Thursday, December 13, 2018

BENKI KUU TAWI LA DODOMA WAANIKA MAJUKUMU YAO ILI KUFANIKISHA SHUGHULI ZA UCHUMI KWA WANANCHI

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Dodoma limefafanua kwa kina majukumu yake mbalimbali na miongoni mwa majukumu hayo ni kutunza na kusambaza fedha (noti na sarafu) safi za thamani mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha wananchi kutekeleza shughuli mbalimbali za uchumi katika Kanda ya kati. 

Tawi la BoT, Kanda ya Kati, Dodoma, ni tawi la tano kufunguliwa tangu nchi ipate uhuru; na ni moja ya matawi mawili ambayo yamefunguliwa miaka ya hivi karibuni.Wakati tawi la Dodoma limefunguliwa 15/10/2015, Tawi la Mtwara limefunguliwa Machi 2017. 

Awali Tawi la Dodoma lilitarajiwa kutoa huduma za benki kuu katika mikoa ya Dodoma, Singida Iringa and Tabora. Hata hivyo kutokana na kukamilika ujenzi wa tawi la Mtwara, na kama ilivyokuwa kwa matawi mengine ya awali, mgawanyo wa mikoa katika kanda za Benki Kuu ulibadilika. 

Meneja wa masuala ya Fedha na Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania(BoT) tawi la Dodoma Dk.Camilius Kombe ametaja baadhi ya majukumu ya tawi hilo wakati anazungumzia majukumu ya benki hiyo kwa waandishi wa habari waliokuwa kwenye mafunzo ya habari za fedha na uchumi.

Ambapo katika majukumu hayo yapo pia ya kukusanya fedha zilizotumika kutoka vituo maalum vya kusambazia fedha vilivyo katika baadhi ya mabenki ya biashara na kuondoa katika mzunguko fedha ambazo zimechakaa na hazifai kutumika tena.

Pia kukusanya takwimu na taarifa za uchumi na biashara katika mikoa ya kanda ya kati na kuandaa ripoti za vipindi tofauti ambazo zinajumuishwa katika maandalizi ya sera ya fedha na utekelezaji wake. Kutoa huduma za kibenki na malipo kwa Serikali zote mbili, taasisi za serikali na mabenki.

"Majukumu haya yote ni kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT Act, 2016, Vifungu 5, 6, 31 na 32 vinavyohusu kukusanya na kuchambua takwimu za uchumi, BOT kuwa benki ya serikali na benki ya mabenki mengine na kushiriki na kutoa huduma za malipo au kukamilisha malipo,"amesema.

Amefafanua ili kutekeleza majukumu haya makuu, Tawi la Dodoma linafanya kazi muhimu zifuatazo ambazo ni kupanga na kutekeleza taratibu za kusambaza fedha (kwa ujumla) katika kanda kupitia mabenki ya biashara na kupitia vituo maalum vilivyopo Tabora na Kigoma.

"Ili kuwezesha usambaji wa fedha katika mikoa iliyo mbali na Dodoma, Benki Kuu ina mkataba na benki ya biashara ya NMB (tawi la Tabora, Mihayo) na benki ya CRDB (tawi la Kigoma) kwa ajili ya kutunza fedha za Benki Kuu katika matawi yao ili mabenki mengine yahudumiwe kupitia vituo hivyo maalum kama mabenki yaliyopo hapa Dodoma au mikoa ya jirani yanavyohudumia na tawi letu hapa jijini Dodoma. 

"Kwa hiyo, vituo hivi vya fedha na ofisi ya tawi hapa Dodoma, kwa pamoja, ndio mhimili mkubwa wa usambaji fedha safi katika mabenki kwa ajili ya shughuli za uchumi katika kanda yetu, kama ilivyo katika matawi mengine ya Benki Kuu,"amesema Dk.Kombe.

Kuhusu mchango wa maalum wa Tawi la Dodoma katika kuimarisha huduma za Benki Kuu Dk.Kombe amesema katika kutekeleza dhiima ya taasisi yao licha ya uchanga wake, zimekuwa zikiimarika tangu kufunguliwa kwake Oktoba 2015 ambapo tawi hilo lilipofunguliwa Oktoba 15, 2015 kulikuwa na benki saba; na tano tu ndizo zilikuwa zinapata huduma ya kibenki na sarafu hapo tawini. Hivi sasa katika kanda hiyo ya kati kuna jumla ya mabenki 21 yaliyo na matawi 101.

Amefafanua pamoja na majukumu ya kawaida ambayo matawi yote yanafanya, tawi la Dodoma limepewa nafasi ya kutoa baadhi ya huduma za msingi kwa wadau wakuu, hasa Serikali na taasisi zake, huduma ambazo zimekuwa zikifanyika makao makuu, Dar es Salaam pekee. 

Amesema tangu serikali ilipoanza kuhamisha shughuli zake kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, na hatimaye kuhamia rasmi, huduma zote za kibenki kwa serikali, taasisi zake na Bunge wanazipata kwenye tawi hilo."Kwasababu hii ongezeko la kazi ya kutoa huduma katika tawi letu ni kubwa na linaendelea. Hata hivyo tumeendelea kujipanga na wadau wetu wanaridhishwa sana na huduma zetu"amesema Dk.Kombe.
Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania(BoT) tawi la Dodoma Nolasco Maluli akizungumzia majukumu ya tawi hilo wakati wa semina ya waandishi wa habari mjini Dodoma leo
Meneja Msaidizi wa Huduma za kibenki BoT tawi la Dodoma Lilian Silaa akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa semina ya mafunzo ya uandishi wa habari za fedha na uchumi
Mtangazaji na Mwaandishi wa redio Clouds FM akizungumza kwenye semina ya waandishi wa habari za fedha na uchumi

No comments: