Thursday, December 20, 2018

Ushirika Afya ni Mkombozi wa Afya ya Mkulima- Waziri Umm


Na Grace Michael, Nachingwea

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa mpango wa Ushirika Afya ndio njia pekee na ya kisasa inayomwezesha mkulima kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote na kuepukana na upotevu wa fedha nyingi kwa kulipia gharama za matibabu.

Amesema kuwa ili mkulima aweze kunufaika na fedha anazozipata kutokana na kuuza mazao yake ya biashara ni lazima awe na uhakika wa kupata huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Ameyasema hayo wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma pamoja na uhamasishaji wa wananchi na wakulima kujiunga na mpango wa Ushirika Afya ili waweze kunufaika na huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

“Ndugu zangu wana Nachingwea, nafahamu kabisa mmeweka mipango mingi kwenye fedha zenu mtakazopata kutoka kwenye mazao mliyouza lakini niwaombe sana katika vipaumbele vyenu suala la Ushirika Afya liwe ni miongoni mwake, kuwa ndani ya mpango huu kunakusaidia wewe na familia yako kutokupoteza fedha zako unapopatwa na magonjwa,” alisema Mhe. Ummy.

Alifafanua kuwa gharama atakayotumia mkulima huyo kujiunga na Ushirika Afya ni ndogo sana ikilinganishwa na kugharamia huduma za matibabu kwa fedha taslimu hali ambayo imesababisha wananchi wengi kuingia kwenye umasikini kwa kuuza mali zao ili wapate fedha za kujitibia.

“Kuwa ndani ya NHIF ni nafuu kubwa sana, familia itakuwa na amani wakati wote hata pale wanapopatwa na magonjwa, gharama kwa mtu mmoja kupitia Ushirika Afya ni shilingi 76,800 tu lakini unatibiwa katika vituo vya ngazi zote hapa nchini na hata kwa yale magonjwa ya gharama kubwa hivyo niwaombe sana mtakapopata fedha mhakikishe mnajiunga mara moja,” alisema Mhe. Ummy.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga aliwahakikishia wananchi wilayani Nachingwea kuwa, Mfuko umejipanga vyema katika kutoa huduma kwa wanachama wake kwa ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za matibabu.

Alisema kuwa Mfuko umeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha unawafikia wananchi katika maeneo yao na kuwasajili lengo ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na huduma za matibabu kupitia NHIF.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy aliwahakikishia wananchi hao juu ya upatikanaji wa huduma za matibabu kuwa ni mzuri na bora zaidi hususan upatikanaji wa dawa ambao ni zaidi ya asilimia 93 katika vituo vya kutolea huduma. 

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akielezea umuhimu wa kujiunga na Ushirika Afya kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika wilayani Nachingwea.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mhe. Hassan Masala.

 Wananchi wilayani Nachingwea wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wakati akielezea upatikanaji wa huduma za matibabu.
 Wananchi wakisoma vipeperushi vya Ushirika Afya wakati wa uhamasishaji wilayani Nachingwea.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi fomu 1,000 kwa Kiongozi wa Vyama Vya Ushirika wilaya ya Nachingwea.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi kadi kwa Mwanaushirika aliyejiunga na mpango wa Ushirika Afya.
 Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Bi. Rukia Muwango akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Benard Konga wakifuatilia maelezo ya Mhe. Waziri.Mhe. Waziri akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa vyama vya Ushirika katika Wilaya ya Nachingwea.

No comments: