Thursday, February 1, 2018

KAMISHNA MKUU KICHERE AWATAKA WAFANYAKAZI SIRARI KUENDELEA NA UTOZAJI WA KODI STAHIKI

Na: Veronica Kazimoto-Sirari

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere amewataka Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali wakiwemo wa mamlaka hiyo wanaofanya kazi katika Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari kilichopo wilaya ya Tarime mkoani Mara kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha wanaendelea kutoza kodi stahiki.

Akizungumza wakati wa ziara yake kituoni hapo, Kamishna Mkuu Kichere alisema nchi inaendeshwa kwa kodi za ndani hivyo ni muhimu kila taasisi iliyopo eneo hilo kutimiza wajibu wake katika suala zima la ukusanyaji wa kodi.

“Wote mnajua umuhimu wa kodi na pia mnafahamu kuwa, kwa kupitia kodi hizi, Serikali inajenga miundombinu ya barabara, umeme, inasomesha wanafunzi, inajenga shule, inalipa mishahara ya wafanyakazi wake na mambo megine mengi. Hivyo, mfanye kazi kwa bidii na kwa weledi ili mkusanye kodi inayotakiwa kukusanywa kwa mujibu wa sheria bila kumuonea mtu yeyote.” alisema Kichere.

Kichere aliongeza kuwa, wafanyakazi wote kituoni hapo wana wajibu wa kukusanya kodi ili kuisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo kwa kutumia mapato yanayokusanywa nchini kupitia kodi mbalimbali.Aidha, Kamishna Mkuu huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano wanaoutoa kwa TRA.

“Nachukua fursa hii kukushukuru wewe Mhe. Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati yako ya Ulinzi na Usalama na pia napenda kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Glorious Luoga kwa ushirikiano mkubwa mnaoutoa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania,” amesema Kichere.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima alisema kwamba, mkoa wake umepanga utaratibu wa kufanya kikao kila mwezi ili kupitia taarifa ya ukusanyaji mapato mkoani humo.

“Kwa mkoa wa Mara kituo hiki cha Sirari ni muhimu sana na kina maslahi makubwa hususani katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, hivyo sisi kama mkoa tumejipanga kila mwezi kukaa pamoja kupitia taarifa ya TRA ili kupata viashiria vya maeneo muhimu ya ukusanyaji mapato ndani ya mkoa wetu,” alisema Malima.

Naye Kaimu Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mkoa wa Mara Laurent Kagwebe ameushukuru uongozi wa mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika suala zima la ukusanyaji mapato mkoani humo na kusema kuwa ushirikiano huo ukiendelea, kuna dalili njema za kuongezeka kwa makusanyo hapo baadae.

“Nikili wazi kuwa, nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya mkoani hapa na kama ushirikiano huu ukiendelea, nina imani kuwa, makusanyo yataongezeka kwa kiasi kikubwa,” amefafanua Kagwebe.

Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari kina jumla ya wafanyakazi 86 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyakazi hao wana jukumu la kulinda afya za wananchi kwa kukagua bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia kituo hicho, kulinda usalama wa raia pamoja na kukusanya mapato ya Serikali.

UONGOZI WA CCM MKOA WA PWANI WALAANI VIKALI VITENDO VYA WATU WANAOHUJUMU ZAO LA KOROSHO

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno akizungumza jambo na baadhi ya viongozi wa chama kikuu cha ushirika (CORECU) hawapo pichani baada ya kufanya ziara katika ofisi zao kupata taarifa ya baadhi ya watu wanaohujumu zao la korosho.
Mwenyekiti wa chama kikuu vha ushirikika Mkoa wa Pwani (COORECU) Rajab Ng’onoma akitoa ufafanuzi kwa viongozi wa CCM Mkoa wa Pwani kuhusiana na mwenendo mzima wa zao la korosho pamoja na changamoto amabzo zinawakabili katika utendaji wao wa kazi.
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya CORECU wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Pwani mara baada ya kumalizika kwa kutano wa kujadili masuala mbali mbali ya zoa la korosho.PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU




VICTOR MASANGU-PWANI

SAKATA la kuhujumu zao la korosho linalofanywa na baadhi ya wanunuzi,wakulima,pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika hatimaye limechukua sura mpya baada ya uongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kuamua kuliingilia kati suala hilo kwa lengo la kuweza kuwabaini wale wote ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine ili waweze kuchukulia hatua kali za kisheria.

Uamuzi huo wa CCM mkoa wa Pwani umekuja kufuatia kuwepo kwa taarifa ya kuibuka vikundi vya watu wachache ambao wana lengo la kukwamisha juhudi za serikali ya awamu ya tano kutokana na kuamua kufanya vitendo vya kuhujumu zao hilo kwa kuweka mawe,michanga, na takataka katika magunia ya korosho kitu ambacho ni kinyume kabisa na sheria na taratibu za nchi.

Akizungumza katika ziara ya kushitukiza katika ofisi za Chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU) kwa ajili ya kupata ufafanuzi juu ya jambo hilo Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa Ramadhani Maneno alisema kuwa suala hilo limemchukiza sana hivyo hawezi kulifumbia macho na atalivalia njuga kwa lengo la kuweza kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli ya kupambana na watu ambao ni wezi na mafisadi.

“Sisi kama chama cha CCM mkoa wa Pwani tumeamua kuja hapa kwa ajili ya kupata maelekezo juu ya suala hili la baadhi ya watu ambao wanahujumu zao la korosho kwa kweli na kwa kuwa tunatelekeza ilani ya chama kwa kweli hatuwezi kulivumilia tutahakikisha tunashirikiana na vyombo vya dola katika kulifanyia kazi suala hili la kuwapata wale ambao wanajihusisha,”alisema Maneno.

Naye mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) kutokea Mkoa wa Pwani Haji Jumaa alisema kuwa lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanatekeleza ilani ya chama ipasavyo ili kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi wote hususan kuweza kuwatetea wakulima waweze kupata haki zao za msingi wanazostahili bila ya kuzulumiwa na watu wachache.

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU) Rajab Ng’onoma amesema wamekuwa wanakabiliwa na changamoto ya kushuka kwa ubora wa korosho ambao umesababishwa na mambo mabali mbali yakiwemo ukosefu wa maghala ya kuhifadhia,ukosefu wa vifungashio,pamoja na baadhi ya vyama ya ushirika kupokea korosho mbichi hivyo kupelekea wanunuzi kugoma kununua na kujikuta wanadaiwa madeni makubwa.

HIVI karibuni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kujionea shughuli mbali mbali za mfumo unaotumika katika uuzaji wa zao la korosho aliweza kubaini kuwepo kwa baadhi ya magunia yaliyokuwa na korosho kuwekewa uchafu wa aina mbali mbali ukiwemo, mawe, mchanga, pamoja na matakataka mbali mbali.

WAKAZI ELFU 16 KONDOA VIJIJINI WAONDOKANA NA KERO YA MAJI

Mmoja wa akina mama wa kijiji cha Mauno, Kata ya Bumbuta, Jimbo la Kondoa Vijijini akiongea na vyombo vya habari kuhusu furaha yao baada ya kisima cha maji kuzinduliwa hatua iliyowaondolea kero ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, na Mbunge wa Jimbo la KOndoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wafadhili wa mradi wa kisima cha maji pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji na viongozi wa dini katika kijiji cha Mauno, wilayani Kondoa.
Wanakijiji wa Kijiji cha Mauno Wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakichota maji baada ya kuzinduliwa rasmi kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki kupitia Ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Wanakijiji wa Kijiji cha Mauno Wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakichota maji baada ya kuzinduliwa rasmi kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki kupitia Ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Wakazi wa kijiji cha Mauno wakiwa wamemwangusha ng’ombe kwa ajili ya kupata kitoweo ikiwa ni namna ya kujipongeza na kusherehekea baada ya kuzinduliwa kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango

Na Benny Mwaipaja, Kondoa

ZAIDI ya wakazi elfu 16 wa vijiji vitatu vya Mauno, Makiranya na Kinyasi-Majengo, katika Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma wameondokana na adha ya kukosa maji baada ya kuzinduliwa kwa visima viatu vya maji vilivyojengwa kwa msaada wa wahisani kutoka nchini Uturuki kupitia ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa visima hivyo katika Kijiji cha Mauno, Kata ya Bumbuta, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dokta Ashatu Kijaji, amesema kuwa kuzinduliwa kwa visima hivyo kunalifanya jimbo lake lifikishe visima 41 hatua ambayo amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika jimbo lake.

Dkt. Kijaji ameushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa kuratibu msaada huo wa zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 36, sawa na shilingi milioni 81, zilizotumika kuchimba visima hivyo pamoja na kuweka miundombinu mingine zikiwemo jenereta zinazotumika kusukuma maji hayo na kuwezesha upatikanaji wa maji hayo.

“Hivi sasa ujenzi wa visima 15 kati ya 25 vinavyojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji unaendelea huku wahisani wakiwa wametujengea visima 36 hivyo kufikisha idadi ya visima 61 katika kipindi cha miaka miwili tu tangu Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie madarakani hali ambayo haijawahi kutokea na lengo letu ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote 84 vinapatiwa huduma ya maji ifikapo mwaka 2020” Alisisitiza Dkt. Kijaji

Diwani wa Kata ya Bunbuta Bw. Bashiru Mtolo na mkazi mmoja wa kijiji hicho Bi. Khadija Hussein wamesema kuwa tatizo la maji katika kijiji cha Mauno lilikuwa kubwa na kuwalazimisha wanawake na watoto kwenda umbali mrefu kusaka maji kwa ajili ya matumizi yao ya majumbani pamoja na kunywesha mifugo.

“Tunaushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa msaada wao huu mkubwa na Mbunge wetu kwa ufuatiliaji wake wa karibu uliowezesha kupatikana kwa visima hivi na vingine ambavyo vimesaidia kwa kiwango kikubwa kutatua kero ya maji na tunaamini mpaka kufikia mwaka 2020, matatizo ya maji katika wilaya yetu ya Kondoa litakuwa historia” alisema Diwani Mtolo.

Naye Mwakilishi na Mwambata wa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini Sheikh Muhammad Cicek ameeleza kuwa msaada wa Dola elfu 36 zilizotumika kujenga miradi hiyo mitatu ya visima vya maji umetolewa na wahisani mbalimbali wa Uturuki ikiwa ni kuenzi uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na Tanzania.

Alisema kukamilika kwa miradi hiyo ya maji kutasadia kuwawezesha akina mama na wananchi wa Kondoa kwa ujumla kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji ambayo hata hivyo hayakuwa safi wala salama.

EXIM IMEKABIDHI VITANDA NA MAGODORO 40 KWA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA MBEYA, WODI YA WAZAZI META.

Mkurugenzi Mtendaji was hospital ya rufaa ya Mbeya Dr Godlove Mbwanji akitoa shurkani kwa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Stanley Kafu (kushoto) baada ya kukabidhiwa msaada wa vitanda na magodoro 40 kutoka benki hiyo jana asubuhi kwa ajili ya wagonjwa katika hospitali hiyo kitengo cha wazazi-Mbeya jijini Mbeya.  Wa pili kulia ni Mkuu wa idara ya wodi ya wazazi-Meta, katika hospitali hiyo Dr John France.

HOSPITALI na kliniki nyingi nchini zina tatizo la ukosefu wa dawa, vifaa na vitanda hasa katika hospitali za rufaa.  Katika kukabiliana na uhaba huu unaosumbua taifa , Exim Bank Tanzania, yenye uwepo wa kimataifa  imeanzisha mradi unaolenga kusaidia upungufu wa vitanda katika hospitali nchini - hivyo benki ya Exim itatoa magodoro and vitanda 500 katika hospitali za serikali katika mikoa 13 nchini kama sehemu ya kampeni yake yenye lengo la kusherehekea miaka 20 ya kutumikia jamii.

Benki ya Exim Tanzania iliadhimisha miaka 20 ya huduma, mwezi wa Agosti mwaka jana, kwa kuzindua mradi wa mwaka mzima unaoitwa “miaka 20 ya kujali jamii” ambao Benki hiyo itawekeza katika sekta ya afya Tanzania. Kama benki ya kiTanzania iliyoanzishwa mwaka wa 1997, Benki ya Exim inafafanua mafanikio kwa jinsi inavyoleta mabadiliko kwa wateja na jamii kwa ujumla.

Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mbeya, ni hospitali ya sita kupokea mchango huu, baada ya Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Arusha mwezi uliopita, Hospital ya rufaa Dodoma mwezi Novemba, hospitali ya rufaa Ligula, Mtwara mwezi Oktoba, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja, Zanzibar mwezi Septemba na Hospitali ya rufaa Temeke, Dar es Salaam mwezi wa nane mwaka jana. Tukio lilifanyika kwenye hospitali hiyo wodi ya wazazi META na mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo Dr. Godlove Mbwanji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa idara ya masoko wa benki ya Exim, Bwana Stanley Kafu alisema, “ Benki ya Exim imekuwa ikisheherekea miaka 20 ya uanzilishi toka Agosti mwaka jana 2017. Kama ishara ya kushukuru  watumishi wake na jamii kwa ujumla, benki imeanzisha mpango wa kutoa vitanda na magodoro kwa hospitali nchini kote kila mwezi. Benki itaendelea mpango huu kwa mwaka mmoja hadi Julai 2018. "

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya rufaa ya Mbeya, Dr Godlove Mbwanji alipongeza Exim Bank Tanzania kwa ahadi yake ya kukabiliana na upungufu wa vitanda kwenye ma hospitali ambao unakabiliwa na taifa na kuleta juhudi zake kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mbeya. Alisema “Upungufu wa vitanda katika mahospitali ni changamoto kubwa. Msaada huu kutoka benki ya Exim wa hivi vitanda 40 na magodoro utasaidia sana katika kupunguza changamoto hii san a sana kwenye wodi ya wazazi.”

Ikiwa kama sehemu ya mradi wa “miaka 20 ya kujali jamii” benki ya Exim itatoa msaada wa vitanda 500 na magodoro yake kwa hospitali katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Dodoma, Kigoma, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Shinyanga, Mtwara, Pemba na Unguja ambapo mpaka sasa Dar es Salaam, Unguja, Mtwara, Arusha, na Dodoma tayari wameshapokea misaada.

Katika kipindi cha miaka 20 ya kuwepo sokoni benki ya Exim imejenga taasisi imara kijiografia, katika bidhaa za kivumbuzi, mahusiano mazuri na wateja na uwezo wake wa kutoa huduma kwa haraka zaidi.

MAGAZETI YA LEO ALHAMIS FEBRUARY MOSI, 2018































MFANYABIASHARA WA NGUAO KARIAKOO AJISHINDIA MILIONI 60 ZA TATUMZUKA


Mwakilishi wa TatuMzuka,Kemi Mutahaba akimkabidhi mfano wa hundi Bi Neema  Mtewele (38),ambaye ni mfanyabiashara wa nguo za akina mama Kariakoo jijini Dar Es Salaam,aliyeibuka na kitita cha shilingi milioni 60 za TatuMzuka mwishoni mwa wiki.
Neema  Mtewele (38),ambaye ni mfanyabiashara wa nguo za akina mama Kariakoo jijini Dar Es Salaam,akifafanua mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani),namna alivyofanikiwa kushinda mamilioni hayo ya Mchezo wa kubahatisha wa Tatumzuka.Neema alisema kuwa amekuwa akiucheza muda mrefu mchezo huo bila mafanikio,lakini hakukata tamaa,alindelea kucheza na hatimae akabahatika kuibuka mshindi wa milioni 60.

"Hizi fedha kwakweli matumizi yake makubwa yatakuwa ni kuendeleza na kuunyanyua zaidi mtaji wangu niliokuwa nao kwenye biashara yangu,bado nahitaji kuikuza zaidi biashara yangu",alisema Neema huku akionesha furaha ya wazi kwa kushinda kitita hicho cha milioni 60.

Msanii Wastara awatoa hofu watanzania kuhusu matibabu yake


Na: Genofeva Matemu – WHUSM 

Msanii wa filamu nchini Bibi. Wastara Issa ameendelea kumshukuru Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kuonyesha moyo wa kuguswa na tatizo linalomsumbua na kuweza kumpatia kiwango cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya matibabu ya mguu pamoja na mgongo. 

Bibi. Wastara ametoa shukrani hizo jana  Jijini Dar es Salaam alipokua akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa awali ilikua aondoke nchini tarehe 28 mwezi januari mwaka huu kwenda mjini Mumbai kwa ajili ya matibabu lakini kutokana na baadhi ya mipango kutokaa vizuri safari hiyo ilisogezwa hadi jumapili tarehe 4 Februari 2018 ambapo anatarajia kuondoka mida ya jioni na kufika Mumbai mapema alfajiri siku ya jumatatu ambapo ataanza matibabu siku hiyo hiyo. 

Bibi. Wastara amesema kuwa katika safari hiyo ataongozana na nesi mmoja kutoka hospitali ya TMJ pamoja na mtu mmoja kutoka katika familia yake ambapo matibabu yake yatafanyika katika hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai na kutarajia matibabu hayo kuchukua takribani wiki tatu na zaidi. 

Aidha msanii Wastara Issa ameishukuru wizara inayosimamia tansia ya filamu kwa kumfariji katika kipindi hiki kigumu anachopitia huku akimshukuru Waziri mwenye dhamana na tasnia ya filamu nchini, Bodi ya Filamu Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa pamoja na watanzania wote kwa kuonyesha upendo wa dhati kwake. 

“Asanteni sana watanzania mmeonyesha moyo wa dhati kwangu kwa muda mrefu sasa, mmekua pamoja nami tangu kipindi cha matibabu ya Saduki hadi sasa, uzito wa neno asante kutoka kwangu leo hauwezi kulipa fadhila kwa dua na michango yenu kwangu, mwenyezi mungu aendelee kuifanya nchi yetu kuwa na amani na upendo” amesema msanii Wastara Issa 

Naye Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa serikali kupitia bodi ya filamu inashukuru kwa kupata taarifa kamili ya safari ya msanii Wastari Issa ilipofikia kwani bodi ya filamu inapenda kumuona Wastara akiwa katika afya nzuri na kurudi katika hali yake ili aweze kuungana na wanatasnia wenzake kuendeleza tasnia ya filamu nchini. 

Bibi. Fissoo amesema kuwa Watanzania wengi wamekua wakiwasiliana na Wastara kwa njia mbalimbali, kumchangia na hata kufika kumuona, hivyo serikali inatambua kuwa msanii Wastara Issa yupo katika maandalizi ya safari ambapo awali alikua asafiri tarehe 28 mwezi januari mwaka 2018 lakini kutokana na taratibu za safari kutokukamili kumepelekea safari hiyo kusogezwa hadi tarehe 4 februari mwaka huu. 



Msanii wa Filamu nchini Bibi. Wastara Issa (wapili kulia waliokaa chini) akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake kuhusu maandalizi ya safari yake ya matibabu kuelekea Mjini Mumbai walipofanya naye mazungumza jana Jijini Dar es Salaam. Watatu kulia waliokaa ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo

Mkutano wa Waziri Mahiga na mwenyeji wake Waziri Kyung-hwa wa Jamhuri ya Korea Kusini

 Mheshimiwa Augustine Phillip Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akilakiwa na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, mara baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mazungumzo ya kikazi tarehe 31 Januari 2018. 
 Mheshimiwa Augustine Phillip Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akilakiwa na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, mara baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mazungumzo ya kikazi tarehe 31 Januari 2018. 

 Mheshimiwa Augustine Mahiga na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa wakiwa kwenye mazungumzo ya kikazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea tarehe 31 Januari 2018. Wakwanza kushoto ni Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Korea. Wakwanza kulia ni Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea.

 Mheshimiwa Augustine Mahiga na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa wakiwa kwenye mazungumzo ya kikazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea tarehe 31 Januari 2018
 Mheshimiwa Augustine Mahiga na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa wakiwa kwenye mazungumzo ya kikazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea tarehe 31 Januari 2018. Wakwanza kushoto ni Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Korea. Wakwanza kulia ni Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea.
 Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania akimkabidhi zawadi ya picha ya mlima Kilimanjaro na kinyago cha mnyama waziri mwenzake wa Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Kang Kyung-hwa baada ya kukamilisha mazungumzo ya kikazi yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi baina ya nchi hizo mbili.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukamilisha mazungumzo ya kikazi. Wakwanza kulia ni Mheshimiwa Balozi Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bi. Bertha Makilagi, afisa dawati wa Korea Kusini, Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo  ya Nje ya Korea Kusini na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.