Sunday, December 9, 2018

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YAIBUKA NA TUZO MBILI ZA TAARIFA BORA YA HESABU KWA MWAKA 2017


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akielezea kuhusu taaluma ya Uhasibu kuwa nia muhimu katika maendeleo ya Viwanda   na kutimiza ndoto ya Serikali ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 wakati wa kuhitimisha mkutano wa mwaka wa Wahasibu na kugawa tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa washindi wa mwaka 2017, katika Kituo cha  Uhasibu na Ukaguzi eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akimkabidhi tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi Fungu 23, Bw. Aziz Kifile, katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
hasibu mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango fungu 50, Bw. Mwita Wambura (katikati) akiwa amenyenyua tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la Bunju, Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. 
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila (katikati), Mhasibu Mkuu wa Fungu 50 Bw. Christopher Nkupama (wa pili kushoto), Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi Fungu 23, Bw. Aziz Kifile, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa na furaha baada ya kupokea tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) eneo la Bunju, Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Washindi wa wa makundi mbalimbali ya Tuzo ya taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 zinazotolewa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA)  wakiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu baada ya kukabidhiwa tuzo hizo eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
(Picha na Peter Haule- Wizara ya Fedha na Mipango)





Na, Peter Haule. WFM, Dar es Salaam


Wizara ya Fedha na Mipango Fungu Hamsini (Vote 50) linalohusika na masuala ya utawala, na Fungu ishirini na tatu (Vote 23) la Mhasibu Mkuu wa Serikali yamepata tuzo ya mshindi kwa nafasi ya pili na tatu katika utoaji wa  Taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 katika kundi la Wizara na Idara za Serikali inayoandaliwa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).

Tuzo hizo zimetolewa kwa washindi na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kilichopo  Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa Mkutano wa mwaka wa Wahasibu nchini uliofanyika katika eneo hilo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, taaluma ya Uhasibu inamchango mkubwa katika kukuza uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wanahusika moja kwa moja katika suala la utawala na uongozi kupitia mipango, kudhibiti matumizi ya fedha za  Serikali na pia kuweka mazingira bora ya uwekezaji kuelekea katika maendeleo ya uchumi wa viwanda hivyo kuwa na tija katika agenda hiyo ya Taifa.

“Ni wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha Tanzania inakua na uchumi wa kati ifikapo 2025, jambo hili haliwezi kufikiwa na Serikali pekee bali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wanaweza kutumia taaluma yao na kuishauri Serikali kwa njia mbalimbali, ikiwemo mijadala inayotokana na mikutano ya mwaka ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa, ni vema Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu kuhakikisha wanaandaa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu maendeleo ya viwanda ili wawekezaji wasipotoshwe kuhusu uhalisia wa maendeleo ya Sekta hiyo, kwa kuwa taarifa za fedha huwasaidia walipa kodi, wawekezaji na wadau wengine kufanya maamuzi.

Aidha alisema kuw,a Serikali inaendelea kupambana na wararushwa na watumiaji wabaya wa fedha za umma, kwa kuwa bado wapo Wahasibu ambao sio waaminifu ambao wanacheza na hesabu kupitia taaluma hiyo kupotosha ukweli, alisema kipindi cha kufanya mambo hayo kimepita na yeyote anayeendelea na tabia hiyo awe na uhakika hatabaki salama kama hata badilika.

Alibainisha kuwa suala la maadili ni muhimu sana kwa wahasibu kwa kuwa wao wanaweza kufanya Serikali ikapata mapato au kupoteza na kufanya ndoto za kuwa na uchumi wa viwanda kufikiwa au la

Hata hivyo kufikiwa kwa uchumi wa Viwanda kunategemea uimara wa Sekta ya Umma na Binafsi kwa kuwa wote wanajukumu la msingi la kufikia maendeleo hayo kwa kuwa na taarifa za soko, taarifa za kihasibu na kutafuta suluhisho kwa masoko ya fedha.

Naibu Waziri huyo amefurahishwa na kuongezeka kila mwaka kwa idadi ya washiriki katika ushindani wa taarifa bora ya fedha kutoka Sekta binafsi na umma, hasa Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi za Serikali, kwa kuwa ni hatua kubwa kuelekea katika uwajibikaji na uwazi katika Sekta ya umma na kuongeza imani ya wananchi katika utendaji wa sekta hiyo.

Naibu Waziri Kijaji, amewapongeza washindi wote kwa juhudi walizozifanya na kuwataka waendelee kufanya hivyo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla. Aidha amewapongeza wahasibu kwa kuamua kukaa pamoja na kujadili taaluma ya uhasibu katika maendeleo ya Sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda ambayo ni ajenda ya kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA. Pius Maneno, alisema kuwa tuzo zinazotolewa na NBAA zinalengo la kuhamasisha uwajibikaji na kuandaa taarifa ya fedha zilizo na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Alisema kuwa washindi wa tuzo hizo wanapatikana kupitia mchakato uliosheheni weledi wa hali ya juu kutoka kwa wabobezi wa taaluma ya uhasibu nchini ambao wanaangalia vigezo kadhaa vikiwemo taasisi kusajiliwa nchini, kuwasilisha hesabu kwa wakati na pia kufikisha kiwango cha ubora wa taarifa kuanzia asilimia 75.

Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50, Bw. Christopher Nkupama na Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi Fungu 23, Bw. Aziz Kifile, walisema kuwa tuzo hizo walizopata zinawapa morali ya kufanyakazi kwa umahili zaidi na kuwapongeza watumishi walioko katika idara hizo kwa kufanyakazi kubwa na bila kuchoka kuhakikisha kuwa wanazingatia kanuni na taratibu za uhasibu wanapotekeleza majukumu yao.

Mshindi wa Jumla katika tuzo hizo kwa taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2017 ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tanga Cement Plc na kwa upande wa Wizara na Idara za Serikali ni Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya

Washiriki wa Tuzo hizo ni pamoja na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Wizara na Idara za Serikali na Sekta Binafsi.

No comments: