Thursday, December 6, 2018

MKUU WA WILAYA NAMTUMBO SOPHIA KIZIGO AONGOZA OPERESHENI YA KUONDOA WAVAMIZI NDANI YA HIFADHI

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ikongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Kizigo imeamua kufanya operesheni maalumu ya kusaka na kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya hifadhi ya Mbarang'andu ambapo kuna watu kadhaa wamekamatwa na sasa wanaohojiwa.

Akizungumzia operesheni hiyo Mkuu wa Wilaya Kizigo ameiambia leo, Michuzi Blog kuwa wameanza kuifanya juzi na jana (Desemba 4 na Desemba 5 mwaka 2018) ambapo mbali ya kamati ya ulinzi na usalama pia kulikuwepo na vikosi kazi na timu ya wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri ya wilaya hiyo na kwamba uamuzi huo wa kufanya msako umekuja baada ya doria ya kwanza iliyofanyika kwa njia ya anga (ndege) ambapo walijionea uharibifu uliofanyika kwenye hifadhi ya Ushoroba wa Selous , Niassa, Mbarang'andu , Kisungule na Kimbanda.

"Kwa kutumia usafiri wa anga ambao tumefanya kwenye maeneo mbalimbali ya hifadhi tumejionea namna ambavyo kuna uharibu wa mazingira.Hivyo jana tumeamua kufanya msako maalumu wenye lengo la kuwaondoa wavamizi ambao wanaharibu hifadhi hiyo,"amesema Mkuu wa Wilaya Kizigo.

Amesema katika kuhakikisha wanafanikiwa kwenye operesheni hiyo juzi na jana waliamua kwenda kwa miguu maeneo ambayo yamefanyiwa uharibifu na tayari kuna baadhi ya watu ambao wamewakamata kwa kutuhuma za kuharibu hifadhi ambapo pia amesema wapo watu ambao wanaingia kwenye msitu huo kwa ajili ya kufanya ujangiri kwa kuua wanyama.

Amesema baadhi ya watu ambao wamewahoji wamedai wanaingia kwenye hifadhi hiyo kwa ajili ya kilimo lakini ukweli ni kwamba watu hao hao ndio wamekuwa wakihusika na ujangiri, uharibifu wa mazingira kwa kutaka miti bila mpangilio."Tunaendelea kuwahoji watu ambao tumewakamata ndani ya hifadhi na kisha sheria itachukua mkondo wake,"amesisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo.

Wananchi mbalimbali ambao wamezungumza na Michuzi Blog kuhusu operesheni hiyo wamempongeza Mkuu wa Wilaya kwa hatua anazochukua kuhakikisha hifadhi zilizopo ndani ya wilaya yao zinakuwa salama kwa kutoharibiwa na watu ambao wamekuwa na tabia ya kuvamia na kufanya matukio ya ujangiri. Wamemuahidi Mkuu wa Wilaya pamoja na wasaidizi wake kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kuwataja kwa majina watu ambao wanavamia misitu hiyo na kufanya uharibifu.


KAMATI ya Ulinzi na Usalama ikongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Kizigo wakiendelea kukamata vifaa mbambali vya watu waliovamia maeneo ya hifadhi ya Mbarang'andu ambapo kuna watu kadhaa wamekamatwa na sasa wanaohojiwa.
Sehemu ya Kamati i ya Ulinzi na Usalama ikongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Kizigo (wa pilia kulia) wakiwa kwenye operesheni maalumu ya kusaka na kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya hifadhi ya Mbarang'andu ambapo kuna watu kadhaa wamekamatwa na sasa wanaohojiwa.
Baadhi ya Watuhumiwa waliokamatwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ikongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Kizigo  (hayupo pichani) walipokuwa wakifanya operesheni maalumu ya kusaka na kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya hifadhi ya Mbarang'andu ambapo watu kadhaa wamekamatwa na sasa wanaohojiwa.

No comments: