Saturday, December 8, 2018

TUMEANZISHA BENKI YA KILIMO ILI KUTOA MITAJI KWA WAKULIMA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa lengo la kuwasaidia wakulima wapate mitaji ili waongeze tija.

Pia amewataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wahahakikishe wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha miwa.Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Desemba 7, 2018) alipotembelea shama la miwa Mkulazi na MbIgiri mkoani Morogoro alipokuwa njiani kwenda jijini Dodoma.

Alisema lengo la kuanzishwa shamba la mwa la Mkulazi ni katika jitihada za Serikali za kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikikia katika kiwango kinachohitajika.Waziri Mkuu alisema Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee ni kuboresha kilimo cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.

Alisema shamba hilo linaendeshwa kwa ubia kati ya NSSF na Jeshi la Magereza, hivyo, aliiagiza Menejimenti mpya ya Mkulazi kuhakikisha shamba hilo linasimamiwa kikamilifu.Waziri Mkuu pia, alimuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike apeleke wataalamu wengi wa kilimo katika shamba hilo ili wasaidie kusimamia kitaalamu.

“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu, uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na watu binafsi,” alisema.Kuhusu suala la maji hususan kipindi cha mvua ambayo huaribu shamba, Waziri Mkuu aliwataka watafute namna nzuri ya kuyahifadhi ili wayatumie kipindi cha kiangazi.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka watafute mashine nyingine zitakazotosha kumwagilia shamba hilo wakati wa kiangazi ili miwa isiharibike na iendelee kuwa ya kijani wakati wote.Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenistar Mhagama, alisema shamba la Mkulazi II ni miongoni mwa mashamba mawili yanayomiilikiwa na wabia wawili yaani NSSF na Jeshi la Magereza.

Alisema walikubaliana wao na Magereza wafanye kazi kwa kuongozwa na uzalendo, maadili ya utendaji wa kazi, uaminifu ili mwisho wa siku mradi huo uwe na tija na uweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa.Alisema wanaamini fedha zilizowekezwa kwenye mradi huo ambazo ni za wanachama zinatakiwa zirudishe faida kwa wanachama wenyewe na kujenga uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha tatizo la upatikanaji wa sukari nchini linakuwa historia.

Alisema mbali ya shamba hilo la Mkulazi II pia kuna lingine la Mkulazi I ambalo ni kubwa zaidi, hivyo alishauri liendelezwe ili limalize tatizo la sukari nchini. Waziri Mkuu alimtaka ashughulikie shamba hilo kwa kuwa lipo Wizara ya Kilimo.


  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kulia)  wakati alipowasili kwenye shamba la miwa la Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro,
PMO_1450
          Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipotembalea shamba la miwa la Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro, Desemba 7, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stevene Kebwe.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


No comments: