Saturday, December 29, 2018

MAJALIWA ATEMBELEA MRADI WA UENDELEZAJI MIJI YA KIMKAKATI KATIKA JIJI LA DODOMA



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua uboreshaji wa Mandhari ya eneo la kupumzikia la Chinangali jijini Dodoma, wakati alipokagua Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika Jiji hilo, Desemba 29, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na kulia ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Gowin Kunambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Maegesho ya Malori Makubwa katika eneo la Nala jijini Dodoma, wakati alipotembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma, Desemba 29, 2018. Watatu kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde na wapili kushoto ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Maegesho ya Malori Makubwa katika eneo la Nala jijini Dodoma wakati alipotembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji hilo, Desemba 29, 2018. Watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na kulia ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utekelezaji wa agizo alilolitoa Oktoba 21, 2018 kwa uongozi wa jiji la Dodoma la kubomoa uzio wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto na kuziba barabara ya tisa katika Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Madukani jijijini Dodoma. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa katika ziara ya kukagua Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma, Desemba 29, 2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

………………………………………………………………………………….

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma na kukagua ujenzi wa maegesho ya malori makubwa katika eneo la Nala na uboreshwaji wa mandhari ya eneo la kupumzikia la Chinangalijijini Dodoma.

Pia amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi andelee kutenga maeneo ya mapumziko ili wananchi wapate sehemu za kukutana na kubadilishana mawazo baada ya kumaliza kufanya kazi. Waziri Mkuu amekagua maeneo hayo leo (Jumamosi, Desemba 29, 2018) ambapo ameupongeza uongozi wa jiji la Dodoma kwa kubuni wazo hilo na kusema kwamba ni muhimu kwa miji mikubwa kutenga maeneo ya kwa ajili ya mapumziko.

Amesema lazima jiji la Dodoma lipangwe kisasa na amewataka wahandisi wahakikishe maeneo ya mapumziko yatengwa na yanatumika kama ilivyokusudiwa. Pia amemtaka Mkurugenzi wa Jiji, Kunambi aendelee kusimamia ujenzi wa kimkakati ndani ya jiji hilo. ”Hatuwezi kuwa tumejaza nyumba kila eneo, watu hawana mahali pa kupumzika na kukutana na marafiki zao plan ya Chinangali Park ni nzuri, Jiji la Dar es Salaam plan ya awali kulikuwa na maeneo ya mapumziko lakini watu wa Idara ya Ardhi waliyauza.”

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amekagua utekelezaji wa agizo alilolitoa Oktoba 21, 2018 kwa uongozi wa jiji la Dodoma la kubomoa uzio wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto na kuziba barabara ya tisa katika Mtaa wa Mji Mpya Kata ya Madukani jijijini Dodoma. Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezwaji wa agizo lake baada ya kutembelea eneo hilo na kukuta uzio umebomolewa na sasa kuna bustani iliyojengwa kwa ajili ya mapumziko na pia barabara imefunguliwa na wananchi wanaendelea kuitumia kama ilivyokuwa awali.

Uzio huo ambao mbali na kujengwa katika eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto kwenye mtaa wa Mji Mpya kata ya Madukani pia uliziba barabara ya tisa, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo. Waziri Mkuu ameendelea kusisistiza uongozi wa jiji kutenga ardhi na kupima viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya biashara, makazi, taasisi, huduma za jamii, viwanda pamoja na maeneo ya wazi kwa ajili ya mapumziko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma amesema jiji la Dodoma ni miongoni mwa majiji manane nchini yanayotekeleza mradi wa uboreshaji wa miji ya kimkakati unaofadhiliwa na Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia. Amesema katika jiji la Dodoma mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo ya Kikuyu, Chidachi, Kinyambwa, Itega, Njedengwa, Mapinduzi, Ilazo, Ipagala, Chamwino, Kilimani, Majengo, Mlezi pamoja na maingilio na stendi kuu ya mabasi na soko kuu zenye jumla ya urefu wa kilomita 26.6.

Mkurugenzi huyo amesema barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami, pia zitawekwa taa za barabarani takriban 925 zinazotumia mfumo wa umeme wa jua. Hata hivyo mradi huo utahusisha ujenzi wa kituo cha maegezo ya malori makubwa takribani 300 katika eneo la Nala.

Ameongeza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na soko kuu katika eneo la Nzuguni, ujenzi wa vituo sita vya watembea kwa miguu, ujenzi wa vizimba saba vya kukusanyia taka ngumu, uboreshaji wa mandhali ya eneo la kupumzikia katika eneo la Chinangali na ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wenye urefu wakilomita 6.5 katika eneo la Ipagala.

No comments: