Thursday, December 20, 2018

UCSAF KUPELEKA MAWASILIANO YA UHAKIKA KWA WANACHI WA PEMBA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akiwasili kisiwani Pemba kukagua changamoto za mawasiliano. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah na wa kwanza kushoto ni Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Baucha
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyenyoosha mkono) akijadiliana na Shehia wa Sheha ya Kiungoni, Omari Khamisi Othman kuhusu eneo la kujenga mnara wa mawasiliano katika ziara yake ya kukagua changamoto za mawasiliano Pemba. Aliyevaa miwani akisikiliza kwa makini ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akiwa kwenye boti eneo la Makangale – Mnarani akikagua upatikanaji wa mawasiliano wakati wa ziara yake Pemba. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter UlangaNaibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi kwa wananchi waishio kwenye Mkoa wa Kaskazini kisiwani Pemba na kubaini kuwa yapo baadhi ya maeneo yana usikivu mdogo wa mawasiliano na mengine hakuna kabisa mawasiliano ya simu za mkononi

Nditiye aliambatana na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah ambaye ndiye chimbuko la ziara hiyo kwa kuuliza maswali Bungeni wakati wa vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu changamoto ya mawasiliano kisiwani Pemba.

“Zipo changamoto mbali mbali ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, wananchi wanapata tabu za kuwasiliana hasa nyakati za usiku hasa wakipata msiba au mgonjwa, tuliwasilisha changamoto hizi Bungeni ili ziweze kutekelezwa,” amesema Maida

Nditiye amebaini uwepo wa usikivu mdogo wa mawasiliano na ukosefu wa mawasiliano wakati wa ziara yake kwenye Shehia ya Kiungoni – Wingwi, Dodeani, Kiuyu Mbuyuni, Sizini – Chwaka, Tumbe, Kipande Konge na Makangale – Mnarani zilizopo kwenye Wilaya ya Micheweni pamoja na kwenye Shehia nyingine za Weni – Tungamaa – Machwengwe, Mtambwe, Mkanjuni na Kivumoni zilizopo kwenye Wilaya ya Wete

“Kuna maeneo ambayo minara ipo ila mawasiliano hayana nguvu na sehemu nyingine hakuna mawasiliano kabisa kutokana na jiografia ya Pemba, nimekuja na wataalamu wa kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), nimewaelekeza hili walifanyie kazi, raha yangu ni kuona wananchi wote wana wasiliana,” amesema Nditiye

Amefafanua kuwa masuala ya mawasiliano ni masuala ya muungano ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha UCSAF ili kupeleka mawasiliano nchi nzima, Tanzania Bara na Visiwani kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara

“Nimeshuhudia hapa nilipo hamna mawasiliano na simu yangu ni kopo tu, sipati mtandao wowote”, amesema Nditiye. Ameongeza kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa popote ambapo hamna mawasiliano wanafikisha mawasiliano kwa wananchi, kwa kuwa akiwa njiani ziarani humo ameshuhudia ukosefu wa mawasiliano

Katika ziara hiyo, Nditiye aliambatana na Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Peter Ulanga ambapo amemwelekeza kuchukua maeneo yote ambayo hayana usikivu wa kutosha na yale ambayo hayana mawasiliano kabisa ili waanze kuyafanyia kazi mapema mwezi Januari mwakani

“Tunachukua changamoto hizi ili tuweze kuongeza usikivu wa mawasiliano” amesema Mhandisi Ulanga. Ulanga ameongeza kuwa UCSAF itahakikisha mwananchi akiwa ndani au nje ya nyumba yake kwenye eneo lote la kisiwa cha Pemba mwananchi anapata mawasiliano mazuri

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamisi Othmani amemwambia Nditiye kuwa, “tuna imani ujio wako utatuondolea changamoto ya mawasiliano katika mkoa wa Kaskazini na kisiwa cha pemba kwa ujumla kwa kuwa umeona hali halisi,”

Sheha wa Shehia ya Kipange, Ramadhan Omari Ahmed akizungumza kwa niaba ya masheha wenzake amesema kuwa anamshukuru Nditiye na msafara wake pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah kwa kupata ujio huu ili kufika maeneo hayo ambapo amesema kuwa, “hamna mawasiliano popote ya TIGO, Vodacom au Zante, pale tunapohitaji mawasiliano tunakwenda sehemu kama vile kupanda juu ya mlima au uende kwenye uwanja wa mpira au kwa kutembea umbali wa kilomita 1.5 hadi 3.1 kutafuta mawasiliano,”.

“Ni faraja kubwa sana kwa kutembelewa na kuja kusikiliza maoni ya wananchi kwa kuwa mawasiliano hayako vizuri, tukitaka kupiga simu tukiwa ndani inatukwaza, hatupati mawasiliano, lengo tupate mawasiliano na wametuahidi tatizo la mawasiliano sio tu kwa Kiungoni ila litaisha Pemba yote”, amesema Shehia wa Kiungoni, Omary Khamisi Othmani

“Kilio hiki kimetukwaza muda mrefu, naamini alichokuarifu Maida kitafanyiwa kazi, tumefarijika sana kuona viongozi mnashuka hadi chini kusikiliza wananchi, naamini wataalamu wako wataifanyia kazi changamoto ya mawasiliano ili wananchi waweze kuwasiliana,” amesisitiza Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Salama Mbarouk Khatib

Katika hatua nyingine, Nditiye amekagua vituo viwili vya TEHAMA kati ya kumi vilivyojengwa na UCSAF kwenye kisiwa cha Unguja na Pemba ili wanafunzi waweze kujifunza TEHAMA na wananchi watumie TEHAMA ambapo ametoa wito kwamba wananchi waruhusiwe kutumia bure kituo cha TEHAMA kwa muda kabla ya kuanza kuwatoza gharama za uendeshaji wa vituo hivyo ili wafaidi matunda ya Serikali yao

Nditiye ameongeza kuwa mawasiliano ni ulinzi na usalama na mawasiliano ni uchumi ambapo mwananchi akiwa na simu, inamuwezesha kuuza na kununua kiurahisi bidhaa zake, hivyo kwa kutumia TEHAMA tunajiunga na dunia kupitia mawasiliano

No comments: