Sunday, December 30, 2018

VIDEO' INAYOSAMBAA MITANDAONI YAWAIBUA TFS

*Yaomba radhi wasafiri, yafafanua utaratibu kusafirisha mazao ya misitu
*Pia yamzungumzia Ofisa wake wa Misutu, kumchukulia hatua za kinidhamu 


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAKALA Wakala wa  Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  umepokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii na wadau  mbalimbali  zinazohusisha  namna  Ofisa  Misitu  wa Wilaya  ya  Korogwe mkoani Tanga ambavyo alikuwa akitekeleza majukumu ya kusimamia Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni
zake za  mwaka 2004.

Ofisa huyo  alikuwa akitekeleza  majukumu hayo kwa mujibu wa  kifungu cha 93 (Powers of officers with respect to offences) inayompa mamlaka Ofisa Misitu au Ofisa wa Jeshi  la  Polisi  kukagua,  kukamata  na  kuzuia  mazao  yanayodhaniwa  kupatikana  kinyume  na sheria.

Kwa kukumbusha tu leo kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na video inayosambaa kwa kasi kubwa ikionesha namna ambavyo wananchi wanalalamikia kitendo cha Ofisa Misutu akilumbana na abiria baada ya kulisamamisha gari na kubaini kuna vitanda vimebebwa.Hivyo kukaibuka malumbano ambayo yamechangia TFS kuamua kutoa ufafanuzi kwa vyombo vya habari.

Taarifa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) iliyotolewa leo Desemba 30,2018 imesema uongozi wa  TFS  umefanya uchunguzi wa haraka na kubaini  kuwa abiria mmoja  alikuwa akisafirisha  vitanda  viwili vipya  kwa  basi. Vitanda hivyo vililipiwa  ushuru wa Serikali kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Malipo Serikalini (GePG) na kupewa stakabadhi halali ya Desemba 26, 2018 katika kituo cha Mkata, Handeni Mkoani Tanga.

Imefafanua katika kutekeleza  majukumu  yake,  Ofisa  wao alimtaka  abiria  huyo  kuonesha  hati  ya Kusafirishia  bidhaa  hizo  kwa  mujibu  wa  Kanuni  za  Misitu  Kifungu  cha  13, sehemu ndogo ya 4 ambayo inakataza mwenye chombo chochote  cha usafiri kusafirisha mazao ya  misitu  ambayo  hayana  hati  ya  usafirishaji  ambapo  abiria  huyo  hakuwa  nayo. 

"Hata  hivyo, Ofisa  wetu  alishindwa  kutafsiri  masharti  ya  kifungu  hiki  na  mahitaji  ya  utoaji  wa  hati  ya usafirishaji  kwani  kama  msafirishaji  binafsi  kwa  matumizi  ya  nyumbani  asingeweza  kukidhi vigezo vya kuwa na hati hiyo. Hati ya usafirishaji huhitaji msafirishaji kuonesha  usajili, leseni ya  biashara, 
utambulisho  wa  mlipa  kodi  na  namba  ya  usajili  wa  chombo  kinachotumika kusafirisha mazao hayo pamoja na kuonesha vituo atakavyopaswa kukaguliwa,"imeeleza taarifa ya TFS ambayo imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano.

Imeeleza kutokana na tukio hilo Wakala wa  Huduma za Misitu Tanzania  unamwomba  radhi  abiria huyo  na umma wa watanzania kwa    tukio hilo  na usumbufu uliojitokeza na kwamba wakala unaendelea kufuatilia suala  hilo,  na  utahakikisha  kuwa  tukio  kama  hilo halijirudii  tena. Aidha hatua  za  kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za utumishi wa umma dhidi ya mtumishi aliyehusika na utoaji  wa  lugha  isiyo  na  staha  wakati  akitekeleza  sheria  ya  misitu  ambapo  alitegemewa  kutoa elimu stahiki kwa umma. Hata hivyo TFS imefafanua ikiwa mwananchi yeyote amenunua samani mpya kutoka kwa watengenezaji au wauzaji mahali popote kuhakikisha anapatiwa risiti halali kwa malipo aliyofanya. 

"Hivyo, mmiliki wa samani mpya kwa matumizi binafsi halazimiki kuwa na  Hati ya Usafirishaji anaposafirisha toka eneo moja kwenda jingine isipokuwa awe tayari kuonesha uthibitisho wa nyaraka za malipo halali ya samani hizo kwa ukaguzi pale itakapohitajika. Mwananchi  yeyote  anayesafirisha  samani  zilizotumika  kutoka  eneo  moja  hadi  jingine halazimiki kuwa hati za malipo wala kuwa na hati ya kusafirishia samani hizo. 

"Serikali  itaendelea  kufanya  mapitio  ya  Sheria  ya  Misitu  na  Kanuni  zake  ili  kuepuka mkanganyiko  wowote  wa  tafsiri  ya  sheria  unaoweza  kujitokeza  na  kuondoa  usumbufu kwa wananchi. Wakala  wa  Huduma  za  Misitu  Tanzania  unapenda  kutoa  rai  kwa  wananchi wote  kuendelea kuzingatia  Sheria  za 
uhifadhi  wa  misitu.  Aidha,  Wakala  hauna  nia  ya  kuzuia  utengenezaji, usafirishaji  na  matumizi  ya  samani  za  mbao  mahali  popote  nchini  ilimradi  tu  upatikanaji  wa malighafi  zake  uwe  umefuata  utaratibu.  Lengo  ni  kuhakikisha  kuwa  rasilimali  za  misitu zinatunzwa  na  kutumika  kwa  njia  endelevu  kwa  maendeleo  ya  Taifa. 

"Wakala  wa  Huduma  za Misitu Tanzania utaendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na watumishi wake kuhusu taratibu za  uvunaji,  usafirishaji  na  biashara  ya  mazao  ya  misitu  nchini  kupitia  njia  mbalimbali  na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi,"imesema sehemu ya taarifa hiyo ya TFS

Saturday, December 29, 2018

YANGA YAENDELEZA UBABE TPL, YAIFUNGA MBEYA CITY 2-1 SOKONE MBEYA

Na Ripota Wetu, Mbeya

Timu ya Yanga imeendelea kushikilia usukani wa ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Mbeya City mechi iliyochezwa kwenye dimba la Sokoine Jijini Mbeya.

Yanga wamefanikiwa kuibuka ushindi huo na kufikisha alama 50 akiwa amecheza michezo 18 akishinda 16 na kutoa sare michezo miwili.Katika dakika ya ... Mshambuliaji wa Kimataifa Heritier Makambo anaiandikia Yanga goli la kwanza akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajib baada ya madhambi kutokea nje ya 18.

Dakika ya 24, Mbeya City wanasawazisha goli kupitia kaa Msambuliaji wake Iddy Seleman 'Nado' na kuanza kulisakama lango la wapinzani wao ili wapate goli la kuongoza.Makambo akiwa ndani ya eneo la hatari aliweza kuwainua mashabiki wa Yanga katika dakika ya 41 akiwapeleka wana jangwani hao mapumziko wakiwa wanaongoza kwa goli 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Mbeya City wakisaka goli la kusawazisha lakini umakini wao ukiwa mdogo na kushindwa kutumia nafasi walizozipata.Mpaka filimbi ya mwisho ya mwamuzi Martin Sanya inapigwa Yanga anatoka kifua mbele kwa ushindi wa goli 2-1 akiendelea kushikilia rekodi ya kutokufungwa.Kiungo wa Yanga Feisal Salum 'Fei Toto'  na Haruna Moshi 'Boban' wakiwania mpira na mchezaji wa Mbeya City  Mpoki Mwakinyuke wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa goli 2-1.
Kiungo wa Yanga Feisal Salum 'Fei Toto'  na Haruna Moshi 'Boban' wakiwania mpira na mchezaji wa Mbeya City  Mpoki Mwakinyuke wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa goli 2-1.
Mchezaji wa Mbeya City Medson Mwakatundu akiwa anaoambana kuchukua mpira kutoka kwa Heritier Makambo wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa goli 2-1.
Kazi kaziniiiiii............................Heritier Makambo na Medson Mwakatundu
Mchezaji wa Mbeya City Mpoki Mwakinyuke akiondosha mpira mbele ya Mshambuliaji wa Yanga Mrisho Ngasa wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa goli 2-1.
Picha zote na Fadhil Attik Teammapicha Mbeya



TAMASHA KUBWA LA MKESHA WA MWAKA MPYA KUFANYIKA UWANJA WA TAIFA,KIINGILIO BURE


Tamasha kubwa la mkesha wa kufunga 2018 na kufungua mwaka 2019 linatarajiwa kufanyika Desema 31 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mkesha huo utakaokuwa wa aina yake unatarajia kumdondosha Mwanamuziki wa nyimbo za injili kutoka nchini Nigeria anaejulikana kwa jina la Chris Shalom, anayetamba na wimbo wake maarufu uitwao 'my beautifier' na nyingine nyingi.

Pamoja Na Chris Shalom pia waimbaji wengine mbalimbali mahiri kutoka hapa nchini akiwemo Jesica Honore, Goodluck Gosbert, Joel Lwaga Na John Lisu wanatarajiwa kutumbuiza katika mkesha huo.

Mkesha wa mwaka 2019 umeandaliwa na Nabii (prophet) Clear Malisa wa Passion Java ministry, kutoka ubungo kibangu jijini Dar es Salaam.Waigizaji/wachekeshaji na watu maarufu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa pia kuwepo akiwemo Pastor Kuria kutoka show ya churchchill nchini Kenya.

Katika tamasha hilo hakuna kiingilio na usafiri utatolewa kwa watu wote katika vituo vyote vikubwa vya usafiri Dar es Salaam.Mkesha wa mwaka 2019, umedhaminiwa Na Clouds media group, Elishadai shopping center Na Fair Travel adventures.

Matukio Katika Picha Maendeleo ya Ujenzi wa Mji wa Serikali

 Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe akikabidhi fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme za Wizara zote kwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi.Peter Mwaisabula walipokutana wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali jijini Dodoma leo tarehe 29 Desemba, 2018. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Titus Mwinuka. Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe akisisitiza jambo mara baada ya kukabidhi fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme za Wizara zote kwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi. Peter Mwaisabula (katikati) walipokutana wakati wa zoezi la kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali jijini Dodoma leo tarehe 29 Desemba, 2018.Wapili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Titus Mwinuka na kushoto ni Mkurugenzi wa Uwezeshaji Sekta Binafsi toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bedason Shallanda. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Titus Mwinuka (katikati) akisikiliza kwa makini maelekezo toka kwa Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe walipokutana wakati wa zoezi la kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali jijini Dodoma leo tarehe 29 Desemba, 2018 Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe akitoa maelekezo kwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi.Peter Mwaisabula (katikati) mara baada ya kumkabidhi fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme za Wizara zote wakati wa zoezi la kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali jijini Dodoma leo tarehe 29 Desemba, 2018. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Titus Mwinuka.Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe (watatu kutoka kushoto) na Mkurugenzi wa Uwezeshaji Sekta Binafsi toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bedason Shallanda (kulia kwake) wakikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo jijini Dodoma.Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe (kushoto) akikagua utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bibi. Maimnua Tarishi (hayupo picha) lilomtaka Mkandarasi anayejenga Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambaye ni Kikosi cha Ujenzi ambao walitakiwa kufuata muongozo wa Mkandarasi Mshauri ambaye ni TBA leo jijini Dodoma. Mkurugenzi wa Uwezeshaji Sekta Binafsi toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bedason Shallanda akifafanua jambo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano leo jijini Dodoma. Aliyevaa tisheti ni Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe. Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe akielezea jambo alipokuwa akikagua maendeleo ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuitaka TBA kuwa na Ofisi katika eneo unapojengwa Mji wa Serikali ili kuharakisha huduma za ushauri kwa Makandarasi wanaoendelea na ujenzi wa Ofisi za Wizara mbalimbali leo jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uwezeshaji Sekta Binafsi toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bedason Shallanda. Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe (kulia) akielezea jambo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu na Bunge) leo jijini Dodoma Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma, Bw. Meshach Bandawe (kulia) akielekeza jambo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa leo jijini Dodoma. (Picha zote na: Frank Shija - MAELEZO, Dodoma)

MAJALIWA ATEMBELEA MRADI WA UENDELEZAJI MIJI YA KIMKAKATI KATIKA JIJI LA DODOMA



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua uboreshaji wa Mandhari ya eneo la kupumzikia la Chinangali jijini Dodoma, wakati alipokagua Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika Jiji hilo, Desemba 29, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na kulia ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Gowin Kunambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Maegesho ya Malori Makubwa katika eneo la Nala jijini Dodoma, wakati alipotembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma, Desemba 29, 2018. Watatu kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde na wapili kushoto ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Maegesho ya Malori Makubwa katika eneo la Nala jijini Dodoma wakati alipotembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji hilo, Desemba 29, 2018. Watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na kulia ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utekelezaji wa agizo alilolitoa Oktoba 21, 2018 kwa uongozi wa jiji la Dodoma la kubomoa uzio wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto na kuziba barabara ya tisa katika Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Madukani jijijini Dodoma. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa katika ziara ya kukagua Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma, Desemba 29, 2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

………………………………………………………………………………….

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma na kukagua ujenzi wa maegesho ya malori makubwa katika eneo la Nala na uboreshwaji wa mandhari ya eneo la kupumzikia la Chinangalijijini Dodoma.

Pia amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi andelee kutenga maeneo ya mapumziko ili wananchi wapate sehemu za kukutana na kubadilishana mawazo baada ya kumaliza kufanya kazi. Waziri Mkuu amekagua maeneo hayo leo (Jumamosi, Desemba 29, 2018) ambapo ameupongeza uongozi wa jiji la Dodoma kwa kubuni wazo hilo na kusema kwamba ni muhimu kwa miji mikubwa kutenga maeneo ya kwa ajili ya mapumziko.

Amesema lazima jiji la Dodoma lipangwe kisasa na amewataka wahandisi wahakikishe maeneo ya mapumziko yatengwa na yanatumika kama ilivyokusudiwa. Pia amemtaka Mkurugenzi wa Jiji, Kunambi aendelee kusimamia ujenzi wa kimkakati ndani ya jiji hilo. ”Hatuwezi kuwa tumejaza nyumba kila eneo, watu hawana mahali pa kupumzika na kukutana na marafiki zao plan ya Chinangali Park ni nzuri, Jiji la Dar es Salaam plan ya awali kulikuwa na maeneo ya mapumziko lakini watu wa Idara ya Ardhi waliyauza.”

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amekagua utekelezaji wa agizo alilolitoa Oktoba 21, 2018 kwa uongozi wa jiji la Dodoma la kubomoa uzio wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto na kuziba barabara ya tisa katika Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Madukani jijijini Dodoma. Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezwaji wa agizo lake baada ya kutembelea eneo hilo na kukuta uzio umebomolewa na sasa kuna bustani iliyojengwa kwa ajili ya mapumziko na pia barabara imefunguliwa na wananchi wanaendelea kuitumia kama ilivyokuwa awali.

Uzio huo ambao mbali na kujengwa katika eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto kwenye mtaa wa Mji Mpya kata ya Madukani pia uliziba barabara ya tisa, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo. Waziri Mkuu ameendelea kusisistiza uongozi wa jiji kutenga ardhi na kupima viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya biashara, makazi, taasisi, huduma za jamii, viwanda pamoja na maeneo ya wazi kwa ajili ya mapumziko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma amesema jiji la Dodoma ni miongoni mwa majiji manane nchini yanayotekeleza mradi wa uboreshaji wa miji ya kimkakati unaofadhiliwa na Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia. Amesema katika jiji la Dodoma mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo ya Kikuyu, Chidachi, Kinyambwa, Itega, Njedengwa, Mapinduzi, Ilazo, Ipagala, Chamwino, Kilimani, Majengo, Mlezi pamoja na maingilio na stendi kuu ya mabasi na soko kuu zenye jumla ya urefu wa kilomita 26.6.

Mkurugenzi huyo amesema barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami, pia zitawekwa taa za barabarani takriban 925 zinazotumia mfumo wa umeme wa jua. Hata hivyo mradi huo utahusisha ujenzi wa kituo cha maegezo ya malori makubwa takribani 300 katika eneo la Nala.

Ameongeza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na soko kuu katika eneo la Nzuguni, ujenzi wa vituo sita vya watembea kwa miguu, ujenzi wa vizimba saba vya kukusanyia taka ngumu, uboreshaji wa mandhali ya eneo la kupumzikia katika eneo la Chinangali na ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wenye urefu wakilomita 6.5 katika eneo la Ipagala.

TBC TAFUTENI USHAURI WA MAENEO KWA WAZAWA KABLA YA KUSIMIKA MITAMBO YENU



Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Julianna Shonza akitoa maelekezo ya mambo ya kuzingatia kabla ya kusimika mitambo ya usikivu kwa Meneja wa Shirika la Utangazaji Taifa (TBC) Kanda ya Kaskazini Bw.Gerald Uisso (hayupo pichani) leo katika Kijiji cha Kwemashai alipotembelea eneo hilo walilosimika mitambo yao wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo iliyoko mitambo ya TBC kwa Kanda ya Kaskazini.
Mtambo wa kurushia matangazo ya Shirika la Utangazaji Taifa (TBC) uliyopo katika Kijiji cha Kwemashai Wilayani Lushoto ambapo Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Julianna Shonza alitembelea eneo hilo leo ikiwa ni ziara yake ya kukagua maeneo iliyopo mitambo ya TBC kufuatia changamoto ya usikivu katika maeneo hayo ya Kanda ya Kaskazini.
Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza (wapili kulia) akitizama mitambo iliyopo Lushoto, (watatu kulia)Meneja wa Shirika la Utangazaji Taifa Kanda ya Kaskazini Bw.Gerald Uisso akimwonyesha mitambo ya kurushia matangazo ya TBC iliyoko katika eneo la Kijiji cha Kwemashai alipofanya ziara yake aliyoifanya leo ya kukagua maeneo yaliyisimikwa mitambo ya TBC kutokana na kuendelea kuwepo kwa kero ya usikivu katika eneo hilo.
Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza akikagua Uwanja wa Michezo wa Sabasaba unaomilikiwa na CCM Wilaya ya Lushoto ambao uongozi wa CCM unautafutia mwekezaji wa kuuendeleza leo alipofanya ziara yake ya kikazi leo Wilayani Lushoto.
Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza akiwashauri viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Lushoto kuuendeleza uwanja wa michezo wa Sabasaba kwa kuomba wataalamu Wizarani wa kuwapa ushauri wa kiutalamu wa namna ya kuboresha uwanja huo alipotembea uwanja huo leo,wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilayani Lushoto Bw.Amiri Shekelata .

………………………..

Na Anitha Jonas – WHUSM,Lushoto -Tanga

Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo amewataka viongozi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC )kusikiliza ushauri wa wazawa wa maeneo wanayoenda kusimika mitambo yao pale wanapofanya utafiti wa maeneo yatakayofaa kulingana na Jiografia ya eneo husika.

Mheshimiwa Shonza ametoa kauli hiyo leo Wilayani Lushoto alipotembelea eneo lililowekwa mitambo ya TBC iliyoko katika eneo la Kwemashai kwa lengo la kutaka kubaini changamoto zinazosababisha kutokuwepo kwa usikivu kwa baadhi ya maeneo Wilayani hapo.

“Changamoto kubwa katika Wilaya hiyo ya Lushoto ni Jiografia ya eneo hilo kwani inamilima mingi sana kati maeneo yake yote hivyo ni vyema mkashirikiana na Halmashauri katika kuelekezana eneo abalo itakuwa na mlima mrefu zaidi kushinda yote ambao utawafaa kwakuweza kusimika mtambo wenu utakao rusha matangazo katika maeneo yote ya Wilaya hii,”alisema Mhe.Shonza.

Akiendelea kuzungumza katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo aliusisistiza uongozi wa TBC kanda ya Kaskazini kuhakikisha wanafanya utafiti huo haraka na kusimika mitambo hiyo mapema kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha inakamilisha usikivu kwa mikoa iliyoko karibu na maeneo ya mipakani kabla ya mwaka 2020 na ndiyo maana fedha za bajeti ya kuboresha usikivu zinatolewa kila mwaka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Bw.January Lugangika alimwomba Naibu Waziri huyo kuzungumza na uongozi wa TBC kuweza kuwapatia mwandishi kwa Wilaya hiyo ya Lushoto kwani kuhusu suala la ofisi tayari wamekwisha muandalia ipo.

“Tumekuwa tunapata changamoto kubwa ya mwandishi wa TBC kwani inatulazimu kumtumia mwandishi aliyeko Tanga ambaye inamlazimu kusafiri kwa basi kwa mwendo wa masaa matatu hii changamoto kwetu na Wilaya hii inafursa nyingi ya kuzitangaza na tunaamini kuwa TBC wanawza kushirikiana nasi katika kufanikisha hili,”alisema Mhe.Lugangika.

Kwa upande wa Meneja wa Shirika la Utangazaji Taifa (TBC) Bw.Gerald Uisso alieleza kuwa amapokea maelekezo yote na ofisi yake itahakikisha inazingatia ushauri na kufanikisha zoezi hilo la kuboresha usikivu mapema .

Pamoja na hayo nae Mwenyekiti wa Chama cha CCM Wilaya ya Lushoto alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa chama hicho kimeanzakutafuta mwekezaja wa kuendeleza uwanja wa michezo wa Sabasaba ilikuweza kuuweka katika hali nzuri itakayo faa kwa kutumika katika michezo mbalimbali.

SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA LATOA USHAURI KUHUSU VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

SHIRIKA la Bima la Taifa Tanzania(NIC) limeshauri kwamba ufike wakati sasa kuwepo na sera ambayo itahimiza mashirika, taasisi na wadau mbalimbali kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya vita ya dawa za kulevya nchini.

Ushauri huo umetolewa leo Desemba 28,2018 na Ofisa Masoko wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania(NIC) Israel Severe wakati wa tamasha la Kataa Mihadarati liloandaliwa na Taasisi ya Binti Filamu chini ya Mwenyekiti wake muigzaji maarufu wa filamu Ndumbagwe Misayo a.k.a Thea .Mgeni rasmi kwenye tamasha hilo alikuwa Naibu Waziri Stella Ikupa.

"Shirika la Bima la Taifa Tanzania tumeamua kushiriki kwenye tamasha hilo kutokana na kutambua umuhimu wake kwa jamii.Tunajua moja ya jukumu letu ni kushughulika na mambo ya bima lakini kwetu ni muhimu zaidi kuona jamii tunayoihudumia inakuwa salama kiafya.Sote tunatambua athari za matumizi ya
dawa za kulevya, hivyo tumeamua kushiriki kikamilifu kwenye vita hii ili kukomesha dawa hizo nchini.

"Tunashauri ifike wakati kuwe na sera ambayo itazungumzia umuhimu wa mashirika na taasisi mbalimbali nazo kushiriki kwenye vita hii ya dawa za kulevya.Hivyo ni wakati muafaka kwa Serikali kuweka sera itakayokwa chachu kwa mashirika na taasisi zote kushiriki kwa vitendo na iwe ni wajibu wetu,"amesema
Severe.

Kuhusu tamasha hilo , Severe amesema anaupongeza uongozi wa Binti Filamu kwa uamuzi wake wa kuandaa tamasha hilo lenye lengo la kutoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wao ambao wamedhamiria kwa dhati kukomesha dawa hizo nchini kwetu.

"Tunawapongeza Binti Filamu kwa kuandaa tamasha hilo ambalo kwetu sisi tunaona ni mwanzo mpya kwa wasanii kuamua kushirikiana na wadau wengine kukomesha dawa za kulevya.Wanastahili kuendelea kuungwa mkono na sisi NIC tutaendelea kuwaunga mkono kadri watakavyokuwa wanaandaa matamasha haya ya kukataa mihadarati,"amesema Severe.

Kwa upande wa Naibu Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi ,Vijana,Ajira na Wenyeulemavu Stella Ikupa ametumia nafasi hiyo kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupambana na dawa za kulevya nchini na kwamba tatizo la dawa za kulevya, hivyo unapoona kuna jitihada za wadau lazima utoe pongezi.

"Tunawapongeza Binti Filamu kwa kuandaa tamasha hilo linalofahamika kwa jina la Kataa mihadarati.Athari za dawa za kulevya kwa namna moja au nyingine zinamgusa kila mtu kwenye jamii yetu.Serikali katika kuhakikisha inakomesha dawa za kulevya iliamua kuunda mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo hakika imefanya kazi kubwa,"amefafanua Ikupa.

Ametoa ushauri kwa Binti Filamu kuhakikisha katika matamasha yanayokuja waende kwenye mikoa ambayo athari za matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na kwa kufanya hivyo watasaidia kuikoa jamii kupitia elimu ambayo wanaitoa kuhusu madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa hizo.Kuhusu mapendekezo ambayo yametolewa na wadau mbalimbali kwenye tamasha hilo yakiwemo ya Serikali kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu dawa za kulevya amesema ameyachukua na watayafanyia kazi kwani ni mambo yanayowezekana.

Akizungumzia tamasha hilo msanii wa muziki wa Bongo Fleva Haruna Kahena Inspekta Haroun amesema kitendo cha Binti Filamu kuandaa tamasha hilo ni wazi wameonesha dhamira njema ya kupambana na dawa za kulevya ambapo kwa sehemu kubwa wapo baadhi ya wasanii wamekuwa wakiyatumia.Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Simon Mwakifamba ambaye pia ni Katibu wa Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam amesema umefika wakati wa kuunga mkono juhudi za Rais Dk.John Magufuli katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Amesema kuna wasanii wengi wamekuwa wakijihusisha aidha kutumia dawa za kulevya au kugeuzwa makontena wa kubeba dawa hizo kwa maslahi ya wafanyabiashara lakini madhara yake ni makubwa, hivyo umefika wakati wa kukataa kuwa sehemu ya makontena na watumiaji wa dawa hizo.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Stella Ikupa akimkabidhi cheti Bw. Israel Severe ambaye ni Ofisa Masoko wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania(NIC) kutokana na mchango wa shirika hilo katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya wakati wa tamasha la (Kataa Mihadarati Festival) lililoandaliwa na tasisi ya Binti Filamu inayoundwa na wasanii wa filamu, tamashahilo limefanyika aktika viwanja vya Barafu Mburahati Foundation jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Stella Ikupa akimkabidhi cheti Kamishna wa Kitengo cha Tiba na Kinga kutoka Mamalaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi kutokana na mchango Mamlaka hiyo katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya wakati wa tamasha la (Kataa Mihadarati Festival) lililoandaliwa na tasisi ya Binti Filamu Foundation inayoundwa na wasanii wa filamu, tamashahilo limefanyika aktika viwanja vya Barafu Mburahati jijini Dar es salaam.
Bw. Israel Severe ambaye ni Ofisa Masoko wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania(NIC) akizungumza katika tamasha hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Mburahati Barafu jijini Dar es salaam.
Kamishna wa Kitengo cha Tiba na Kinga kutoka Mamalaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi akizungumza na wananchi waliohudhuria katika tamasha hilo.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fisoo akizungumza na wananchi waliohudhuria katika tamasha hilo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Stella Ikupa akihutubia wananchi waliofika katika tamasha hilo kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo.
Baadhi ya wasanii wa filamu wakifurahia baadhi ya burudani zilizokuwa zikitolewa katika tamasha hilo.
Baadhi ya waalikwa wakiwa katika tamasha hilo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Stella Ikup kushoto, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo na Kamishna wa Kitengo cha Tiba na Kinga kutoka Mamalaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi wakipunga mikono yao juu wakati msanii Inspector Haroun hayupo pichani alipokuwa akitumbuiza katika tamasha hilo.
Baadhi ya wasanii wa filamu wakiwa katika tamasha hilo.

NAMAINGO YAZINDUA MRADI WA ASALI MIZINGA 55000 KIBITI

Baadhi ya Wanachama wa Taasisi ya Namaingo wakiangalia moja kati ya mabanda ya ufugaji nyuki wa asali wakati wa uzinduzi Mradi wa Mizinga 55000 katika Kijiji cha Kikale, wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani.PICHA NA RICHARD MWAIKENDA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Namaingo, Ignus Augustino, akiwaongoza wanachama kuangalia mizinga.


Na Richard Mwaikenda, Kibiti.

TAASISI ya Namaingo, imezindua uwekezaji wa Mradi wa Mizinga ya nyuki wa asali 55000 wa wanachama wake katika Kijiji cha Kikale, wilyani Kibiti, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana kijiji hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Namaingo, Ignus Augustino, alisema mipango yao ni kila mwanachama kuwa atamiliki mizinga 50.

Uzinduzi huo ulifanywa mbele ya wananchama waliotoka Dar es Salaam pamoja na wanakijiji wa Kikale katika mabanda matatu yenye mizinga 200 ya kuanzia. Mizinga hiyo ipo ndani ya msitu wa miti ya mikoko inayoaminiwa kutoa daraja la kwanza la asali yenye kiwango cha kimataifa.

Augustino alisema kuwa wamejiandaa vilivyo kuutekeleza mradi huo mkubwa ambapo hivi sasa tayari watalaamu wa kutengeneza malkia wapo eneo la mradi. Urinaji ukianza baada ya miezi sita Kila mzinga utakuwa unatoa kilo 20 za asali. Naye Mwenyekiti Msaidizi wa Namaingo, Elesia Mkuru, alisema baadhi ya wanachamama walikuwa 

hawaamini kuwa mradi huo utandinduliwa, lakini sasa wameshaona ukweli wa mambo.Aliipoongeza Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kwa kuwaruhusu kuwekeza mradi huo katika misitu iiyopo mikoa ya Pwani, Iringa, Njombe, Dar es Salaam na Morogoro. Mwanachama wa Namaingo, Queen Ryoba, alisema kuwa wamefurahi sana kuona mradi huo umeanza 

kwani walikuwa wanausubiri kwa muda mrefu. Aliimpongeza sana Mkurugenzi wa Namaingo Bi Ubwa Ibrahim kwa kufanikisha mradi huo. Pia aliutaka uongozi wa taasisi hiyo kuendeleza kwa njia ya kisasa miradi mingine ikiwemo kilimo cha kisasa cha mazao mbalimbali wanayoisimamia ii wapate mavuno mazuri hivyo kuwapunguzia umaskini.

Mmoja wa wanakijiji wa Kikale ambapo mradi huo upo, Khamis Ngwaya, alifurahia kuwepo kwa mradi huo ambao anaamini utawaletea maendeleo katika kijiji chao kwani nao wameshirikishwa. Pia kwa niaba ya wenzie aliahidi kutoa ushirikiano kuulinda mradi huo na kuwasihi wanaoupinga mradi huo waachane kabisa na mlengo huo bali wajiunge kwani mradi huo ni faida kwa wananchi wa kijiji hicho, kwa baadhi kupata ajira na kipato pia.

Baada ya wanachama hao waliokuwa kwenye msafara wa mabasi madogo 6 (Coaster) kushiriki katika uzinduzi huo, waliondoka kwenda katika Kijiji cha Mbawa wilayano humo kukagua mipaka ya mashamba yao waliyogawiwa na Namaingo kwa ajili ya kuendesha kilimo cha kisasa na ufugaji pamoja na mabwa ya samaki. 
Mwenyekiti Msaidizi wa Namaingo, Elesia Mkuru, akizungumza na wanachama wakati wa uzinduzi huo ambapo, alisema baadhi ya wanachamama walikuwa hawaamini kuwa mradi huo utandinduliwa, lakini sasa wameshaona ukweli wa mambo.
Wanachama wakiangalia baadhi ya mizinga
Baadhi ya wanachama wa Namaingo wakijiandaa kupanda magari kuelekea Kijiji cha Mbawa kukagua mipaka ya mashamba yao
Wanachama wakiwa mbele ya moja ya majengo ya Namaingo wlipofika kukagua mikuza ya mashamba yao katika Kijiji cha Mbawa kwa ajili Kilimo cha Kisasa na ufugaji
Katapila lialotumika kuweka mipaka katika shamba la Wanachama la Mbawa.
Wanchama wakikagua moja ya mipaka ya mashamba yao

Friday, December 28, 2018

WAITARA AZITAKA HALMASHAURI ZOTE KUTEKELEZA MPANGO WA ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI NCHI NZIMA

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mwita Waitara amezitaka Halmashauri zote kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima kwenye Halmashauri zao bila ya kutumia kisingizio cha ukosefu wa bajeti za kufanya vikao vinavyohusu utoaji wa majina ya mitaa 

“Suala la gharama halipo, tumieni vikao vyenu vya kawaida, vya kisheria kutaja majina ya mitaa, suala la anwani za makazi na postikodi iwe ajenda mahususi ya ulinzi na usalama”, amefafanua Waitara 

“Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote nchi nzima waliopo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI wahakikishe kwamba wanatoa maelekezo mahususi kwa watendaji wote na kuhakikisha kuwa wanatoa majina ya mitaa,” amesema Waitara. Pia amewaelekeza Makatibu Tawala wote Tanzania Bara wahakikishe Halmashauri zote zinatekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi

Waitara ameongeza kuwa mpango huu unatuwezesha kujitambua na kuwatambua watu wetu wanakoishi, na nini kilichowaleta eneo hilo kama ni biashara, uwekezaji na ni muhimu kwa ulinzi na usalama wa raia. Pia amesema kuwa suala la anwani za makazi na postikodi litawasaidia viongozi wao wenyewe kuwatambua wananchi, kuwezesha ukusanyaji wa kodi na kufikisha huduma za Serikali kwa wananchi

“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anataka watanzania walipe kodi, jambo hili likitekelezwa, watanzania watalipa kodi na mpango huu wa kuwatambua wananchi utasaidia kuongeza mapato ambayo yataleta maendeleo ya taifa letu na kujenga miundombinu ya barabara, huduma za afya na elimu,” amesema Waitara

“Wenzetu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa upande wa Sekta ya Mawasiliano wametimiza majukumu yao, wanataka majina ya barabara na mitaa ili waweke namba za nyumba, naomba muwasaidie kutimiza wajibu wao, mtoe majina kwenye vikao vyenu ili Wilaya hii iwe kweli ya mfano,” amesema Waitara

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa Sengerema ni moja ya Wilaya chache zilizoteuliwa kuwa ya mfano kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi ambapo tunahitaji kila Wilaya Tanzania iwe na mitaa na majina ili tufahamu kila mtanzania anakaa wapi, hii itatusaidia katika masuala ya ulinzi, usalama na uchumi

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amekiri kuwa Sengerema imepata fursa ya kuwa Wilaya ya mfano na ya mwanzo katika utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi ambapo utekelezaji wa mpango huu kwa wilaya ya Sengerema ambayo iko mpakani itasaidia katika masuala ya ulinzi na usalama, ukusanyaji wa mapato na kodi za Serikali.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Joseph Henry Kanyumi akizungumza kwa niaba ya viongozi na watumishi waliohudhuria mafunzo ya mpango huo alisema kuwa wametambua umuhimu wa mpango huo. “Nasi tumenufaika na mafunzo hayo na ifikapo tarehe 15 Januari, 2019 tutakuwa tumekamilisha utoaji wa majina ya mitaa,” alisema Kanyumi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi alisema kuwa ni muhimu kuweka sheria ndogo ndogo katika Halmashauri ili mpango huu uweze kutekelezwa na kudhibiti ujenzi holela pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili mfumo huu uweze kufanya kazi

Mpango wa Anwani za Makazi na Postikodi ulianza kutekelezwa kwa majaribio mwaka 2009 kwenye mikoa minne ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Zanzibar ambapo sasa utekelezaji huo unaendelea kwenye Halmashauri 12 na utafanyika kwenye Halamshauri zote nchi nzima. Aidha, hadi sasa kata zote nchi nzima zina postikodi ambazo zimeridhiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) ambapo tangazo la Serikali Na. 220 lilitolewa kwa mara ya kwanza tarehe 22 Juni mwaka 2012 na kuboreshwa na kutolewa tena tangazo la Serikali Na. 140 tarehe 22 Aprili mwaka 2016. Vile vile, Serikali imeandaa mwongozo wa postikodi na anwani za makazi ili watendaji wa Halmashauri waweze kuzingatia na kutumia kufanikisha utekelezaji wa mpango huu

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara wakiwa wanatoka kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema (hayupo pichani) wakati wa ziara yao wilayani humo ya utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi
 Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara akizungumza na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi wakiwa Nyehunge, Mwanza. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, wa tatu kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi na wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi yaliyofanyika Nyehunge, Mwanza. Wa nne kushoto ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara na pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi
 Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara (wa tatu kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao Wilayani humo
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi James Kilaba akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara (wa pili kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao wilayani Sengerema.  Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Kipole.