Saturday, December 22, 2018

WAZIRI WA UCHUKUZI AENDA KIMYA KIMYA KITUO CHA MABASI UBUNGO,ABAINI UPANDISHWAJI NAULI KIHOLELA

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii

HALI ya usafiri katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam hasa kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka inaonekana kubadilika kutokana na nauli kupandishwa kiholela bila kufuata utaratibu was Serikali.

Uwepo wa madalali katika kituo hicho nao umeelezwa unachangia kuongezeka kwa adha ya usafiri na hivyo abiria kutoa ombi kwa Serikali kuhakikisha kituoni hapo taratibu zinafuatwa.

Hayo  yamebainika baada ya Waziri wa  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe kufaya ziara kituoni hapo kuona hali ya usafiri akiwa kama abiria ambapo hata yeye alipewa nauli mpya ambayo haiko katika bei elekezi.

"Nimefika kitoni hapo saa 11:15 alfajiri nakuzunguka kwenye baadhi ya mabasi na kubaini  baadhi ya abiria kulipishwa nauli tofauti na bei elekezi ya  Serikali,"amesema Mhandisi Kamwelwe.Amesema baada ya ukaguzi amebaini abiria kulipa nauli tofautitofauti inatokana na kuwepo kwa madalali nje ya kituo.

Hivyo amesema kuna haja yakupekeka mapendekezo bungeni  ili kuwepo kwa tiketi za mfumo wa kieletroniki zitakazosaidia kuondokana na  ulanguzi unaoumiza abiria.Baadhi ya abiria wamesema kinachosababisha nauli ipande ni madalali wanaokatisha tiketi nje ya kituo.

Mmoja wa abiria Joseph Malisa amesema unapoenda kwenye ofisi au gari husika unaambiwa gari limejaa lakini nje ya kituo unakuta madalali wanauza tiketi za basi hiyo waliodai kuwa imejaa."Unapofika kwenye gari au ofisi zao unaambiwa nafasi zimejaa lakini nje ya kituo madalali wanauza tiketi kwa bei ya juu na mimi nataka kusafiri inanililazimu kukata bei ya juu" amesema Malisa.

 Abiria nwingine  Emili Msuya amesema kupanda kwa nauli kiholela kumechangiwa na watu wasio rasmi ikiwemo wapiga debe wanaolundikana ndani ya kituo, hivyo Serikali iangalie utaratibu wa kuwaondoa.Meneja wa Kituo cha Ubungo jijini Dar es Salaam Imani Kasagala amesema mabasi yote yanapaswa kuingia ndani ya kituo cha mabasi Ubungo badala ya wamiliki kupaki nje na kutafuta madalali ambao ndio chanzo cha   kwa nauli hizo kupanda.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ramadhan Kailima amesema kuwa abiria wakiona kuna kupandishiwa nauli wanatakiwa kutoa taarifa.Amesema mabasi yote yanakaguliwa na kupongeza Ukaguzi unaofanywa katika kituo hicho. 
 Askari wa Usalama Barabarani Ibrahim Samwix akifanya ukaguzi katika kituo  Kikuu cha  Mabasi Ubungo,jijini Dar es Salaam. 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ramadhan Kailima akizungumza na abiria katika basi wakati alipofanya ziara katika kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Ramadhan Kailima akipewa maelekezo na Askari wakati alipofanya  ziara kuangalia Usalama wa abiria katika mabasi wanayosafiri nayo leo jijini Dar es Salaam.

 Mwenyekiti wa Umoja wa Chama cha Madereva Wafanyakazi (TADWU) Shaban Mdemu akizungumza na waandishi habari wakati ukaguzi wa mabasi ya mikoani kuelekea siku kuu za mwisho wa mwaka katika kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam. 
 Baadhi ya wananchi wakiangalia ukaguzi katika kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ramadhan Kailima Kailima akizungumza na waandishi wa habari wakati alipofanya ziara katika kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
 Askari wa Usalama Barabarani katika Kituo cha Ukaguzi wa Mabasi Ibrahim Samwix akizungumza na waandishi habari kuhusiana na ukaguzi  wa mabasi katika kituo cha mabasi leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe akiwa katika basi mara alipofanya ziara katika kituo Kikuu cha Mabasi ikiwa ni kuangalia hali ya usafiri kuelekea siku za mwisho wa mwaka,jijini Dar es Salaam.

No comments: