Friday, December 14, 2018

Mkuu wa Wilaya ya Magu Adhamiria Kuleta Ustawi wa Wananchi Wanyonge

Mkuu wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza  Mhe. Philemon Sengati  amesema kuwa  Dhamira yake ni Kuhakikisha kuwa Ustawi wa Wananchi hasa Wanyonge Unafikiwa kwa Wakati kama ilivyo Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano. Akizungumza wakati akifunga mafunzo  ya kuwajengea uwezo   wakulima  200 wa  vijiji vya Shinembo na Kitongosima Wilayani humo yakilenga kuwawezesha kutumia rasilimali ardhi kujiletea maendeleo baada yakurasimisha maeneo yao na kupatiwa hati za kimila za kumiliki ardhi.

“Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa tunaleta ustawi wa wananchi na hasa wale wanyonge kwa kuhakikisha kuwa wanapata haki zao katika maeneo yote ambayo yanalenga kuwawezesha wananchi kujikwamua ndio maana tunawasisitiza kufanya kazi kwa bidii”; Alisisitiza Mhe. Sengati Akifafanua amesema kuwa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania umefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kufanikisha urasimishaji wa mashamba ya wakulima hao na kuandaa na kutoa jumla ya Hati Milki za kimila 1383 .

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Mhe. Sengati amesema kuwa kati ya wakulima 2,690 waliopimiwa mashamba yao ni wakulima 200 waliobahatika kupata mafunzo hayo yakuwajengea uwezo ili waweze kushiriki katika kutekeleza dhana ya kilimo biashara hivyo jukumu lao ni kutumia vizuri mafunzo waliyopata na kuwashirikisha elimu hiyo wananchi wengine ambao hawakupata bahati ya kushiriki katika mafunzo hayo.

Akieleza faida za wananchi kurasimishiwa mashamba yao na kupewa hati Mhe. Sengeti amesema kuwa ni pamoja na kuondoa migogoro ya mara kwa mara, kuongeza thamani ya mashamba hayo, kuwawezesha wananchi kupata mikopo katika taasisi za fedha yakiwemo mabenki, kupanua wigo wa fursa katika vijiji husika. Pia aliwaasa watendaji katika Wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa weledi katika kuwahudumia wananchi  na kutoa kipaumbele katika kusimamia haki katika huduma zote zinazotolewa.

“ Wananchi wa Wilaya ya Magu naomba muunge mkono juhudi za Serikali yenu ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kuwa mnapata maendeleo  na wakati wote mnatendewa haki na hakuna wananchi anayepoteza haki ndio maana Mhe. Rais, Dkt. Magufuli amenileta hapa nisaidieane nanyi kuleta mageuzi ya kweli katika kuwaletea maendeleo”. Alisisitiza Mhe.  Sengati Mafunzo kwa wakulima hao 200 yamejikita katika stadi za kilimo bora cha mpunga na dengu, utunzaji wa kumbukumbu za kilimo na biashara, Uthamini wa ardhi na utunzaji wa mazingira, utafutaji wa fursa za kiuchumi na kuzitumia, uandishi wa mpango wa biashara na uundaji wa vikundi vya uchumi na vikundi hiari na huduma zitolewazo na taasisi za fedha hususan mabenki.

Aliongeza kuwa Wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki katika maeneo yote ya kutolea huduma ikiwemo hospitali na kwingineko ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya uwajibikaji na kuleta ustawi kwa wananchi. Kwa upande wake Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini Bw. Antony Temu amesema kuwa lengo la mafunzo kwa wakulima hao ni kuwajengea uwezo wa kutekeleza dhana ya kilimo Biashara ili kujikwamua  kiuchumi kwa kuzalisha kwa kuzingatia mbinu za kilimo cha kisasa.

Aliongeza kuwa wananchi hao sasa wamepata ujuzi unaolenga kuleta ukombozi wa kweli na ustawi wa wananchi hao na tayari wananchi hao wameonesha mwamko katika kutekeleza malengo yatakayochea maendeleo kwa kutumia mbinu walizojifunza. “ Tayari baadhi ya wananchi wameanza kufungua akaunti  benki na kusajili vikundi vyao ili waweze kujikita katika kuzalisha na kuleta ustawi wa maisha yao”. Alisisitiza Temu.

Mafunzo kwa wakulima 200 wa Wilayani Magu yameratibiwa na kuendeshwa na mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania  (MKURABITA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza.
 Mkuu wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza akizungumza na wanachi walioshiriki katika mafunzo yakuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza dhana ya kilimo biashara katika Wilaya hiyo, mafunzo hayo yameratibiwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwashirikisha wakulima 200, Kushoto ni mwenyekiti wa mafunzo hayo Bw. Benet Makongoro na kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi. Atupele Mwaikuju.
 Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoka MKURABITA Bw. Antony Temu akisisitiza faida za mafunzo kwa wakulima wa vijiji vya Shinembo na Kitongosima vya Wilayani Magu Mkoani Mwanza.
 Sehemu ya Wananchi wa  wakionesha hati ya kimila ya kumiliki ardhi wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza dhana ya kilimo biashara kwa vitendo.
  Sehemu ya wananchi walioshiriki katika mafunzo yakuwajengea uwezo ili watekeleze dhana ya kilimo biashara.
 Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoka MKURABITA  Bw. Antony Temu akisisitiza jambo kwa wakulima 200 Wilayani humo ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wao kupitia sekta ya kilimo baada yakujengewa uwezo ili waweze kutekeleza miradi yakujiletea maendeleo ikiwemo kutekeleza kwa vitendo dhana ya kilimo biashara.
(Picha na MAELEZO)


No comments: