Thursday, December 6, 2018

WAZIRI WA KILIMO AAGIZA VYUO VIKUU KUTANGAZA MATOKEO YA TAFITI ZAO

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza kwenye sherehe ya nne ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tarehe 6 Disemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akimkabidhi zawadi ya mwanafunzi bora kitaaluma ngazi ya Stashahada ya Uhasibu na Uongozi Ndg Methusela Piniel kwenye sherehe ya nne ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tarehe 6 Disemba 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akimkabidhi zawadi ya mwanafunzi bora kitaaluma ngazi ya Shahada ya Biashara na Uchumi Bi Diana Kibodya kwenye sherehe ya nne ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tarehe 6 Disemba 2018.
Makamu Mkuu Wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi Prof Faustine K. Bee akitoa taarifa ya chuo hicho kwenye sherehe ya nne ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tarehe 6 Disemba 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi sambamba na baadhi ya wahitimu kwenye sherehe ya nne ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma chuoni hapo tarehe 6 Disemba 2018.


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kilimanjaro

Imebainika kuwa tafiti na machapisho mengi yanayofanywa na wanataaluma na wanafunzi katika Vyuo mbalimbali si tu zinasaidia kujenga taswira za vyuo bali zinapaswa kuwa sehemu ya kufanya elimu iwe nzuri na bora zaidi.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 6 Disemba 2018 wakati akizungumza kwenye sherehe ya nne ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Mhe Hasunga amewaagiza watendaji wa Chuo hicho sambamba na vyuo vingine nchini kufanya tafiti za kutosha katika tasnia ya ushirika na kuhakikisha kuwa Matokeo ya tafiti hizo yanawafikia walengwa. "Serikali nayo kwa upande wake imeweka na itaendelea kuweka mazingira rafiki zaidi yatakayosaidia kuimarisha dhana ya ushirika miongoni mwa jamii ya watanzania" Alisema

Alisisitiza kuwa moja ya kadhia inayovikumba vyuo mbalimbali nchini ni kutowekwa wazi kwa haraka machapisho na Tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutangaza ili zijulikane katika sehemu mbalimbali Duniani.

"Ndugu zangu hakuna nchi inaweza kuendelea bila kuwekeza kwenye utafiti hivyo ni lazima kuongeza jitihada na juhudi katika utafiti" Alisisitiza.Alisema kuwa Vyuo vikuu vinatambuliwa kama taasisi zilizobobea katika kufundisha, kujifunzia, kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri hivyo vinapaswa kutangaza matokeo ya Tafiti wanazozifanya.

Alisema, kupitia elimu hiyo itolewayo na vyuo vikuu, maarifa, ujuzi na mtazamo chanya kwa maendeleo vinaweza kujengwa, kuboreshwa, kuendelezwa na kusambazwa kwa walengwa mbalimbali. Kwa msingi huo, utoaji elimu bora inayokidhi viwango na inayoendana na mahitaji ya soko lazima izingatiwe. 

Akizungumzia Ushirika, Mhe Hasunga amesema kuwa Ushirika ni dhana ya kujisaidia wenyewe katika maendeleo. "Hatuna budi sisi kama wadau wa ushirika kuhakikisha kuwa tunajenga misingi imara ya elimu ya ushirika kwa wadau wetu ili waweze kujikwamua katika wimbi la umaskini kwa kuanzisha shughuli zenye tija (kwa mfano ushirika wa viwanda) zitakazowapatia kipato cha uhakika" Alisisisitiza 

Aidha, Waziri Hasunga ameupongeza uongozi Wa chuo kikuu cha Ushirika Mosho kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya Ushirika nchini kwa kuandaa na kutoa wataalamu katika sekta ya Ushirika kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada hadi shahada za awali, Umahiri na Uzamivu.

Akitoa maelezo ya awali Makamu Mkuu Wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi Prof Faustine K. Bee wakati akimkaribisha mgeni rasmi alisema kuwa sekta ya Kilimo imekumbwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na Ushirika kama dhana kuwa na mtazamo hasi kwa baadhi ya watu inayosababishwa na uendeshwaji Wa Ushirika usiokuwa na tija kwa wanachana, jamii na Taifa kwa ujumla.

"Vilevile migogoro ya Mara kwa mara katika vyama vya Ushirika kutokana na kuwepo kwa watu wachache wasiowaaminifu na kukosa maadili" Alikaririwa Prof Bee

Alisema Chuo hicho kinatambua kuwa vyama vya Ushirika ni vyombo muhimu sana katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/2017) - (2020/20121), Malengo yavMaendeleo endelevu 2030 pamoja na ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

No comments: