Friday, December 28, 2018

WAZIRI MKUU AFANYIA KIKAO CHA MAWAZIRI IHUMWA

*Aagiza wakae na wakandarasi wao na kupima kama watamaliza kazi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Mawaziri na Makatibu Wakuu kwenye eneo la tenki la maji la kutolea huduma katika ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba badala ya ukumbi wa Hazina kama alivyokuwa amepanga awali.

Akiwa Ihumwa, Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri wafike kwenye maeneo ya ujenzi wa ofisi zao, watathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara na pale watakapojiridhisha kuwa uwezo wao ni mdogo, wawabadilishe mara moja.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Ijumaa, Desemba 28, 2018) akiwa kwenye kikao cha kazi (site meeting) na mawaziri 15 na manaibu mawaziri katika eneo la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

“Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu hapa site ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapa mrejesho Mawaziri juu ya changamoto alizokutana nazo jana alipofanya ukaguzi wa ujenzi kwa kila wizara. “Nataka Mawaziri ambao ofisi zao zinajengwa wa watu wa Mzinga, wakae nao na kutathmini uwezo wao na kama mtaona hawawezi, mkabidhi kwa mkandarasi mwingine,” amesema Waziri Mkuu.

Amewataka wakandarasi wahakikishe wanaongeza idadi ya vibarua ili kazi hiyo iweze kwenda haraka. “Wizara iliyofanya vizuri kuliko zote ni ya Utumishi, wao wako hatua nzuri. Kwa maana ya uchapaji kazi, eneo nililokuta lina wafanyakazi wengi ni magereza,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna wagongaji wa kokoto ambao wamepokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.

“Waziri wa Madini aongee nao hawa watu ili warejee na kufanya kazi kwa sababu baadhi yao wameshapokea fedha na mahitaji ya kokoto hapa ni makubwa na aliyebakia akifanya kazi ni Nyanza Road Works peke yake,” alisema.

Naye Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alimweleza Waziri Mkuu kwamba wizara yake imetoa transforma tisa za kusaidia kupoza umeme lakini ni wizara nne ambazo zimejitokeza na kulipia line za transforma hizo.

“Wizara yetu tumetoa transforma tisa za kusaidia umeme upatikane eneo la ujenzi. Niwaombe mawaziri waliopo, walipie service linetu ambazo gharama yake ni sh. 921,000 ili wafungiwe transforma na kazi iweze kufanyika mchana na usiku. Hadi sasa, tumeshapokea maombi kutoka  wizara nne tu za Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati ili kazi imalizike ndani ya muda mfupi,” alisema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,                      
IJUMAA, DESEMBA 28, 2018.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati alipowasili kwenye eneo la Ihumwa jijini Dodoma, unapojengwa Mji wa Serikali kukutana na Mawaziri na Makatibu Wakuu, Desemba 28, 2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Augustine  Mahiga, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mawaziri na Makatibu Wakuu kwenye eneo la Ihumwa jijini  Dodoma unapojengwa mji wa Serikali, Desemba 28, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt. Maulid Banyani baada ya kuzungumza na Mawaziri na Makatibu Wakuu kwenye eneo la Ihumwa jijini Dodoma unapojengwa Mji wa Serikali, Desemba 28, 2018.  Katikati ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi baada ya kuzungumza na Mawaziri na Makatibu Wakuu kwenye eneo la Ihumwa jijini Dodoma unapojengwa mji wa serikali, Desemba 28, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

No comments: