Mmoja wa akina mama wa kijiji cha Mauno, Kata ya Bumbuta, Jimbo la Kondoa Vijijini akiongea na vyombo vya habari kuhusu furaha yao baada ya kisima cha maji kuzinduliwa hatua iliyowaondolea kero ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, na Mbunge wa Jimbo la KOndoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wafadhili wa mradi wa kisima cha maji pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji na viongozi wa dini katika kijiji cha Mauno, wilayani Kondoa.
Wanakijiji wa Kijiji cha Mauno Wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakichota maji baada ya kuzinduliwa rasmi kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki kupitia Ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Wanakijiji wa Kijiji cha Mauno Wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakichota maji baada ya kuzinduliwa rasmi kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki kupitia Ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Wakazi wa kijiji cha Mauno wakiwa wamemwangusha ng’ombe kwa ajili ya kupata kitoweo ikiwa ni namna ya kujipongeza na kusherehekea baada ya kuzinduliwa kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango
Na Benny Mwaipaja, Kondoa
ZAIDI ya wakazi elfu 16 wa vijiji vitatu vya Mauno, Makiranya na Kinyasi-Majengo, katika Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma wameondokana na adha ya kukosa maji baada ya kuzinduliwa kwa visima viatu vya maji vilivyojengwa kwa msaada wa wahisani kutoka nchini Uturuki kupitia ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa visima hivyo katika Kijiji cha Mauno, Kata ya Bumbuta, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dokta Ashatu Kijaji, amesema kuwa kuzinduliwa kwa visima hivyo kunalifanya jimbo lake lifikishe visima 41 hatua ambayo amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika jimbo lake.
Dkt. Kijaji ameushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa kuratibu msaada huo wa zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 36, sawa na shilingi milioni 81, zilizotumika kuchimba visima hivyo pamoja na kuweka miundombinu mingine zikiwemo jenereta zinazotumika kusukuma maji hayo na kuwezesha upatikanaji wa maji hayo.
“Hivi sasa ujenzi wa visima 15 kati ya 25 vinavyojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji unaendelea huku wahisani wakiwa wametujengea visima 36 hivyo kufikisha idadi ya visima 61 katika kipindi cha miaka miwili tu tangu Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie madarakani hali ambayo haijawahi kutokea na lengo letu ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote 84 vinapatiwa huduma ya maji ifikapo mwaka 2020” Alisisitiza Dkt. Kijaji
Diwani wa Kata ya Bunbuta Bw. Bashiru Mtolo na mkazi mmoja wa kijiji hicho Bi. Khadija Hussein wamesema kuwa tatizo la maji katika kijiji cha Mauno lilikuwa kubwa na kuwalazimisha wanawake na watoto kwenda umbali mrefu kusaka maji kwa ajili ya matumizi yao ya majumbani pamoja na kunywesha mifugo.
“Tunaushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa msaada wao huu mkubwa na Mbunge wetu kwa ufuatiliaji wake wa karibu uliowezesha kupatikana kwa visima hivi na vingine ambavyo vimesaidia kwa kiwango kikubwa kutatua kero ya maji na tunaamini mpaka kufikia mwaka 2020, matatizo ya maji katika wilaya yetu ya Kondoa litakuwa historia” alisema Diwani Mtolo.
Naye Mwakilishi na Mwambata wa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini Sheikh Muhammad Cicek ameeleza kuwa msaada wa Dola elfu 36 zilizotumika kujenga miradi hiyo mitatu ya visima vya maji umetolewa na wahisani mbalimbali wa Uturuki ikiwa ni kuenzi uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na Tanzania.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo ya maji kutasadia kuwawezesha akina mama na wananchi wa Kondoa kwa ujumla kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji ambayo hata hivyo hayakuwa safi wala salama.
No comments:
Post a Comment