Sunday, December 9, 2018

TAASISI YA ULINGO WAFANYA USAFI SOKO LA MWANANYAMALA, WAHIMIZA WANAWAKE NCHINI KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI


Makamu Mwenyekiti wa Ulingo Nancy Mrikaria akishiriki kufanya usaifi na wanachama wenzake kwenye soko la Mawananyamala kama maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake ambapo kilele chake kitafanyika Desemba 10 mwaka huu.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Ulingo Bi Saumu Rashid akibandika kipeperushi chenye ujumbe wa kuhamasisha wanawake kujiunga katika vyombo vya maamuzi na kupinga ukatili dhidi ya wanawake katika moja ya kuta za soko la Mwananyamala wakati wanachama wa taasisi hiyo walipofanya usafi sokoni hapo leo.
Picha mbalimbali zikionyesha baadhi ya wanachama wa Taasisi ya Ulingo wakishiriki kufanya usafi katika soko la Mwananyamala ambapo pia wamewahamasisha wanawake kujiunga katika vyombo vya kufanya maamuzi.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Ulingo Bi Saumu Rashid akishiriki kufanya usafi katika soko la Mwananyamala pamoja na wenzake.
Mmoja wa wanachama wa Taasisi ya Ulingo Salma Masoud akibadika kipeperushi chenye ujumbe wa kuhamasisha wanawake kujiunga katika vyombo vya maamuzi na kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake katika moja ya bajaji katika soko la Mwananyamala.Na Said Mwishehe Globu ya Jamii

TAASISI Ulingo ambayo inajihusisha na kusimamia wanasiasa wanawake wa vyama vyote nchini imefanya usafi kwenye Soko la Mwananyamala jijini Dar es Salaam huku ikitumia nafasi hiyo kuwahimiza wanawake wanaofanya kazi katika shughuli mbalimbali kuhakikisha wanashiriki kugombea nafasi zenye maamuzi.

Mbali ya kuhimiza wanawake kushiriki kugombea nafasi zenye maamuzi, pia wamekemea tabia ya vitendo vya rushwa ya ngono ambapo wamesema wanaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa mstari wa mbele kukomesha vitendo vya rushwa ikiwamo rushwa ya ngono.

Wakizungumza leo mapema asubuhi wakati wa kufanya usafi kwa kufagia maeneo yanayozunguka soko hilo la Mwanayamala ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake, wadau mbalimbali wa taasisi hiyo wakiongozwa na viongozi wao wamesema wao kama taasisi inayosimamia wanasiasa wanawake wamekuwa na jukumu la kuendelea kuhamasisha wanawake nchini unapotokea uchaguzi washiriki ili wawe sehemu ya nafasi za maamuzi.

Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo Nancy Mrikaria amesema pamoja na kufanya usafi sokoni hapo wamepata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya viongozi wa soko na moja ya kitu ambacho wamebaini bado kuna idadi ndogo ya wanawake kwenye nafasi za uongozi katika soko hilo , hivyo wameendelea kuwahamasisha ili utakapotokea uchaguzi mwingine wajitokeze kugombea nafasi za uongozi kwa maendeleo ya soko na Taifa kwa ujumla.

"Moja ya jukumu letu ni kuwahamasisha wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi na hasa ambazo zinahusu maamuzi ili kufikia asilimia 50 kwa 50 katika ngazi ya maamuzi.Kwa mfano ndani ya nafasi za uongozi katika Soko hili la Mwananyamala idadi ya wanawake iko chini , hivyo ni kazi yetu kuwakumbusha wanawake wote kwenye maeneo yote kutambua wanayo nafasi ya kugombe nafasi za uongozi,"amesema Mrikaria na kuongeza uongozi ni haki ya watu wote.

Kwa upande wa Mjumbe wa Sekretarieti ya Ulingo Saum Rashid amesema taasisi yao imeamua kufanya usafi kwenye soko hilo kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhimiza usafi wa mazingira nchini ambapo ameelezea namna ambavyo wameitumia siku hiyo kusambaza vipeperushi vinavyozuia rushwa ya ngono.

"Tumefanya usafi kwenye soko la Mwananyamala leo hii, tukiri tu ni jukumu letu sisi wadau wa taasisi ya Ulingo kushiriki kikamilifu kwenye kuweka mazingira yetu safi.Tunajua tunalojukumu pia la kusimamia wanasisa wanawake kutoka vya vyama vyote nchini kuhakikisha wanagombea nafasi zenye maamuzi.Kwetu sisi ni fahari kubwa kufanya usafi soko la Mwananyamala, tumezungumza mengi na viongozi wa soko hili lakini tumeelezea namna ambavyo kuna umuhimu wa kuendelea kukomesha rushwa ya ngono,"amesema.

Ameongeza kuwa kwenye maeneo mengi yakiwamo ya sokoni , kumekuwa na lugha nyingi ambazo zinatolewa za kumdhalilisha mwanamke, hivyo wanaiomba jamii kumheshimu mwanamke kokote aliko."Tunaomba wanawake wanaofanya kazi kwenye maeneo yoyote yale waheshimiwe, ukifika kwenye masoko utasikia baadhi ya watu wanavyotoa lugha za kumdhalilisha mwanamke. Wapo wasichana ambao wanafanya biashara ya mama lishe lakini baadhi ya watu wanaona kama vile wapo kwenye biashara hiyo kwa ajili ya kujiuza.Hii si sawa hata kidogo na tunaikemea vikali,"amesema Rashid.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Soko la Mwananyamala Mbaraka Salum amewashukuru wanawake wa Ulingo kufanya usafi sokoni hapo na kwamba wamefurahishwa na uamuzi wao wa kuchagua soko lao.Hata hivyo amesema changamoto kubwa iliyopo taka hizo ambazo zimekusanywa baada ya kufanyika usafi hawana pa kuzipeleka kwani gari ya manispaa kwa wiki inafika mara moja na hivyo taka kuzagaa.

"Changamoto yetu kubwa hapa ni gari la taka , kwa wiki linakuja mara moja tu.Hivyo taka zinajazana na kama uavyojua kuna taka zikikaa zaidi siku moja zinaanza kuharibika na kutoa harufu kali, hivyo tunaomba manispaa waje wachukue taka kwa wakati.Tunafirikia kubeba taka hizi na kuzipeleka manispaa kwani wao ndio watajua wapi wanatakiwa kuzipeleka na Mkuu wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam alishawahi kusema kama taka hazizolewi na zinarundikana sehemu moja basi zibebebwe zipelekwe ofisi ya mazingira,"amesema Salum.

Kuhusu usawa kwenye nafasi za uongozi katika soko hilo, Salum amesema wamekuwa wakihamasisha wanawake kugombea uongozi lakini changamoto iliyopo idadi ya wanaojitokeza ni ndogo ambapo amefafanua uchaguzi uliopita sokoni hapo walijitokeza watatu na hivyo wawili wakachaguliwa "Kati ya viongozi tisa wa soko la Mwananyamala wanawake wapo wawili tu na wanaume saba, sababu kubwa wanawake wenyewe hawajitokezi kugombea pindi uchaguzi unapotangazwa lakini tunaendelea kuwahamasisha."

No comments: