Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanajenga madarasa 122 na matundu ya vyoo ili wanafunzi 4,731 waliobaki kujiunga kidato cha kwanza waweze kuanza masomo ,ifikapo January 30 mwaka 2019.
Aidha amewaelekeza ,kufuatilia shule za msingi kumi zilizofanya vibaya kimkoa na kuhakikisha wanachukua hatua mahsusi. Pamoja na hayo, Ndikilo amekemea walimu wavivu na kuwataka wafanye kazi kwa molari ili kuinua ufaulu na taaluma kwa wanafunzi.
Akitoa maagizo katika kikao cha kamati ya uchaguzi wa wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza mkoani hapo, alieleza wanafunzi 4,731 hawatapata nafasi hivyo watasubiri hadi ujenzi ukamilike awamu ya II. Alisema, endapo halmashauri zingekamilisha wajibu wake wa kujenga majengo ya madarasa hali hiyo isingetokea.
Mkuu huyo wa mkoa alitaja takwimu kihalmashauri ambapo wanafunzi 487 halmashauri ya Bagamoyo hawana nafasi, Chalinze 103, Kibaha Vijijini 285,Kibaha Mjini 711 na Kibiti 537 . Ndikilo alitaja halmashauri ya Kisarawe wanafunzi 324,Mkuranga 1,071 na Rufiji 213 .
"Halmashauri zote zilizobakiza wanafunzi zijipange, mjiwekee mkakati kuondoa tatizo hili ili watoto waweze kwenda shule "Watumieni wadau wa elimu na wawekezaji kushirikiana kwenye hili "alisisitiza Ndikilo. Ofisa elimu mkoani Pwani, Abdul Maulid, aliahidi kutekeleza maagizo waliyopewa na mkuu huyo wa mkoa kwani zipo wilaya ambazo zinaendelea na zoezi la kukamilisha ujenzi huo.
Alisema, kwa mwaka 2018 mkoa wa Pwani umepanda na kushika nafasi ya 11 kitaifa ukilinganisha na 2017 ambapo ilishika nafasi ya 19 kitaifa.
No comments:
Post a Comment