Sunday, December 9, 2018

TASWA YAKAMILISHA RASIMU YA KWANZA YA MAPENDEKEZO YA KATIBA YAKE

KAMATI ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), imekamilisha Rasimu ya Kwanza ya Mapendekezo ya Katiba ya chama hicho na itaanza kutolewa kwa wadau mbalimbali leo Jumapili Desemba 9, 2018 kwa ajili ya kujadiliwa.

Hatua ya kuandaa rasimu hiyo ya kwanza imefanywa na Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya TASWA kwa kuangalia Katiba za vyama mbalimbali duniani vinavyohusiana na waandishi wa habari za michezo na pia kupitia muongozo kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS), ambacho TASWA ni mwanachama.

Pia Kamati imechambua Katiba ya sasa ya TASWA na kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu maeneo yenye upungufu kwa nia ya kuiboresha.Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi katika rasimu hiyo baadhi yakiwa ni sifa za mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo wa uongozi, sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi.

Pia kuna mapendekezo katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati ya Utendaji.Kutokana na hali hiyo, Kamati imepanga hatua ya kwanza baada ya kuitoa rasimu hiyo leo, itapokea maoni binafsi ya wadau kwa njia ya email (katibataswatz@yahoo.com), kisha itakutana na wahariri wa habari za michezo, waandishi waandamizi na waandishi chipukizi kwa kadri mtakavyotaarifiwa.

Baada ya kupokea maoni kutoka makundi hayo, Kamati itafanya mikutano miwili, ambapo wa kwanza utakuwa wa wadau wote kuijadili kwa pamoja na kisha kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ya TASWA utafanyika Mkutano Mkuu wa kuipitisha na kuiwasilisha kwa Msajili tayari kwa Uchaguzi Mkuu haraka iwezekanavyo.Ni matumaini ya Kamati ya Katiba kila mdau ataisoma vyema rasimu hiyo na kutoa mchango wake na mwisho wa kufanya hivyo ni Desemba 12 mwaka huu. Mapendekezo ya Rasimu hiyo nimeambatanisha katika email zenu.

Kamati ya Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 25 mwaka huu na badala yake BMT ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.

Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi wengine ni Katibu wa Kamati Amir Mhando ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari, Gift Macha ambaye ni Katibu Msaidizi wa Kamati.

Wajumbe ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA, Nasongelya Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelu.

Nawasilisha,
Amir Mhando
Katibu wa Kamati ya Katiba/ Katibu Mkuu TASWA
9/12/2018

No comments: