Sunday, December 23, 2018

MHE HASUNGA ASIMIKWA KUWA CHIEF NZUNDA, ASEMA HAKUNA MBADALA WA CCM

Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Katikati) amesimikwa Kiongozi wa Machief katika Wilaya ya Mbozi Chief Muleshwelwa Nzunda kuwa Chief Nzunda kutokana na majukumu makubwa anayoyafanya katika wizara yake sambamba na uwajibikaji uliotukuka katika Jimbo la Vwawa, Tarehe 22 Disemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal)
Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akicheza ngoma ya jadi, mara baada ya kuwasili Mkoani Songwe kwa ajili ya ziara ya kijimbo, Tarehe 22 Disemba 2018. 
Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akicheza ngoma ya jadi, mara baada ya kuwasili Mkoani Songwe kwa ajili ya ziara ya kijimbo, Tarehe 22 Disemba 2018. 
Baadhi ya Machief Wilayani Mbozi wakifatilia hotuba ya Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano uliofanyika leo tarehe 22 Disemba 2018 katika viwanja vya Stendi ya Maroli akiwa katika ziara ya siku tano ya kijimbo.
Baadhi ya wananchi Wilayani Mbozi wakifatilia hotuba ya Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga wakati akihutubia kwenye mkutano uliofanyika leo tarehe 22 Disemba 2018 wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Songwe.


Na Mathias Canal, Songwe

Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) amesimikwa kuwa Chief Nzunda kutokana na majukumu makubwa anayoyafanya katika wizara yake sambamba na uwajibikaji uliotukuka katika Jimbo la Vwawa.

Mhe Hasunga amesimikwa kuwa Chief na Kiongozi wa Machief katika Wilaya ya Mbozi Chief Muleshwelwa Nzunda wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano uliofanyika leo tarehe 22 Disemba 2018 katika viwanja vya Stendi ya Maroli akiwa katika ziara ya siku tano ya kijimbo.

Sambamba na kusimikwa kuwa Chief Nzunda vilevile amekabidhiwa silaha za jadi ikiwemo mkuki wa kujilinda na maadui kutoka kwa Chifu huyo wa Mbozi.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, Mhe Hasunga amewashukuru wananchi hao kwa kumchagua kuwa mbunge wa Jimbo hilo katika uchaguzi wa Octoba 25, 2015 jambo lililompelekea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kumteua kuhudumu katika Wizara muhimu nchini ya Kilimo.

Alisema ushindi wake katika kiti cha ubunge ulisababishwa na imani kubwa ya wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani pamoja na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi na serikali ya Awamu ya tano lakini CCM Pekee ndicho kitakachowaletea maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa hivyo wananchi wanapaswa kuendelea Kukiunga mkono.

"Huu ni muda wa kuungana na Rais katika kuhakikisha nchi inasonga Mbele kijamii na kiuchumi, Itikadi za kidini, Kisiasa na kikabila zinapaswa kuwekwa kando kwa maslahi mapana ya Taifa" Amesema Mhe Hasunga na kuongeza kuwa "Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Mhe Dkt John Pombe Magufuli anatuhimiza kufanya kazi kwa bidii na hivyo ili kupambana vizuri katika hali zetu kiuchumi ni wazi kuwa lazima tukubali kuweka siasa kando" 

Mhe Hasunga ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kwani ndiyo silaha pekee ya maendeleo huku akisisitiza kuwa serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao hivyo wakulima wanapaswa kuzalisha kwa bidii mazao mbalimbali ya kibiashara.

Aidha, ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya wakulima kuhusu bei za pembejeo za kilimo ili kuwa na unafuu wa gharama zitakazoendana na uwezo wa wananchi.

1 comment:

Quinton Storm said...

Hi nice readiing your blog