Sunday, December 23, 2018

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA UJENZI



Karibu Tuelimishane Mambo Muhimu Kadhaa Ya Kuzingatia Kabla Ya Kuanza Ujenzi

Unaweza Ku-Share Na Watu Zaidi Ujumbe Huu, Unaweza Ukawasaidia Sasa Au Hata Wakati Mwingine Kwa Namna Moja Au Nyingine


NOTE: Kufuata taratibu za kitaalamu katika UJENZI kunaweza kukusaidia kupunguza gharama za ujenzi mpaka 15% pamoja na kukuepushia hasara inayoweza kutokea mbeleni, sambamba na kukupatia kitu bora, kizuri na chenye thamani

1. Baada Ya Kuwa Umetayarisha Kiwanja Chako Kizuri Katika Eneo Ulilochagua, Anza Kujiridhisha Na Unachotaka Kujenga, kwa mfano

(i) Matumizi, jengo lako ni kwa ajili ya matumizi gani, makazi, biashara, ofisi, taasisi, starehe, godown/kiwanda n.k.

(ii) Jengo la aina gani, ghorofa au nyumba ya chini ya kawaida?

(iii) Unahitaji kuwe na vyumba vya matumizi gani(functional requirements) kama vile vyumba vingapi vya kulala pamoja na nini cha ziada kama vile movie theatre, maktaba n.k, kwa jengo la nyumba ya kuishi, au kama ni matumizi mengine ujue mahitaji yake

2. Tafuta mtaalamu wa majengo, msanifu au mbunifu majengo(architect), huyu ana utaalamu juu ya jengo, kazi zake na mipangilio yake yote ya kitaalamu. Atakushauri na kukuongezea uelewa wa sayansi ya majengo kwa ujumla

-Baada ya kumpeleka kuona eneo lako(site visit) mkajadiliana mkaelewana mwambie akafanye michoro ya mwanzo arudi mjadiliane na kujiridhisha kama kilichofanyika kimeendana na mahitaji yako, kisha mkishapitisha akafanye michoro ya 3D's(picha) za muonekano wa jengo husika uzione na ujiridhishe kama umeridhika na muonekano huo kisha ndio umruhusu amalizie michoro ya mwisho kwa ajili ya kufuatilia kibali cha ujenzi halmashauri husika
 
NB; Ni muhimu sana kujiridhisha na jengo lako usije kujuta baadaye au kujikuta unabomoa na kubadilisha baada ya kuona makosa, kwa sababu unakwenda kuweka pesa zako nyingi sana usije ukaingia gharama zaidi baadaye ambazo ungeweza kuziepuka mapema kwa kujiridhisha wakati wa michoro
Likifanyika vile unavyotaka utalifurahia na hutaona umepoteza

3. Kama jengo lako ni la ghorofa hutaishia hapo, unalazimika kumtafuta mtaalamu mwingine wa kutengeneza muundo wa mihimili ya jengo(structural engineer au mhandisi mihimili). Huyu hataongeza au kupunguza chochote ila atatumia michoro iliyofanywa na architect kutengeneza michoro ya muundo wa mihimili inayoshikilia jengo, kisha atakukabidhi michoro hiyo iliyopigwa mhuri kabisa kwa ajili ya kufuatilia kibali cha ujenzi halmashauri

4. Umeshakabidhiwa michoro yote ya msanifu/mbunifu majengo(architect) ambayo ni (architectural drawings) na ya mhandisi mihimili(structural engineer) ambayo ni (structural engineering drawings) yote ikiwa imepigwa mhuri utaenda nayo katika halmashauri yako kuomba kibali cha ujenzi ukiwa pamoja na hati yako ya kiwanja

5. Baada ya kupata kibali cha ujenzi halmashauri unaweza kuanza ujenzi lakini kama jengo lako ni la ghorofa utatakiwa kufuatilia vibali vingine kutoka kwenye bodi mbalimbali za ujenzi kutegemeana na ukubwa na matumizi ya jengo lako.

Bodi za ujenzi utakazopaswa kuchukua vibali kabla ya kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa ni hizi zifuatazo;-

(i) AQRB(Architects Quantity Surveyors Registration Board)
(Hii ni bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi)

(ii) ERB(Engineers Registration Board)
Hii ni bodi ya Wahandisi

(iii) CRB(Contractors Registration Board)
Hii ni bodi ya Wakandarasi

Utapatiwa vibali vya bodi hizi(kwa mfumo wa stikers) ambazo utaweka kwenye kibao chako cha ujenzi kwa ridhaa za kampuni zilizokupatia huduma za ushauri wa kitaalamu na michoro husika

6. Baada ya hapo unaweza kuanza ujenzi sasa. Kitu cha kuzingatia ni kwamba siku hizi kuna usumbufu mwingi na ni vigumu kujenga bila kuwa na kibali hasa kibali cha halmashauri na hasa katika eneo lililopimwa, ni rahisi kukutana na usumbufu mkubwa.

 Faida nyingine za kupata kibali cha ujenzi ni kwamba utaingiza katika kumbukumbu zako na utaingia pia katika kumbukumbu za halmashauri husika hivyo inaweza kukusaidia muda wowote utakaohitajika kuwasilisha taarifa hizo sehemu yoyote kuhusiana na jengo lako katika kuonyesha uhalali wa umiliki na uhalali wa jengo lenyewe ili kukusaidia katika mambo mbalimbali

7. Mwisho napenda nigusie kidogo swala la matumizi ya eneo maana ni swala ambalo limekuwa changamoto kwa wengi katika kupata kibali
Kiuhalisia maeneo mengi yamepimwa kwa matumizi ya makazi japo kuna watu pia wengi wanaonunua maeneo kwa ajili ya kujenga majengo ya biashara au makazi biashara(residential apartments) Utakapotengeneza michoro kwa ajili ya jengo la biashara au makazi biashara wakati eneo lako hati inaonyesha matumizi yake ni makazi pekee hutapewa kibali na wakati huo pengine umeshafanya michoro yote na kuwalipa watu pesa halafu halmashauri wanakukwamisha na kukutaka uanze mchakato wa kuomba kubadili matumizi.

 Huu ni mchakato mrefu na utakaoweza kukuchukua tena muda mwingi na gharama wakati huo pengine ulishachukua mkopo ambao unatakiwa uwe umeanza kuulipa japo bado hujapata hata hicho kibali. Endapo umejikuta kwenye jambo kama hili unaweza kumtafuta mtaalamu mkashauriana nini cha kufanya kwa haraka wakati mchakato wa kubadili matumizi unaendelea

Karibu kwa swali au ufafanuzi wowote maana mengi nimeeleza kwa kifupi ili nisikuchoshe msomaji

Ahsanteni
Arch. Sebastian Moshi
+255717452790

No comments: