Thursday, December 6, 2018

SERIKALI YAZISHAURI BENKI NCHINI KUSHUSHA RIBA ZA MIKOPO KUCHOCHEA UCHUMI WA VIWANDA

Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amezitaka Benki nchini kushusha viwango vya riba za mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Tawi la Benki Azania, Sokoine, na kusisitiza kuwa Benki zina nafasi kubwa wa kuisaidia nchi kufikia azma yake ya kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji na biashara za wananchi.

Alisema kuwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinapungua, ikiwemo Benki Kuu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara, kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.

"Tumepunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17" aliongeza Dkt. Kijaji

"kama haya yote yamefanyika, iweje benki ziendelee kutoza riba ya asilimia 17 kwa kisingizio cha kuogopa mikopo chechefu wakati Serikali kupitia Benki Kuu, imeanzisha kanzi data ya kuhifadhi na kutoa taarifa ya wakopaji (Credit Reference Bureau System)" alihoji Dkt. Kijaji

 Aidha, Dkt. Kijaji ameelezea kusikitishwa kwake na hatua ya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki 5 zilizofungiwa kwa kipindi maalum kushiriki katika kuuza na kununua fedha za kigeni baada ya kukiuka taratibu za biashara hiyo.

" Kisheria, benki zote za biashara zinatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu kuhusu miamala ya Soko la Fedha za Kigeni kati ya Mabenki waliyofanya kwa siku lakini Benki yako ni miongoni mwa benki zilizovunja utaratibu huu, hii niaibu!" alisisitiza Dkt. Kijaji "

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania Bw. Charles Itembe, amesema Benki yake imeendelea kufanya vizuri katika soko kwa kupata faida na kwamba imejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.

"Benki yetu, mwaka 2017, imetengeneza faida ya shilingi bilioni 1.81 ikilinganishwa na hasara ya Shilingi bilioni 6 iliyoripotiwa Desemba 2016, na imeongeza rasilimali zake kutoka sh. bilioni 338 hadi bilioni 390" alisema Bw. Charles Itembe.

Alisema kuwa Benki yake imeongeza kiasi cha mikopo iliyotoa kutoka sh. bilioni 129 mwaka 2016 hadi sh. bilioni 187.7  mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 10.23 huku akiba za wateja zikiongezeka kutoka shilingi bilioni 236 mwaka 2016 hadi sh. bilioni 271 mwaka jana.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Azania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Watumishi wa Umma (PSSSF) Bw. Eliud Sanga, ameitaka Benki hiyo kutekeleza mkakati wake wa kuanza kutoa mikopo ili kuimarisha Sekta ya ujenzi wa viwanda nchini.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akiwa katika ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine, Jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Benki hiyo Bw. Charles Itembe na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Bw. Eliud Sanga.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akihutubia wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine, Jijini Dodoma, ambapo aliipongeza benki hiyo kwa kuwa miongoni mwa benki chache zilizofanya maamuzi sahihi ya kuunga sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamia Dodoma kwa vitendo.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akihutubia wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la benki ya Azania, Sokoine Jijini Dodoma, ambapo alitoa wito kwa benki hiyo kupunguza riba za mikopo ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa bodi ya Benki ya Azania, Bw. Eliud Sanga, baada ya kuhutubia katika ufunguzi wa tawi la benki hiyo la Sokoine Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine, Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiagana na Mkurugenzi wa Benki ya Azania, Bw. Charles Itembe, mara baada ya kukamilisha ufunguzi rasmi wa tawi jipya la benki hiyo, Sokoine na kutembelea ofisi za tawi hilo, Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti na wageni waliokuwa meza kuu mara baada ya kufungua rasmi Tawi la Benki ya Azania iliyopewa jina la Sokoine, Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti na watumishi wa Benki ya Azania baada ya ufunguzi rasmi wa tawi jipya la benki hiyo la Sokoine, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa benki ya Azania ambao walihudhuria katika ufunguzi wa tawi jipya la benki hiyo Sokoine Jijini Dodoma.


(Picha na Saidina Msangi-Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments: