Sunday, December 30, 2018

VIDEO' INAYOSAMBAA MITANDAONI YAWAIBUA TFS

*Yaomba radhi wasafiri, yafafanua utaratibu kusafirisha mazao ya misitu
*Pia yamzungumzia Ofisa wake wa Misutu, kumchukulia hatua za kinidhamu 


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAKALA Wakala wa  Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  umepokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii na wadau  mbalimbali  zinazohusisha  namna  Ofisa  Misitu  wa Wilaya  ya  Korogwe mkoani Tanga ambavyo alikuwa akitekeleza majukumu ya kusimamia Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni
zake za  mwaka 2004.

Ofisa huyo  alikuwa akitekeleza  majukumu hayo kwa mujibu wa  kifungu cha 93 (Powers of officers with respect to offences) inayompa mamlaka Ofisa Misitu au Ofisa wa Jeshi  la  Polisi  kukagua,  kukamata  na  kuzuia  mazao  yanayodhaniwa  kupatikana  kinyume  na sheria.

Kwa kukumbusha tu leo kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na video inayosambaa kwa kasi kubwa ikionesha namna ambavyo wananchi wanalalamikia kitendo cha Ofisa Misutu akilumbana na abiria baada ya kulisamamisha gari na kubaini kuna vitanda vimebebwa.Hivyo kukaibuka malumbano ambayo yamechangia TFS kuamua kutoa ufafanuzi kwa vyombo vya habari.

Taarifa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) iliyotolewa leo Desemba 30,2018 imesema uongozi wa  TFS  umefanya uchunguzi wa haraka na kubaini  kuwa abiria mmoja  alikuwa akisafirisha  vitanda  viwili vipya  kwa  basi. Vitanda hivyo vililipiwa  ushuru wa Serikali kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Malipo Serikalini (GePG) na kupewa stakabadhi halali ya Desemba 26, 2018 katika kituo cha Mkata, Handeni Mkoani Tanga.

Imefafanua katika kutekeleza  majukumu  yake,  Ofisa  wao alimtaka  abiria  huyo  kuonesha  hati  ya Kusafirishia  bidhaa  hizo  kwa  mujibu  wa  Kanuni  za  Misitu  Kifungu  cha  13, sehemu ndogo ya 4 ambayo inakataza mwenye chombo chochote  cha usafiri kusafirisha mazao ya  misitu  ambayo  hayana  hati  ya  usafirishaji  ambapo  abiria  huyo  hakuwa  nayo. 

"Hata  hivyo, Ofisa  wetu  alishindwa  kutafsiri  masharti  ya  kifungu  hiki  na  mahitaji  ya  utoaji  wa  hati  ya usafirishaji  kwani  kama  msafirishaji  binafsi  kwa  matumizi  ya  nyumbani  asingeweza  kukidhi vigezo vya kuwa na hati hiyo. Hati ya usafirishaji huhitaji msafirishaji kuonesha  usajili, leseni ya  biashara, 
utambulisho  wa  mlipa  kodi  na  namba  ya  usajili  wa  chombo  kinachotumika kusafirisha mazao hayo pamoja na kuonesha vituo atakavyopaswa kukaguliwa,"imeeleza taarifa ya TFS ambayo imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano.

Imeeleza kutokana na tukio hilo Wakala wa  Huduma za Misitu Tanzania  unamwomba  radhi  abiria huyo  na umma wa watanzania kwa    tukio hilo  na usumbufu uliojitokeza na kwamba wakala unaendelea kufuatilia suala  hilo,  na  utahakikisha  kuwa  tukio  kama  hilo halijirudii  tena. Aidha hatua  za  kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za utumishi wa umma dhidi ya mtumishi aliyehusika na utoaji  wa  lugha  isiyo  na  staha  wakati  akitekeleza  sheria  ya  misitu  ambapo  alitegemewa  kutoa elimu stahiki kwa umma. Hata hivyo TFS imefafanua ikiwa mwananchi yeyote amenunua samani mpya kutoka kwa watengenezaji au wauzaji mahali popote kuhakikisha anapatiwa risiti halali kwa malipo aliyofanya. 

"Hivyo, mmiliki wa samani mpya kwa matumizi binafsi halazimiki kuwa na  Hati ya Usafirishaji anaposafirisha toka eneo moja kwenda jingine isipokuwa awe tayari kuonesha uthibitisho wa nyaraka za malipo halali ya samani hizo kwa ukaguzi pale itakapohitajika. Mwananchi  yeyote  anayesafirisha  samani  zilizotumika  kutoka  eneo  moja  hadi  jingine halazimiki kuwa hati za malipo wala kuwa na hati ya kusafirishia samani hizo. 

"Serikali  itaendelea  kufanya  mapitio  ya  Sheria  ya  Misitu  na  Kanuni  zake  ili  kuepuka mkanganyiko  wowote  wa  tafsiri  ya  sheria  unaoweza  kujitokeza  na  kuondoa  usumbufu kwa wananchi. Wakala  wa  Huduma  za  Misitu  Tanzania  unapenda  kutoa  rai  kwa  wananchi wote  kuendelea kuzingatia  Sheria  za 
uhifadhi  wa  misitu.  Aidha,  Wakala  hauna  nia  ya  kuzuia  utengenezaji, usafirishaji  na  matumizi  ya  samani  za  mbao  mahali  popote  nchini  ilimradi  tu  upatikanaji  wa malighafi  zake  uwe  umefuata  utaratibu.  Lengo  ni  kuhakikisha  kuwa  rasilimali  za  misitu zinatunzwa  na  kutumika  kwa  njia  endelevu  kwa  maendeleo  ya  Taifa. 

"Wakala  wa  Huduma  za Misitu Tanzania utaendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na watumishi wake kuhusu taratibu za  uvunaji,  usafirishaji  na  biashara  ya  mazao  ya  misitu  nchini  kupitia  njia  mbalimbali  na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi,"imesema sehemu ya taarifa hiyo ya TFS

No comments: