Saturday, December 8, 2018

UJENZI WA GATI NYAMISATI WAANZA, SHEHENA YA VIFAA YAANZA KUWASILI -KUANDIKWA


NA MWAMVUA MWINYI, KIBITI 

NAIBU waziri wa Ujenzi, Elias Kuandikwa amesema ujenzi wa gati, uliokuwa ukisubiriwa kwa kipindi kirefu na wakazi wa Nyamisati wilayani Kibiti mkoani Pwani umeanza ambapo shehena ya vifaa vya ujenzi vimeanza kuwasili tayari kwa ajili ya kazi. 

Aidha amewatoa wasiwasi wakazi wa Mafia kuhusu gati la Kilindoni ,kwamba linatarajiwa kuboreshwa kwa kuondoa dosari ndogondogo zilizopo ili liwe la kisasa. 

Akizungumza na wananchi wakati alipotembelea eneo litakapojengwa gati hilo, katika muendelezo wa ziara yake mkoani hapo, Kuandikwa alisema ujenzi utakuwa wa miaka miwili kwa gharama ya sh. bilioni 14 .

Alimtaka , mkandarasi wa gati hilo kufanya kazi inayotakiwa kwa kuhakikisha, ujenzi unakamilika kwa wakati ikiwezekana kuukamilisha kabla ya miezi 24.
Kuandikwa alisema, ujenzi umeshaanza na mkataba ulisainiwa tarehe 24,octoba mwaka huu, ombi lake ni kuona mkandarasi anamaliza kazi haraka.
“Fedha zipo hatutaki kuona mkandarasi anasuasua, gati litasaidia kurahisisha usafiri kwani ndio kiu ya wakazi wa Nyamisati na Mafia”
“Itakuwa gati la kisasa na sasa tunakwenda kufanya maboresho katika gati la Kilindoni wilayani Mafia ili kuwa na gati la uhakika ,kwa kuwa itazingatia ubora, teknolojia mpya kwa lengo la magati haya yaweze kudumu kwa miaka mingi “alisisitiza Kuandikwa. 

Pamoja na hayo, alielezea ujenzi huo utakwenda pamoja na maboresho ya barabara ya Bungu -Nyamisati itakayosaidia kurahisisha usafiri .
Akiwa barabara ya barabara ya Mkuranga -Kisiju kiwango cha lami, yenye urefu wa 1.8km alimpongeza meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) mkoani Pwani, Yudas Msangi kwa kubana matumizi kwenye miradi na kuweza kutumia katika miradi mingine. 


Msangi alisema kwasasa wanaendelea na kazi za kufungua na kuboresha baadhi ya barabara muhimu kuelekea katika miradi mikubwa mbalimbali.

No comments: