathmini ya elimu kwa kujadili mafanikio na changamoto za sekta hiyo ili kuboresha na kukuza elimu nchini.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Elimu.

Waziri Jafo amesema kuwa nchi nyingi ambazo hazina rasilimali za madini wala vivutio vya utalii zinaendelea kuwekeza katika rasilimali elimu ambapo baadae nchi hizo huwa tajiri na kutoa misaada kwa nchi masikini.

“Taifa linalowekeza vizuri katika sekta ya elimu ndilo Taifa lenye nafasi kubwa ya kukomboa wananchi wake na taifa kiujumla hivyo kutathmini juu ya elimu inayotolewa nchini kwetu ni jambo la muhimu sana”, alisema Jafo.

Waziri Jafo amewasisitiza wadau wa elimu walioshiriki katika mafunzo hayo kutekeleza maazimio yote yaliyoazimiwa kwenye kikao hicho ili kuendelea kutoa matokeo chanya katika sekta hiyo.

Vile vile ametoa rai kwa wadau wa elimu kuendelea kutoa michango yao ya hali na mali katika kuinyanyua sekta ya elimu nchini ili kwa pamoja taifa la Tanzania liweze kujinasua katika umasikini kupitia elimu.

Aidha, amewataka wadau wa elimu kuwa huru katika kutoa mawazo yao bila kuogopa na kuwahakikishia kuwa milango ya ofisi hiyo iko wazi kukubali changamoto mbalimbali zinazopelekwa na inaendelea kuzitatua.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu amesema kuwa kwa pamoja mkutano huo umejadili juu ya uboreshaji wa elimu nchini hasa juu ya suala la uwazi katika mipango na utekelezaji wa bajeti za elimu.

“Ili kuboresha sekta ya elimu nchini uwazi ni jambo la msingi hivyo tunawaomba wenzetu wa mashirika na taasisi tunaosaidiana katika sekta hii wajitahidi kuweka bajeti zao wazi kama Serikali inavyofanya ili kuboresha zaidi sekta hii”, amesema Dkt. Ave Maria.

Mkutano huo umeshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakurugenzi, Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Taasisi zisizo za kiserikali.

No comments: