Friday, December 7, 2018

Mtawa awataka wauguzi nchini kuzingatia miongozo ya kazi

Wauguzi nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi kwa kufuata miongozo iliyopo ikiwamo taratibu, kanuni na sheria.

Hayo yamesemwa na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa katika mkutano wa kikao kazi uliowashirikisha wauguzi wakuu wa mikoa ya Tanzania, wauguzi wakuu wa hospitali za rufaa za kitaifa na hospitali maalum, baadhi ya wakuu wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya uuguzi na ukunga pamoja na baadhi ya wauguzi wakuu wa wilaya nchini.

Bi. Mtawa amesema kwamba taaluma ya uuguzi inaongozwa na sheria na kanuni ambazo zimeainisha miongozo jinsi ya kumuwajibisha muuguzi anayekwenda kinyume na taratibu na maadili.“Kutokana na muongozo huu, viongozi wa baraza ngazi ya mikoa, wilaya na vyuo wanapaswa kutimiza wajibu wao katika kusimamia miongozo,” amesisitiza Bi. Mtawa.

Mkurugenzi huyo amewataka wauguzi kuzingatia pia matumizi ya miongozo mipya kama muongozo wa kusimamia utoaji wa huduma ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) uliyoboreshwa yaani NIMART, muongozo wa mafunzo ya kujiendeleza yaani CPD, muongozo wa ufuatiliaji wa huduma za uuguzi na ukunga pamoja na mfumo mpya wa TEHAMA ambao utasaidia kuweka kumbukumbu za huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga kwa kielectroniki.

Pia, Bi. Mtawa amewataka wauuguzi kuwa na vyeti vya taalama yao vinavyotambulika na mamlaka husika kwani wenye vyeti vya kughushi watakamatwa na kushtakiwa katika vyombo vya sheria.Amesema baraza hilo lina mfumo imara ambao una uwezo wa kutambua waauguzi wenye vyeti vya kughushi vya kitaalama, hivyo amewataka kuwa makini.

“Mfumo huu utasaidia sana kutatua changamoto ya wimbi la kughushi vyeti vya kitaaluma ambalo limeibuka katika kipindi hiki. Mpaka sasa jumla ya kesi 15 ziko mahakamani kwa sababu ya watumishi walioghushi vyeti vya uuguzi na ukunga pamoja na leseni,” amefafanua Bi. Mtawa.

Lengo la kikao kazi hicho lilikuwa kuwakumbusha na kuwajengea uwezo wauguzi na viongozi juu ya wajibu wao wa kusimamia utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga Tanzania, kusimamia maadili ambayo bado yanalalamikiwa na wananchi.

Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania ni mamlaka iliyoundwa kisheria ambayo moja ya majukumu yake ni kusimamia taaluma ya uuguzi na ukunga Tanzania.
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa akiwaonyesha washiriki sheria na kanuni inayosimamia taaluma ya uuguzi na ukunga nchini.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia kikao hicho ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa ofisi za baraza hilo, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa baraza hilo.

No comments: