Saturday, December 8, 2018

MWANAMKE APAMBANA NA JAMBAZI MWENYE SILAHA AKIMUOKOA MUMEWE,

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimwangalia mgonjwa ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Mahyolo, Wilayani Bunda, Samson Malegesi aliyevamiwa na jambazi na kukatwakatwa mapanga mwili nzima, jana. Hata hivyo, Mke wa mgonjwa huyo, Busimba Malegesi (katikati), alifanikiwa kumuokoa mumewe kwa kumnyang’anya silaha jambazi hilo. Mgonjwa huyo amelazwa katika Hospitali ya Kibara, Wilayani humo akiendelea kupewa matibabu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akimwangalia mgonjwa ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Mahyolo, Wilayani Bunda, Samson Malegesi aliyevamiwa na jambazi na kukatwakatwa mapanga mwili nzima, jana. Hata hivyo, Mke wa mgonjwa huyo alifanikiwa kumuokoa mumewe kwa kumnyang’anya silaha jambazi hilo. Kulia ni Muuguzi wa hospitali ya Kibara, Godliver Josephat, ambapo mhonjwa huyo amelazwa akipatiwa matibabu. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), akiingia Hospitali ya Kibara Wilayani Bunda kumwangalia mgonjwa aliyevamiwa na jambazi na kukatwakatwa mapanga mwili nzima, jana. Hata hivyo, Mke wa mgonjwa huyo alifanikiwa kumuokoa mumewe kwa kumnyang’anya silaha jambazi hilo. Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara, Wilayani humo, Mkaguzi Boniface Mwalupale. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akiondoka Hospitali ya Kibara Wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, mara baada ya kumwangalia mgonjwa aliyevamiwa na jambazi na kukatwakatwa mapanga mwili nzima, jana. Hata hivyo, Mke wa mgonjwa huyo alifanikiwa kumuokoa mumewe kwa kumnyang’anya silaha jambazi hilo. Kulia ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara, Wilayani humo, Mkaguzi Boniface Mwalupale.




Na Felix Mwagara, (MOHA) MARA.

Mkazi wa Kijiji cha Mahyolo, Kata ya Nyamihyolo, Wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, Busimba Malegesi amemuokoa mumewe asiuawe na jambazi mwenye silaha ambaye alivamia katika nyumba yao na kuanza kumshambulia mwanaume huyo kwa kumkatakata mapanga mwili mzima.

Busimba alimrukia jambazi huyo kiunoni na kumuangusha chini na kufanikiwa kumnyang’anya panga pamoja na tochi ambazo alikua nayo wakati anamshambulia mumewe aitwaye Samson Malegesi (62).

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa 7:30 usiku wa kuamkia Ijumaa wakati familia hiyo ikiwa imelala ndipo jambazi huyo alivunja mlango na kuingia moja kwa moja chumbani kwa wanandoa hao na kuwasha tochi kumsaka Malegesi na baada ya kufanikiwa kumuona alianza kumshambulia kwa kumpiga mapanga kichwani, mikononi, kwenye mbavu na kusababisha damu nyingi kumwagika.

Wakati jambazi hilo akiendelea kumshambulia Malegesi, mkewe alikua naye anapambana kwa kumzuia asimshambulie mumewe, lakini jambazi hilo lilizidiwa baada ya mwanamke huyo kupata nguvu zaidi na kufanikiwa kumuangusha chini na kuhakikisha silaha aliyoishika mkononi akinyang’anywa kwa urahisi kutokana na kubanwa kwa juu na mwanamke huyo.

Mwanamke huyo wakati akipambana na jambazi huyo alikua akipiga kelele lakini sauti yake haikuweza kuwafikia majirani ili waweze kumpa msaada, hata hivyo jambazi huyo baada ya kuona anakosa nguvu baada ya kukandamizwa chini, akafanikiwa kupata upenyo ndipo akakimbia kutoka katika nyumba hiyo.

Hata hivyo, baada ya jambazi huyo kukimbia, mwanamke huyo alitoka nje kuomba msaada zaidi kwa majirani na walifanikiwa kufika na walimpeleka Hospitali ya Misheni ya Kibara Wilayani humo ambapo alifikishwa akiwa hajitambui na kuanza kupewa matibabu ya haraka ili kuokoa maisha yake.

Muuguzi wa Hospitali hiyo, Godliver Josephat alisema amempokea mgonjwa huyo akiwa na waaguzi wenzake, saa 9:00 usiku akiwa hajitambui na ndipo wakashirikiana na madaktari wakamuwekea dawa ya kuzindua uhai wa mgonjwa huyo na kufanikiwa kuzinduka na wakaendelea na tiba zingine ikiwemo kuzuia kutoka damu pamoja na kushonwa sehemu alizokatwa mapanga.

“Tumempokea mgonjwa huyo saa tisa usiku akiwa ana hali mbaya sana, jitihada zetu zilifanikiwa kumpa huduma ya kwanza kwa kumuwekea dawa ya kuzindua uhai wake na baadaye tukaendelea kumpa huduma zingine ikiwemo kuanza kumshona kwasababu alikatwa panga la kichwa, mikono yake yote miwili ilijeruhiwa, mbavu zake upande wa mgongoni alichimbwa kwa kukatwa na panga, hivyo hali yake ilikua tete, hata hivyo tumefanikiwa kumuhudumia kwa umakini mkubwa na sasa mnamuona anaweza kuzungumza,” alisema Godliver.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ambaye alikua katika ziara ndani ya jimbo lake ambapo tukio hilo limetokea, mara baada ya kupata taarifa ya tukio hilo alfajiri ya jana, alifika hospitalini hapo na kuelekea chumba cha upasuaji akakuta madaktari wakiendelea kumshona sehemu mbalimbali za mwili wake zilizojeruhiwa.

Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo la Mwibara, aliwasili Hospitali hapo akiwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara (OCS), Mkaguzi Boniface Mwalupale pamoja na madiwani na viongozi wa Halimashauri wa Wilaya ya Bunda ambao uambatana nao wakati akiwa katika ziara zake jimboni mwake.

“OCS hakikisheni hamlali mpaka mnalipata jambazi hili kwa kutumia njia zote za kiintelejinsia mulizosomea ili muweze kumsaka na kumtia mbaroni haraka iwezekanavyo, huu ni unyama na lazima akamatwe, mtafuteni usiku na mchana, msikae ofisini kunywa chai, hakikisheni huyu mtuhumiwa anakamatwa.” Alisema Lugola.

Lugola baada ya kutoa maelekezo hayo saa mbili asubuhi, alitoka hospitali hapo na kuendelea na mikutano ya hadhara jimboni humo na akasisitiza kuwa majambazi wasiibipu serikali kwa kuwa bado ipo macho kuhakikisha wananchi wake wapo salama, kutokana na tukio hilo Polisi watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa.

“Nampongeza sana mwanamke aliyepambana na jambazi ili amuokoe mumewe, hakika kama sio ushujaa wa mwanamke huyo tungempoteza mumewe kwasababu jambazi huyo alidhamiria kumuua kwa kumkata mapanga zile sehemu ambazo ni hatari zaidi kwa uhai wa ubinadamu,” alisema Lugola alipokua anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Busagara, Kata ya Chitengule, jimboni humo jana jioni.

Kwa upande wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara, Mwalupale alisema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, tayari askari wapo katika msako mkali wa kumsaka jambazi huyo na wamemhakikishia Waziri Lugola pamoja na wananchi kuwa watamkamata mtuhumiwa huyo.

“Jambazi huyo alifanya uvamizi huo lakini hakuiba chochote ndani ya nyumba hiyo, inaonyesha kuwa, lengo la jambazi hilo alitaka kumvamia mtuhumiwa pekee. Ila tunaendelea kufanya uchunguzi kujua lengo la mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo la kinyama, na tutahakikisha tunamkamata na kumfikisha mahakamani,” alisema Mwalupale.

Hata hivyo, Waziri Lugola baada ya kumaliza mikutano yake jioni alirudi tena hospitalini hapo na kumkuta mgonjwa huyo ametoka chumba cha upasuaji na amepelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Lugola alitoa pole kwa ndugu na wananchi waliokuwepo hospitalini hapo kutokana na unyama aliofanyiwa mwananchi huyo na kuhahidi Serikali ipo pamoja nao na watahakikishia jambazi hilo pamoja na wengine watakamatwa.   

No comments: