Naibu
Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mwita Waitara amezitaka Halmashauri zote kutekeleza mpango wa
anwani za makazi na postikodi nchi nzima kwenye Halmashauri zao bila ya
kutumia kisingizio cha ukosefu wa bajeti za kufanya vikao vinavyohusu
utoaji wa majina ya mitaa
“Suala
la gharama halipo, tumieni vikao vyenu vya kawaida, vya kisheria kutaja
majina ya mitaa, suala la anwani za makazi na postikodi iwe ajenda
mahususi ya ulinzi na usalama”, amefafanua Waitara
“Wakurugenzi
wote wa Halmashauri zote nchi nzima waliopo chini ya Ofisi ya Rais –
TAMISEMI wahakikishe kwamba wanatoa maelekezo mahususi kwa watendaji
wote na kuhakikisha kuwa wanatoa majina ya mitaa,” amesema Waitara. Pia
amewaelekeza Makatibu Tawala wote Tanzania Bara wahakikishe Halmashauri
zote zinatekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi
Waitara
ameongeza kuwa mpango huu unatuwezesha kujitambua na kuwatambua watu
wetu wanakoishi, na nini kilichowaleta eneo hilo kama ni biashara,
uwekezaji na ni muhimu kwa ulinzi na usalama wa raia. Pia amesema kuwa
suala la anwani za makazi na postikodi litawasaidia viongozi wao wenyewe
kuwatambua wananchi, kuwezesha ukusanyaji wa kodi na kufikisha huduma
za Serikali kwa wananchi
“Mhe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
anataka watanzania walipe kodi, jambo hili likitekelezwa, watanzania
watalipa kodi na mpango huu wa kuwatambua wananchi utasaidia kuongeza
mapato ambayo yataleta maendeleo ya taifa letu na kujenga miundombinu ya
barabara, huduma za afya na elimu,” amesema Waitara
“Wenzetu
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa upande wa Sekta ya
Mawasiliano wametimiza majukumu yao, wanataka majina ya barabara na
mitaa ili waweke namba za nyumba, naomba muwasaidie kutimiza wajibu wao,
mtoe majina kwenye vikao vyenu ili Wilaya hii iwe kweli ya mfano,”
amesema Waitara
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema
kuwa Sengerema ni moja ya Wilaya chache zilizoteuliwa kuwa ya mfano
kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi ambapo tunahitaji
kila Wilaya Tanzania iwe na mitaa na majina ili tufahamu kila mtanzania
anakaa wapi, hii itatusaidia katika masuala ya ulinzi, usalama na uchumi
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amekiri kuwa Sengerema
imepata fursa ya kuwa Wilaya ya mfano na ya mwanzo katika utekelezaji wa
mpango wa anwani za makazi na postikodi ambapo utekelezaji wa mpango
huu kwa wilaya ya Sengerema ambayo iko mpakani itasaidia katika masuala
ya ulinzi na usalama, ukusanyaji wa mapato na kodi za Serikali.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Buchosa, Joseph Henry Kanyumi akizungumza kwa niaba
ya viongozi na watumishi waliohudhuria mafunzo ya mpango huo alisema
kuwa wametambua umuhimu wa mpango huo. “Nasi tumenufaika na mafunzo hayo
na ifikapo tarehe 15 Januari, 2019 tutakuwa tumekamilisha utoaji wa
majina ya mitaa,” alisema Kanyumi
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi alisema kuwa ni
muhimu kuweka sheria ndogo ndogo katika Halmashauri ili mpango huu uweze
kutekelezwa na kudhibiti ujenzi holela pamoja na kuendelea kutoa elimu
kwa wananchi ili mfumo huu uweze kufanya kazi
Mpango
wa Anwani za Makazi na Postikodi ulianza kutekelezwa kwa majaribio
mwaka 2009 kwenye mikoa minne ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na
Zanzibar ambapo sasa utekelezaji huo unaendelea kwenye Halmashauri 12 na
utafanyika kwenye Halamshauri zote nchi nzima. Aidha, hadi sasa kata
zote nchi nzima zina postikodi ambazo zimeridhiwa na Umoja wa Posta
Duniani (UPU) ambapo tangazo la Serikali Na. 220 lilitolewa kwa mara ya
kwanza tarehe 22 Juni mwaka 2012 na kuboreshwa na kutolewa tena tangazo
la Serikali Na. 140 tarehe 22 Aprili mwaka 2016. Vile vile, Serikali
imeandaa mwongozo wa postikodi na anwani za makazi ili watendaji wa
Halmashauri waweze kuzingatia na kutumia kufanikisha utekelezaji wa
mpango huu
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza
kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI
Mwita Waitara wakiwa wanatoka kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Sengerema (hayupo pichani) wakati wa ziara yao wilayani humo ya
utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi
Naibu
Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara akizungumza na
viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo
pichani) kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi
wakiwa Nyehunge, Mwanza. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, wa tatu kulia ni Naibu Katibu
Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi na wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya
ya Sengerema, Emmanuel Kipole
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye
akifafanua jambo kwa viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema
na Buchosa (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu
utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi yaliyofanyika
Nyehunge, Mwanza. Wa nne kushoto ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Mwita Waitara na pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa
Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi
Mkuu
wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole akifafanua jambo kwa Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne
kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita
Waitara (wa tatu kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao
Wilayani humo
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi James Kilaba
akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Mwita Waitara (wa pili kushoto) kuhusu kituo cha telesenta
wakati wa ziara yao wilayani Sengerema. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa
Wilaya hiyo, Emmanuel Kipole.
No comments:
Post a Comment