Friday, December 28, 2018

RAIS MAGUFULI AREJESHA KIKOKOTOO CHA ZAMANI KWA WASTAAFU....SHANGWE ZALIPUKA IKULU

* Asema kustaafu sio dhambi bali ni heshima kwa Taifa
* Asisitiza hakuna sababu ya kuwasumbua wastaafu

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

RAIS Dk.John Magufuli amerejesha matumaini mapya kwa wafanyakazi na kuagiza wastaafu wote nchini walipwe kwa kutumia kikotoo cha zamani cha asilimia 50.

Pamoja na hilo amesema kuwa kustaafu si dhambi bali ni heshima kwa Taifa.
Ametoa uamuzi huo leo hii Desemba 28, mwaka 2018 katika kikao chake kilichohudhuriwa na wadau wote wa mifuko ya hifadhi ya jamii ,wafanyakazi na viongozi wa ngazi mbalimbali wa mifuko hiyo.

Baada ya Rais kutangaza kutumika kwa kikotoo cha zamani ukumbi wa Ikulu uligeuka kuwa sehemu ya shangwe ambapo nyimbo za mshikamano kwa wafanyakazi zilianza kuimbwa huku Rais akiwaambia "Wafanyakazi Hoyee...wafanyakazi ni muhimu katika kipindi hiki na lazima wapewe stahiki zao na fomuka nzuri ni ile ya kuboresha maslahi ya watu na sio kuwa na fomula inayotesa wafanyakazi."

Akifafanua wakati anatoa uamuzi huo Rais Mafuli amesema kwamba "kustaafu si dhambi bali ni jambo la heshima. Anayestaafu anastahili kuheshimiwa na Taifa hili na hivyo hatakiwi kupata shida , kikokotoo kilichokuwa kinatumika huko nyuma kitumike katika kipindi hiki cha mpito hadi mwaka 2023," amesema Rais huku akishangiliwa.

Amefafanua kuwa kwa takwimu alizonazo ni kwamba kwa kipindi cha mpito ambacho ni kuanzia sasa hadi mwaka 2023 watakaostaafu ni wanachama 58, 000 na hao walipwe kwa kikotoo cha asilimia 50 huku akisisitiza mifuko yote ilipe kama ilivyokuwa inalipa awali.

Ameongeza kuwa Serikali iliyopo madarakani imeweka mfumo imara wa ukusanyaji kodi na miongoni mwa walipa kodi wazuri ni wafanyakazi na hivyo lazima waendelee kulipwa kama zamani ndani ya kipindi hicho cha mpito .

Awali kabla ya uamuzi huo Rais Magufuli alieleza kuwa maelezo yanayotolewa kuhusu mafao yamekuwa ya kitaalamu zaidi.Hivyo amesema kustaafu ni jambo la heshima kwa anayestaafu kwani mfanyakazi anakuwa amejitolea kwa miaka yote halafu mwishoni anakuja kusumbuliwa baada ya kustaafu.

Amesema kuwa yeye amefanya kazi kuanzia mwaka 1981 na anajua changamoto na hayupo tayari kuwachanganya wafanyakazi.Hata hivyo ameelezea historian ya kuunganishwa kwa mifuko ambapo amefafanua Oktoba 20 mwaka 217 kwenye baraza la mawaziri walipitisha uamuzi wa kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kisha ibaki mifuko miwili ambayo ni NSSF na PSSSF kwa lengo la kuhakikisha mifuko hiyo inatimiza wajibu wake.

Amesema hatua hiyo ilitokana na ombi la muda mrefu la wafanyakazi baada ya kuona mifuko hiyo inaelekea kufa.Hivyo baadae Bunge lilipitisha sheria.
Amesema jumla ya wanachama wa mifuko yote ni milioni 1.267 na kwamba mwanachama anachangia asilimia 10 na mwajiri anachangia asilimia 10 na mfuko ili ufanye kazi lazima mwajiri achangie na muajiriwa achangie.

Amefafanua kuwa mifuko baadhi ya ilikuwa inaendeshwa kiajabu ajabu na mingine ilikuwa imejikita kwenye ujenzi wa majengo kwasababu kulikuwa na asilimia 10.Amesema waliokabidhiwa kutunza mifuko ndio waliokuwa wanaamua aina ya miradi bila kushirikisha wadau na kwamba wakati Serikali ya awamu ya Tano inaingia madarakani walikuta deni la zaidi ya Sh.trilioni 1.2 na wamefanikiwa kulipa madeni yote.

"Sh.Trilioni 1.23 ambazo Serikali imelipa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.Kuna deni la Sh.bilioni 740 nazo zitalipwa kabla ya Januari mwakani na kati ya hizo Sh.bilioni 500 zimelipwa tayari kwa wanachama 8000 waliokuwa wanadai mafao yao.

Baada ya ufafanuzi huo Rais Magufuli amesema pamoja na changamoto hizo bado lazima ufumbuzi upatikane ili kuondoa malalamiko yaliyopo.Amesema wafanyakazi wamefanya kazi zao kwa uadilifu na hivyo anatarajia kupata mafao yake.Na kwamba anatambua kuna wafanyakazi wanataka mafao halafu anaambia asubiri.

Mkuu hiyo wa nchi alihoji iwapo mbunge akimaliza muda wake anapewa stahiki sake zote lakini kwa wastaafu wengine wanaambiwa watalipwa kidogokidogo.Pia amefafanua Serikali inatoa Sh.bilioni 126 kwa mwezi kwa ajili ya michango ya wafanyakazi na hapo hapo lazima mishahara yao ilipwe ambayo ni Sh.bilioni 560.Amesema ili kukabiliana na mambo yote hayo lazima kunahatua zichukuliwe kuhakikisha mambo yanakwenda sawasawa.

"Makatibu wakuu wa wakati ule walishiriki kutengeneza fomula ya ukokotoaji kwani nao waliokuwa wananufaika,"amesema Rais.

Rais Magufuli ametoa ombi kwa mifuko ya hifadhi waboreshe daftari la wastaafu kwa mifuko ili kuondoa wastaafu hewa kwani kama kulikuwa na wafanyakazi hewa,mbolea hewa, wanafunzi hewa lazima kutakuwa na wastaafu hewa au ambao wanalipwa mara mbili.

Hivyo amewataka wadau wa mifuko kuhakikisha wanapitia upya orodha ya wanachama wa mifuko hiyo na hilo ndilo agizo lake la kwanza.Agizo la pili mifuko ya hifadhi watumie vizuri fedha za wanachama amesema wanaweza wakawa wanaona tatizo ni kikokotoo kumbe changamoto ni matumizi mabaya ya fedha.

Amesema kuna hifadhi inatumia Sh. bilioni 1.3 kwa ajili ya kutengeneza kalenda ,pia imeajiri walinzi ambao wanalipa zaidi ya Sh.bilioni 3 kwa mwaka.Hivyo lazima matumizi ya fedha yawe ya uangalifu.

Amesisitiza ni marufuku kufanya uwekezaji ambao hauna tija na kwamba kibaya zaidi wanachama hawahusiki kwenye kuamua katika kupanga aina ya miradi.

No comments: