Tuesday, April 2, 2013

PINDA AWAFARIJI WAFIWA WA NDUGU WALIOFUKIWA NA KIFUSI ARUSHA, ATEMBELEA MACHIMBO YA MORAMU YA MOSHONO

 Mh Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitia saini kitabu cha maombolezo alipofika  mkoani Arusha leo Kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao wamefariki katika machimbo ya  Moramu katika eneo la Moshono Mkoani Arusha. Maporomoko hayo yametokea jana na kusababisha vifo vya watu13  na majeruhi wawili ambao mmoja ameruhusiwa na mwingine amelazwa katika Hospitali ya Mount Meru 
 Waziri Mkuu akiwa na wabunge wa Arusha na Meya pamoja na mkuu wa mkoa kwenye msiba huo mzito. Toka Kushoto ni Mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Magessa Mulongo, Meya wa jiji la Arusha Mstahiki Gaudence Lyimo, Mbunge wa Arumeru Mashariki Mhe Joshua Nassari na Mbunge wa kuteuliwa Catherine Magige
 Sehemu ya majeneza ya marehemu katika ibada hiyo maalumu leo
 Kiongozi wa kidini akiombea marehemu
 Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda akitoa pole kwa wafiwa





 Sehemu ya machimbo ya  Moramu iliyopotomoka na kuua watu katika eneo la Moshono Mkoani Arusha
 Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda akiwa na wabunge wote wa mkoa wa Arusha na viongozi wengine akitembelea machimbo ya  Moramu katika eneo la Moshono Mkoani Arusha
 Waziri Mkuu akitembelea sehemu ya tukio
 ukaguzi ukiendelea
Waziri Mkuu akitoa maelekezo baada ya kutembelea machimbo ya  Moramu katika eneo la Moshono Mkoani Arusha. Picha zote na Chris Mfinanga

Monday, April 1, 2013

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2013


HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2013

Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi.  Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;                                       
       Jambo la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013.  Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania.  Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake.  Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake. 
Kwa niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia, nimemshukuru sana Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu.  Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika.  Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake.  Na, kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi wake. 
Tumefarijika sana kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi wapya wa China.  Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika.  Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali.  Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri Mkuu wake Chou En Lai. 
Rais wa China aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya maendeleo.  Katika miaka 49 ya uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;      
Kuna miradi kadhaa mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya China.  Wakati wa ziara yake, Rais Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku ile. 
Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa
Jijini Dar es Salaam

Ndugu Wananchi;
       Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la Dar es Salaam.  Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi kubwa nchini.  Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana.  Watu 17 waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.  Wengine walitibiwa na kuruhusiwa.  Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia ukingoni. 
Ndugu Wananchi;
       Mimi na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali.  Hali niliyoiona pale imenihuzunisha sana.  Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi.  Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti.  Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji. 
       Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa.  Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii.  Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.  Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi. 
Ndugu Wananchi;
       Maneno mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile.  Alimradi kila mtu ana dhana yake.  Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo  wachukuliwe hatua zipasazo.  Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi.  Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake.  Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika.  Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao.  Watimize wajibu wao.  Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote. 
      
Ndugu Wananchi;
       Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane.   Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe.  Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa  Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
       Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini.  Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa.  Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya.  Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka.  Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo.  Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu.  Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake.  Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
 Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua.  Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua.  Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake.  Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu. 
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo.  Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa na shule za Makanisa.  Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife.  Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
       Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote.  Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali.  Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali.  Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo.  Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi.  Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo.  Pale ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi.  Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi.   Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa dini na nyumba za ibada.  Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini.  Lakini hivyo sivyo.  Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.
Kila tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea.  Hakuna ushahidi wa matukio hayo kuunganika.  Mpaka sasa hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa nchini. 
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu.  Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha.  Si tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo nchini.  Ni la pale pale Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu zao. 
Hivi kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao.  Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake.  Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili.  Busara ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali.  Hata mzozo wa kuchinja wanaweza kuumaliza.  Mbona bucha za kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa.  Hatuwatendei haki Watanzania.    
Ndugu Wananchi;
       Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la Buseresere, Geita.  Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje.  Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi.  Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla yake.  Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga.  Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo.  Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana.  Je, Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu?  Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo. 
 Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu nzuri.  Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika.  Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje.  Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.    Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya hivyo.  Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
       Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum.  Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu.  Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu.  Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi.  Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao.  Jeshi la Polisi lilikataa.  Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa. 
Ndugu Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa Bara.  Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote.  Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi.  Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli.  Hata dalili hazijakuwepo. 
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu.  Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru.  Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao.   Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida yao.  Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu wagombane.  Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake.  Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?  
Ndugu Wananchi;
       Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani.  Kwa upande wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu.  Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar, watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea.  Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi.  Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi.  Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa.  Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa. 
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua.  Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini.  Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa.  Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini.  Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita.  Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
       Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu.  Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote walipo wako salama.  Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku zote.  Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha.  Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
       Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu sote.  Tuazimie sote kuwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.  Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na  vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo.  Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena.  Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu.  Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga hili.  
Ndugu Wananchi;
       Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi.  Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya.  Ni masuala yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao.  Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi baya ni viongozi wa dini. 
Ndugu Wananchi;
 Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo hilo.  Nimepata faraja kuona kuwa wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza.  Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na Watanzania.  Kuna upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha tuliyoyazoea.  Maisha ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao.  Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma wawakilishi.  Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi; 
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini.  Waache kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu.  Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au kuzitangaza.  Wawe makini na maneno wanayotumia.  Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote.  Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani.  Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
       Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano wetu.  Tuishi kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au mahali atokako mtu.  Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao.  Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama inavyofanya siku zote.  Kama kuna mtu anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi.  Hatua zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka.  Tusherehekee kwa amani na utulivu.  Tusherehekee pamoja.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

TASWA FC, TASWA QUEENS ZANG'ARA BONANZA LA PASAKA DAR

 Pamoja na Mvua zilizonyesha jijini Dar es Salaam, jana na uwanja wa Netoboli na wa Mpira wa miguu TCC kujaa maji lakini bado timu za TASWA FC na Netiboli ya TASWA Queens, ziliibuka na ushindi mnono katika Bonanza la Pasaka dhidi ya timu ya Kiliflora ya Arusha. Hapa wachezaji na viongozi wa timu hizo wakijitahidi kuondoa maji katika uwanja wa Netiboli kabla ya kuanza kwa mtanange huo, ambao ulimalizika kwa TASWA Queens kuibuka na ushindi wa mabao 28 -8. Picha zote na Nasma Mafoto
 Majuto Omari wa Taswa Fc (kushoto) akichuana kuwania mpira na mchezaji wa Kiliflora ya Arusha, ambapo hadi mwisho Taswa Fc Iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
 Iman wa Taswa Queens, akitupia moja kati ya magoli 28 waliyofunga.
 Mtanange unaendelea.....
Beki wa TASWA Fc Muhidin Sufiani (kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa Kiliflora ya Arusha.
 Mchezo ukiendelea japo uwanja ulikuwa ukisumbua kwa utelezi....
 Mafoto, akiondosha hatari.....
 Utelezi ukiwasumbua wachezaji wa Netiboli, hapa mmoja akienda chini
 Salum Jaba wa Taswa, akiondosha hatari....
 Mtanange ukiendelea.....
 Wachezaji wa Taswa Queens, wakiwa katika picha ya pamoja.....
 Shafii Dauda (kulia) akiwania mpira na wachezaji wa Kiliflora ya Arusha
 Kiliflora ya Arusha.
 Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto akiwa katika picha ya pamoja na Taswa Queens.
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto akiwa katika picha ya pamoja na  Kiliflora ya Arusha.
 Kinadada wakiendelea kuchuana.
 Kipute kikiendelea..
Wakiendelea kuchuana katika uwanja wa TCC Chang'ombe. Picha Zote na Nasma Mafoto wa www.sufianimafoto.com

PROFESA JAY NA FID Q WAFUNIKA KATIKA TAMASHA LA VODACOM COCO BEACH


Msanii mahiri wa mziki wa kizazi kipya,Profesa Jay akiwapagawisha mashabiki waliofurika katika Tamasha la wazi la Vodacom, lililofanyika katika Ufukwe wa bahari ya hindi Coco Beach, jijini Dar  es Salaam,lilohudhuriwa na mashabiki lukuki,waliokwenda kujionea burudani hizo ambapo pia walitumia fursa hiyo kwa kuelimishwa juu ya huduma mbalimbali zinazotelewa na mtandao wa Vodacom.
Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Fid Q,akiandaa muziki katika kompyuta yake ndogo (lap top) wakatiwa Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika katika Ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam,lilohudhuriwa na mashabiki lukuki, waliokwenda kujionea burudani ambapo pia walitumia fursa hiyo kwakuelimishwa juu ya huduma mbalimbali zinazotelewa na mtandao wa Vodacom,wanaoshuhudia kutoka kulia ni Msanii machachari Dar Stamina  na Afisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania,Ibrahim Kaude.
Umati wa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya wakipagawa na muziki wakati wa Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika katika Ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam,lilohudhuriwa na mashabiki lukuki, waliokwenda kujionea burudani hizo ambapo pia walitumia fursa hiyo kwa kuelimishwa juu ya huduma mbalimbali zinazotelewa na mtandao wa Vodacom.
Wafanyakazi wa Kampuni ya Samsung wakiwa tayari kwa kutoa huduma mbalimbali zilizokuwa zikipatikana ikiwemo na uuzaji wa simu za bei rahisi za Tsh 70,000 na 100,000 ikiwani sehemu ya ofa ya Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika katika Ufukwewa Coco Beach, jijini Dar es Salaam.
Msanii wa Hip Pop nchini mzee wa michano Fid Q akichana vilivyo wakati wa Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika katika Ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam.
Msanii nguli wa muziki wakizazi kipya nchini,Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay akipanda jukwani tayari kwa kukonga nyoyo za mashabiki wake kwenye Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika katika Ufukwewa Coco Beach, jijini Dar es Salaam.
Msanii mahiri wa Hip Pop nchini Fid Q a.k.a Ngosha akiingia katika steji wakati wa Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika katika Ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam.
Msanii wa kizazi kipya wa muziki wa Hip Pop nchini,Dar Stamina akiwapagawisha mashabiki walio furika katika ufukwe wa CoCo Beach katika Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika jana katika Ufukwe huo, jijini Dar esSalaam.
Baadhi ya mashabiki wakifuatilia jinsi wanamuziki walivyokuwa wanachana katika Tamasha la wazi la Vodacom Tanzania, lililofanyika jana katika Ufukwewa Coco Beach, jijini Dar es Salaam.


MKALI wamuziki wa Hip Hop nchini, Joseph Haule, maarufu kama Profesa Jay, juzi alifanya makubwa katika tamasha la wazi lililoandaliwa na Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania nakufanyika katika Ufukwe wa Coco Beach.

Mbali na Jay, wengine waliokuwapo na kufanya makubwa katika tamasha hilo lililohudhuriwa na watu wengi, alikuwapo Dar Stamina na Fid Q, ambapo wote kwa pamoja walifanikiwa kuwapatia burudani za aina yake.

Tamasha hilo lililofanyika maalum katika Sikukuu ya Pasaka, liliandaliwa maalum kwa ajili ya kusherehekea na wateja wao, pamoja na kuelimishwa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni ya hiyo, ikiwapo Cheka Nao na promosheni ya Mahela, inayowawezesha wateja kujishindia pesa taslimu.

Akizungumza katika tamasha hilo, AfisaUdhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude, aliwashukuru Watanzania kwenda kwa wingi katika tamasha hilo la bure na kushiriki pamoja katika tukio hilo la kiburudani.

Alisema kuwa katika tamasha hilo, wateja wao walikuwa wakipewa elimu jinsi mtandao wao unavyofanyakazi, ikiwapo kujulishwa kwa huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo kwa kupitia tukio hilo lililofurika watu wengi.

"Sisi kama Vodacom tunashukuru kuwa pamoja na mashabiki wa muziki katika tukio hili la wazi lililoandaliwa mahususi kwa ajili yao, huku tukiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja kwa huduma mbalimbali zinazotolewa.

"Tunawaahidi kufanya kazi kwa moyo, pamoja na kuendeleza promosheni zenye mguso wa aina yake, ikiwapo hii ya Vodacom Mahela, ambapo wateja wetu wanapata fursa ya kujishindia fedha taslimu kutoka kwetu," alisema Kaude.

Aidha, msanii Profesa Jay alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani kuwapatia burudani mashabiki wake na kuungwa mkono, sambamba na kuwaimbisha kila wimbo aliotaka kuimba katika tamasha hilo lililokuwa na mvuto wa aina yake.

Baada ya kushuka kwa msanii huyo, alitoa fursa ya Stamina kupanda, huku dakika kumi baadaye, Fid Q naye alipanda na kufanya shoo pamoja na mkali huyo wa Hip Hop anayekubalika na watu wengi kutokana na nyimbo zake kali, ukiwapo wa 'Kabwela'.

Tamasha la wazi la Vodacom lililofanyika kwa siku mbili katika ufukwe huo wa Coco Beach, ambapo wateja wao wote walipata fursa ya kushuhudia burudani hiyo bila kutoa kiingilio cha aina yoyote.

DIAMOND AUTEKA MJI WA BUKOBA


Mwananmuziki wa kizazi kipya ambae yupo juu kwa sasa katika gemu ya Bongo Flava, Diamond akipokelewa na mashabi wake mjini Bukoba baada ya kuwasili Jumamosi Marcha 30, 2013 kwa ziara yake inayoendelea kanda ya ziwa wiki hii ya Pasaka.
Prezidah wa Bongo flava akisalimiana na mashabiki wake Mjini Bukoba wakati alipowasili akiwa njiani kuelekea Hotelini kwake ilibidi Polisi waingilie kati msafara wake kwa kusimamisha magari kuruhusu msafara wake upite na shughuli nyingine zilisimama kwa muda
Moja ya mashamsham ya shabiki wa Diamond akifanya vimbwanga vyake juu ya Pick up wakati wa msafara wa Prezidah wa Bongo Flava alipowasili Bukoba
Diamond akiwapa Vionjo vya nyimbo zake huku akiwasalimia mashabiki wa mjini Bukoba
kwa picha zaidi bofya read more
Diamond akiwa amembeba mtoto huku akisema waacheni watoto waje kwangu
Mashabiki wa Bukoba wakipagawika baada ya kumuoana Preszidah wao
Prezidah Diamond akidhihirisha ukali wake kwa mashabiki wake wa Geita alipofanya sho yake siku ya Ijumaa Marcha 29, 2013 kwenye ziara yake ya Kanda ya ziwa
Diamond na kundi zima la Wafi wakiwa tayari kuingia ukumbini walipokua Geita siku ya Ijumaa Marcha 29, 2013
Prezidah na kundi la Wasafi wakiendelea kukonga nyoyo za mashabiki mjini Geita
Mashabiki wa Geita waliofika kwenye show ya Diamond
Picha na This is Diamond Website