
Fatma Salum- MAELEZO
Muswada
wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ambao unatazamiwa
kuwasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni katika kikao kilichoanza Novemba
1 mwaka huu umezua mjadala mkubwa na mpana miongoni mwa wadau wa sekta
ya habari.
Mjadala wa muswada huu umekuwa ni mkubwa
ukilinganisha na miswada mingine kwa sababu ukweli ni kwamba kila
mtanzania ni mdau wa sekta hii ambayo wote tunaitegemea kwa kupata
taarifa zinazoaminika ili kutusaidia kufanya maamuzi mbalimbali katika
maisha yetu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Usahihi wa maamuzi
yote makubwa tunayoyafanya mmoja mmoja au kwa pamoja kama jamii – iwe
kuchagua vongozi, kuchagua kozi ya kusoma na mengineyo yanategemea sana
taarifa tulizonazo.
Ili tuweze kupata taarifa sahihi ni muhimu
vyombo vya habari na waandishi watengenezewe mazingira mazuri ya
kufanyia kazi, jambo ambalo ndiyo malengo ya sheria hii tarajiwa.
Licha
ya ukosoaji mkubwa unaofanyika, ukweli ni kwamba Muswada wa Vyombo vya
Habari 2016, kama utapitishwa, utajenga mazingira mazuri ya tasnia hii
na kuirudishia heshima inayostahili.
Katika kupitia muswada huu nimeona faida nyingi za muswada, lakini kwenye makala hii nitataja faida tano kubwa.
Heshima ya tasnia
Kwanza,
muswada huu unairejeshea tasnia hii heshima yake iliyoipoteza siku
nyingi kwa kuifanya fani hii iwe miongoni mwa fani za uweledi, kama
zilivyo nyingine zikiwemo udaktari na uanasheria.
Heshima ya
tasnia hii inastahili kuwa juu na ndiyo maana vyombo vya habari vimeitwa
mhimili wa nne, ukifanya kazi sambamba na mihimili mingine yaani
Serikali, Bunge na Mahakama.
Tasnia hii ilianza kupoteza heshima
kuanzia miaka ya 1990 kufuatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na
baadae kisiasa (vyama vingi 1992) yaliyochochea kuibuka kwa vyombo
vingi vya binafsi, hususan magazeti.
Tangu enzi hizo,
changamoto kubwa ya fani hii imekuwa ni ukosefu wa udhibiti kiasi kwamba
kila anayejisikia, bila kujali kasoma au la, anaingia. Matokeo yake
waandishi wasiosoma (makanjanja) wamekuwa wakifanya madudu na lawama
zimeelekezwa kwa wanahabari wote. Akioza samaki mmoja ndiyo wote.
Kwa
sasa waandishi wanatazamwa kwa kejeli, wanatukanwa, wanabezwa na yote
haya ni kwa sababu ya kundi la waandishi wasio na maadili na ambao
hawana ukomo wala miiko katika kutafuta habari na wanachokiandika ni
tofauti na walivyopokea kutoka katika chanzo chao cha habari.
Mara
nyingi tunasikia mwandishi anavamia stara za watu katika majumba yao au
katika maeneo yao ya starehe kwa jina la kutafuta habari. Kwa hali
hii, ni vigumu kulaumu vyanzo (source) wanapokataa kuzungumza na vyombo
vya habari. Yote haya ni kwa sababu ya waandishi waliokosa taaluma na
weledi (makanjanja).
Uholela wa kuingia katika fani hii
ulitokana na sababu mbili kubwa, kwanza kisingizio cha kipengele cha
katiba kinachomhakikishia kila mtu haki ya kukusanya na kusambaza habari
(Ibara ya 18.1) kwani baadhi ya watu wametafsiri kipengele hiki kuwa
kila mtu anaweza kuwa mwandishi wa habari!
Sababu ya pili ni
maendeleo makubwa ya teknolojia ambapo kila aliyeweza kujitengenezea
blogu yake alifanya hivyo na kuanza kutafuta na kuchapisha habari.
Lakini
ukweli ni kwamba tasnia hii si ya mchezo mchezo na kufanyia majaribio.
Zipo nchi zilizosambaratika au kuingia katika vurugu kutokana na vyombo
vya habari ambavyo havikuwajibika, vikashindwa kutanguliza uzalendo,
weledi na kuzingatia maadili.
Muswada huu katika sehemu ya tatu,
Ibara ya 10, unaondoa shida hiyo kwa kuweka Bodi ya Ithibati ya
Wanahabari itakayowajibika kutoa vitambulisho (press card) kwa
wanahabari kwa kuzingatia sifa na viwango vya elimu vinavyotakiwa. Bodi
pia itasimamia kanuni za maadili ya wanahabari zilizoidhinishwa na
kutunza orodha ya waandishi waliothibitishwa.
Ibara ya 18.1–2
inapiga marufuku wasio na vitambulisho (press card) kufanya kazi ya
uandishi wa habari na ibara ya 47.2 inaweka adhabu ya faini isiyopungua
Milioni 5 au kifungo cha hadi miaka mitano kwa wanaovamia tasnia ya
habari na kutumia huduma ya habari kueneza habari za uongo kwa lengo la
kuhatarisha ulinzi, amani na usalama wa nchi. Bila ya shaka sheria hii
ikitekelezwa, heshima ya tasnia ya habari itarejea.
Msisitizo wa elimu
Ukiangalia
hali halisi ya uandishi wa sasa, utagundua kuwa kiini cha tatizo ni
watu kupita njia za mkato kuingia katika fani hii, yaani kutokuwa tayari
kwenda shule kusoma.
Lakini hata wale waliosoma bado wanahitaji
kuendelea kupigwa msasa juu ya namna bora ya kufanya kazi zao maana
tasnia ya habari inabadilika kila uchao hususan upande wa teknolojia.
Miaka
20 iliyopita hatukuwa na blogu wala hakukuwa na Twitter, Facebook,
Instagram na Whatsapp kama ilivyo sasa, lakini hizi ni silaha za
mwandishi na anaweza kuzitumia kuboresha kazi zake.
Ukiangalia
muswada huu utaona kuwa umeweka msisitizo mkubwa katika elimu ya
waandishi wa habari kiasi kwamba bodi itakayoundwa ina jukumu la
kuishauri serikali kuhusiana na mafunzo ya waandishi, kushauriana na
taasisi za elimu ya mambo ya habari juu ya viwango vya elimu
vinavyotakiwa kwa waandishi na muhimu zaidi bodi hii ina jukumu la
kuandaa mafunzo ya waandishi wa habari.
Katika Ibara ya 21,
muswada huu unazungumzia mfuko wa mafunzo ya habari wenye malengo matatu
ikiwemo kuwezesha mafunzo kwa wanataaluma ya habari, kukuza program za
uendelezaji wa maudhui ya ndani ya nchi na pia kuchochea na kuchangia
utafiti na maendeleo katika nyanja za habari na mawasiliano ya umma.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 22, mfuko huo utapata fedha kutoka bungeni, misaada
na zawadi na michango ya vyombo vya habari. Kwa hiyo ukisoma vifungu
hivi unaona kuna faida nyingi ambazo iwapo muswada huu utapita na
kutekelezwa ipasavyo, utasaidia kuhuisha tasnia ya habari.
Umuhimu wa Baraza Huru la Habari
Pia
muswada huu umeainisha kuwa kutakuwa na Baraza Huru la Habari ambalo
kazi na mamlaka yake yatatambulika kisheria. Kila mwanahabari
aliyethibitishwa atakuwa mwanachama wa baraza hili.
Ibara
ya 25 (1) inaeleza kazi za baraza hili kwa kushirikiana na Bodi ya
Ithibati zitakuwa ni kuandaa na kuidhinisha kanuni za maadili ya taaluma
ya habari pamoja na kukuza maadili na viwango vya taaluma baina ya
wanahabari na kampuni za habari.
Uwepo
wa baraza hili utapelekea tasnia ya habari kuwa taaluma rasmi
inayotambulika kisheria kama taaluma nyingine, tofauti na baraza
lililopo sasa ambalo halitambuliki kisheria hivyo mamlaka yake hayana
nguvu.
Kulinda Maslahi ya Waandishi wa Habari
Sababu nyingine
ya kuunga mkono muswada huu ni maslahi ya moja kwa moja kwa wanahabari.
Sheria hii itasaidia sana kulinda maslahi ya waandishi wa habari pale
wanapopata majanga wakiwa kazini, maradhi, kustaafu au kuachishwa kazi.
Kila
mwajiri atatakiwa kuweka bima na hifadhi ya jamii kwa kila mtu
aliyeajiriwa katika chombo cha habari husika na wanahabari wa
kujitegemea watapaswa kujiwekea kinga kwa mujibu wa sheria hii.
Jambo hili ni la kupongeza sana kwani sheria hii itasaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwenye tasnia ya habari.
Wengi
wetu ni mashahidi kwamba kuna baadhi ya waandishi wa habari wamewahi
kupata matatizo wakiwa kazini lakini wameishia kusubiri kuchangiwa na
wasamaria wema ili wapate matibabu kwa vile hakuna kinga ya kuwabana
waajiri au vyombo vya habari viweze kuwasaidia.
Mwelekeo kwa Vyombo vya Habari.
Sababu
ya tano ya kuafiki muswada huu ni kwamba, pamoja na mambo yote sheria
hii inatoa mwelekeo wa vyombo vya habari kuhusu jinsi ya kufanya kazi
kwa ufanisi, kuzingatia maadili na weledi. Katika hili, sheria imeeleza
majukumu ya vyombo vya habari vya umma na binafsi ili kuhakikisha
majukumu hayo yanaleta tija kwa taifa.
Kwa kuzingatia hayo
muswada huu una manufaa makubwa sio tu kwa wanahabari bali watu wote
watanufaika kwa kupata taarifa sahihi zenye maudhui ya kuelimisha,
kukosoa, kuonya na kuboresha bila ya kuudhi, kukiuka haki za wengine au
kuharibu amani na usalama wa taifa letu.