Thursday, December 13, 2018

MASHAHIDI 15, VIELELEZO VYAO VITATU KUTUMIKA KATIKA KESI YA ZITTO KABWE

Na Karama Kenyunko blogu ya jamii


UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa inatarajia kuleta mashahidi 15 na vielelezo vitatu katika kesi hiyo. 

Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga wameeleza hayo leo Desemba 13, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi Mara baada ya kumaliza kumsomea Zitto maelezo ya awali ( PH).

Katuga amedai watakuwa na mashahidi 15 na vielelezo viwili vya kimaandishi na kielelezo kimoja cha kieletroniki.Ameongeza kudai kuwa jinsi kesi itakavyoendelea kusikilizwa wanaweza kuongeza mashahidi na vielelezo au kupunguza mashidi, kwa sababu hata baada ya Zitto kusomewa maelezo hayo Leo na kuyajibu wanaweza kuwapunguza.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Shaidi alimpa nafasi Wakili wa Zitto, Peter Kibatala kuzungumza, ambapo alidai kuwa wataongea baada ya 
upande wa mashtaka kufungua ushahidi wao.Pia Katuga aliiomba Mahakama iwape muda wa wao kuweza kutoa nakala ya mtoa taarifa ili waweze na kuwapatia upande wa utetezi kama sheria inavyoelekeza.

Awali, Wakili Wankyo akimsomea Zitto PH amedai Oktoba 28, 2018 mshtakiwa akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT_Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Iliendelea kusomwa kuwa, maneno hayo yaliyotamkwa sio tu yalichochea 
chuki lakini pia yalitengeneza uhusama kwenye mamlaka halali akupelekea 
mijadala miongoni mwa makundi mbali mbali katika jamaii na kwenye 
mitandao na vyombo vya habari kwa ujumla.

Pia, alidai kuwa maneno hayo yaliwafanya watu wafikirie kuwa Serikali haiwajali raia wake.Kutokana na maneno hayo, Zitto alikamatwa Oktoba 30 mwaka huu akiwa nyumbani kwake Masaki na kuwekwa mahabausu ya polisi na pia nakala ya taarifa ya vyombo vya habari polisi wali ikuchukua baada ya kuwa Zitto amekamatwa.

Baada ya kumsomewa maelezo hayo, Zitto alikubali majina yake, alikubali kuwa yeye ni Mbunge na pia alikubali kuwa alikamatwa nyumbani kwake Masaki.Hata hivyo Zitto alikataa maelezo mengine yote ikiwemo kuwa yeye si Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na nakala ya taarifa hiyo haikukutwa 
nyumbani kwake wakati anakamatwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 14, 2019 kwa ajili ya kutajwa na itaendelea kusikilizwa Januari 29,2019.

No comments: