Thursday, December 6, 2018

TUCTA YAKIRI KUSHIRIKISHWA KWENYE MCHAKATO WA UTUNGWAJI WA KANUNI ZA MALIPO YA WASTAAFU

Rais wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amekiri shirikisho hilo kuwa na majadiliano mbalimbali katika ngazi ya Utatu na Upili yaani Serikali, Wafanyakazi na Waajiri kuhusu hoja ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi za jamii nchini. 

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Morogoro leo sanjari na vikao vyao vya kikatiba takribani kwa siku mbili, Nyamhokya amesema wajumbe wamekuwa na fursa ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Ustawi wa Wafanyakazi nchini pamoja na kutoa tamko baada ya kuhudhuria kikao hicho rasmi cha utendaji wa maswala yanayotakiwa kufanyiwa utekelezaji.

Moja ya agenda zilizojadiliwa kwa undani ni swala la uunganiswaji wa wa mifuko ya hifadhi ya jamii na mkanganyiko uliojitokeza baada ya serikali kutangaza kuanza kutumika kwa vikokotoo vya mafao ya pensheni kwa wastaafu wa mifuko ya PSSSF na NSSF kuanzia Agosti 8 2018.

Aliongeza kuwa Serikali na Wadau wengine wakiwemo Waajiri walipokea hoja ya wafanyakazi na kuanza mchakato wa uunganishwaji wa mifuko ambapo TUCTA kwa niaba ya wafanyakazi walishirikishwa kwa majadiliano ya Utatu kupitia Vikao vya Kisheria ambavyo pia vilitoa fursa ya wawakilishi wa wafanyakazi kukutana na kujadiliana na wadau wote wakiwemo Waajiri, Serikali, Kamati za Bunge, NGO's, Watumishi wa Mifuko iliyokuwepo kabla ya kuunganishwa na Wafanyakazi wenyewe. 

Amefafanua kwamba TUCTA kama mwakilishi wa Wafanyakazi nchini walishiriki katika mchakato mzima wa kutungwa kwa sheria ya PSSSF namba 2 ya mwaka 2018 kwa kutoa maoni na msimamo wao kwenye vikao mbalimbali vya wadau, ambapo mapendekezo yao kwenye sheria hiyo yalizingatiwa kwa kiwango kikubwa sana. 

Alisema pia baada ya wasilisho la TUCTA la hoja za wafanyakazi kwenye vikao hivyo vya wadau, Serikali na TUCTA walishindwa kufikia muafaka hivyo serikali iliamua hoja za pande zote ziwasilishwe kwenye Baraza la Utatu la Ushauri (LESCO), ambalo lina wawakilishi wa TUCTA (4), Waajiri (4), Serikali (4) na Wataalam wawili chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu.

Kwa mujibu wa Sheria, Kikao cha LESCO ndicho kiako cha mwisho cha Utatu katika kumshauri Waziri mwenye dhamana juu ya masuala mbalimbali yayanayohusiana na kazi ikiwa ni pamoja na utungwaji wa sheria na kanuni mbalimbali zinazogusa wafanyakazi nchini. Mvutano uliojitokeza ndani ya kikao hicho kuhusu vikokotoo vya 1/580, 25% na 12.5 ambavyo vilipendekezwa na serikali na Wafanyakazi kuvipinga ilisabibisha muafaka ufikiwe kwa kura. 

Uchache wa kura za Wawakilishi na Wafanyakazi ndani ya LESCO, upande wa Serikali na wadau wengine walishinda hivyo serikali kupitia Waziri mwenye dhamana ikandelea na hatua ya kutangaza kuanza kutumika kwa kanuni hizo.      
Rais wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya akizungumza na wanahabari mjini Morogoro leo, wakati wa kutoa tamko la Kamati ya TUCTA Taifa kuhusu mkanganyiko wa kikotoo cha mafao ya pensheni yatolewayo na mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tannzania. Kushoto ni Makamu Rais wa TUCTA, Qambos Sulle, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Dk Yahya Msigwa (wa pili kulia) na Naibu Katibu Mkuu Jones Majura. 
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), wakimsikiliza Rais wa shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokya alipozungumza na wanahabari mjini Morogoro leo, wakati wa kutoa tamko la Kamati ya TUCTA Taifa kuhusu mkanganyiko wa kikotoo cha mafao ya pensheni yatolewayo na mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania. 
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), wakiimba wimbo wa 'Solidarity Forever' wakati wa mkutano huo. 
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), wakimsikiliza Rais wa shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokya alipozungumza na wanahabari mjini Morogoro leo, wakati wa kutoa tamko la Kamati ya TUCTA Taifa kuhusu mkanganyiko wa kikotoo cha mafao ya pensheni yatolewayo na mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania. 

No comments: