Saturday, December 22, 2018

KAKUNDA AWATAKA WAFANYABIASHARA KUZINGATIA VIWANGO VYA KIMATAIFAWaziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akizungumza wakati akifungua semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali yaliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi za AN NAHL, TAMPRO, TAMSIA, UKUEM na Pamoja Foundation kwa udhamini wa Taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika katika viwanja vya city Garden jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa semina ya ajira wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda wakati wa ufunguzi wa semina hiyo na maonesho ya ujasiriamali yaliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi za AN NAHL, TAMPRO, TAMSIA, UKUEM na Pamoja Foundation kwa udhamini wa Taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika katika viwanja vya city Garden jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akipata maelezo kutoka Afisa Mradi taasisi ya Milele Zanzibar Eshe Haji Ramadhan katika maonesho ya ujasiriamali yanayoendelea Dar es Salaam katika viwanja vya city Garden Gerezani Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akimsikiliza Mjasiriamali wa taasisi ya SMV Health Centre Dk Hanifa Murithi Wakati wa semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali yaliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi za AN NAHL, TAMPRO, TAMSIA, UKUEM na Pamoja Foundation kwa udhamini wa Taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika viwanja vya city Garden jijini Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni mwenyekiti wa Taasisi ya AN NAHL Trust Injinia Ally Shaban Kilima.
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akinunua bidhaa ya unga wa muhogo kutoka mjasiriamali kijana Zaheer Mfaume wa kampuni ya RUM-Zahrain wakati wa maonesho ya ujasiriamali na semina ya ajira katika viwanja vya City Garden Gerezani Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Tanzania (FAT) Alhaji Muhidin Ndolanga akifuatilia hotuba na waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda wakati wa ufunguzi wa semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali yaliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi za AN NAHL, TAMPRO, TAMSIA, UKUEM na Pamoja Foundation kupitia programu ya GET HIRED kwa udhamini wa Taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika katika viwanja vya city Garden jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi zilizoshiriki kuandaa semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali kupitia program ya GET HIRED kwa udhamini wa taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika viwanja vya City Garden Gerezani Dar es Salaam.

………………………..
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa viwanda na Biashara Joseph Kakunda amewataka wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini kuzingatia ubora wa bidhaa kwa kuangalia viwango vya kimataifa na kitaifa wakati wa kusambaza bidhaa zao.

Waziri Kakunda alisema hayo leo tarehe 22 Disemba 2018 wakati akifungua semina ya ajira pamoja na maonesho ya ujasiriamali yaliyoandaliwa kwa pamoja na taasisi za AN NAHL, TAMPRO, TAMSIA, UKUEM na Pamoja Foundation kupitia program ya GET HIRED kwa udhamini wa Taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema, wafanyabiashara wa Tanzania ni lazima waelewe viwango vya kimatiaifa wakati wa kuzalisha bidhaa zao kwani mbali na kunufaika na ubora wa bidhaa lakini pia watakuwa wanaitangaza nchi na uzalishaji bidhaa wowote usio na ubora wanaopaswa kuwajibika ni wao.

Waziri wa Viwanda na Biashara alibainisha kuwa,kwa Tanzania kuna vyombo vinavyoangalia ubora wa bidhaa na kuvitaja kuwa ni shirika la viwango Tanzania ( TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kusisitiza kuwa ili wafanyaiashara wafanye kazi kwa ufanisi wanapaswa kuzingatia masharti ya vyombo hivyo.

Hata hivyo, Kakunda alisema jukumu la kutangaza bidhaa inayozalishwa ni la wafanyabiashara na hivyo kuwataka kuhakikisha bidhaa zinakuwa na Msimbohuria (Barcode) kwa lengo la kutambulisha sehemu bidhaa ilipotoka ama kuzalishwa.

Kwa mujibu wa Kakunda, kukosekana kwa Barcode katika bidhaa za Tanzania kumesababisha baadhi ya wafanyabiashara wa nchi jirani kutumia mwanya huo kuonesha kama bidhaa hizo zimetengenezwa katika nchi hizo jambo linalofanya Tanzania kushuka katika soko la kimataifa.

Alisema, Tanzania imekuwa ikishuka katika soko la AGOA kadri miaka inavyokwenda na kufikia chini ya asilimia nne kutokana na kushindwa kujitangaza kimataifa wakati inazalisha bidhaa zenye ubora.

Kakunda alibainisha kuwa, kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano kwa sasa ni kuwa na viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo kwa kuwa asilimia 70 ya watanzania wanajishughulisha na kilimo.

Kwa mujibu wa Kakunda, vipaumbele vingine ni viwanda vinavyoajiri wanachi wengi kama elfu moja pamoja na viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika majumbani kama vile mafuta ya kula, dawa za binadamu, chumvi sukari, unga maendeleo nguo.

Akielezea mafunzo ya ajira na maonesho ya ujasiriamali, Kakunda alisema kuwa vijana ni hazina ya kesho hivyo kuna kila jitihada za kuhakikisha nguvu kazi ya vijana haikumbani na kizuizi chochote kitakachowachelewesha kufikia malengo.

“Ni lazima tulinde kazi za vijana na wasiwekewe vigingi visivyo na maana na kama kuna figisu yoyote basi sisi kama serikali tuhakikishe inaondolewa” alisema Kakunda.

Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya AN NAHL Injinia Ally Shaban Kilima alieleza kuwa semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali inayofanyika yana lengo la kuwapatia ujuzi vijana waliomaliza vyuo kuwa na ari ya kujiajiri na suala hilo limechagizwa na juhudi za serikali ya awamu ya tano kuelekea uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda.

Alisema juhudi za taasisi zilizoandaa semina na maonesho ya ujasiriamali ni kutekeleza ibara ya nane hadi kumi ya ilani ya CCM kuhusiana na masuala ya ajira kwa vijana.

Mmoja wa vijana anayeshiriki maonesho hayo Zaheer Mfaume kutoka RUM-Zahrain Investment inayozalisha unga wa Muhogo alisema maonesho yanayofanyika yanasaidia kutangaza bidhaa wanayozalisha. Hata hivyo alielezea changamoto kubwa inayowakabili kuwa ni uhaba wa masoko na kuiomba serikali kusaidia kuwatafutia masoko.

No comments: