Wednesday, December 12, 2018

KAMPUNI YA SETEWICO LIMITED DODOMA YAIOMBA SERIKALI KUANGALIA NAMNA YA KUPUNGUZA UTITIRI WA KODI ZILIZOPO



Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

UTITIRI wa kodi ambazo zinalipwa na wawekezaji nchini bado umeonekana kuwa changamoto kubwa kwao na hivyo kutoa ombi kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kuangalia namna ya kupunguza utitiri huo wa kodi ambao umekuwa mzigo kwao pamoja na wananchi kwa ujumla.

Ombi hilo limetolewa Mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetewico Limited Katrin Boehl baada ya baadhi ya maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) pamoja na waandishi wa habari wa habari za fedha na uchumi kufanya ziara ya kutembelea kampuni hiyo kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.Waandishi hao wapo kwenye mafunzo ya kuandika habari za fedha na uchumi yaliyoandaliwa na BoT ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini.

"Kwa upande wangu lazima niseme nimeona ushirikiano wa hali ya juu katika Serikali yangu Dodoma kwani nikiwa na tatizo lolote ninakwenda katika ofisi za Serikali yangu ya Dodoma, hivyo imeonesha uthamini wa kiwango kikubwa wa kazi tunazofanya" ameongeza Katrin.

Amesema kampuni yao inapongeza juhudi za Serikali katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda nchini ili kufikia uchumi wa kati na wamedhamiria kuunga mkono kwa vitendo kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu lakini changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo ni uwepo wa kodi nyingi ambazo zinawafanya wanakuwa katika wakati mgumu kutekeleza majukumu yao ya uzalishaji kwai gharama ni kubwa.

"Nampongeza sana Rais Dk.Magufuli pamoja na Serikali yake kwani tunaona dhamira njema katika kuhakikisha Tanzania inakuwa ya viwanda.Kampuni yetu tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa kutoka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.Hata hivyo kilio chetu ni wingi wa kodi ambazo zinasababisha kutumia fedha nyingi kwenye uzalishaji na matokeo yake bidhaa zetu zinakuwa juu kiasi cha kushindwa 
kuhimili ushindani wa soko.

"Kampuni yetu pamoja na kuzalisha maji ya kunywa , pia tunayo kampuni ambayo inahusika na utengenezaji wa mvinyo unaotokana na zabibu za Dodoma.Tunajitahidi kutengeneza bidhaa bora ambayo ipo kwenye ubora wa kimataifa lakini kilio chetu ni makodi mengi ambayo yanatufanya tuuze kwa bei kubwa ili kurudisha sehemu ya gharama zetu ambazo nyingi msingi wake ni wa kodi ambazo tunazozwa,"amesema.

Kutokana na utitiri huo wa makodi ambapo alihesabu zipo zaidi ya 13 , ametoa ombi kwa Serikali kuhakikisha wanakaa na kuangalia kodi na ikiwezekana zipunguzwe ili kurahisisha mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania huku akionesha kufurahishwa na kasi ya uwekezaji wa viwanda unaondelea nchini.

"Ombi letu namba moja tunaomba hili la kodi kuangaliwa upya, ni nyingi na zimekuwa mzigo kwetu.Tunapofikia suala la kodi kichwa kinauma na hapa ndipo tunataka Serikali itupie jicho lake.Tunaamini waandishi wa habari ambao mmetutembelea tunaomba mtusaidie kutufikishia kiloo chetu .Kodi zikiwa rafiki  tutapiga hatua na kufanikisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano,"amesema 
Katrin.

Kwa upande wa waandishi waliotembelea kiwanda hicho, wameahidi kutumia kalamu zao kuhakikisha wanafikisha ombi la muwekezaji huyo kwa niaba ya wawekezaji wengine ambao wamekuwa wakilalamikia suala la uwepo wa kodi  nyingi.Hata hivyo tayari Rais Magufuli mara kadhaa amekuwa akizungumzia  umuhimu wa kuwepo kwa kodi rafiki ambazo zitalipika kwa urahisi.
Waandishi wa habari wakiwa pamoja na maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) wakimsikiliza Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetewico Limited Katrin Boehl wakati anafafanua namna kampuni yao inavyotengeneza mvinyo unaotokana na zabibu ya Dodoma.Waandishi na maofisa hao wametembelea kampuni hiyo kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.
:Mwenyekiti wa mafunzo ya waandishi wa habari za uchumi na fedha Nurdin Selemen (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetewico Limited Katrin Boehl wakati wa waandishi wa vyombo mbalimbali walipotembelea kwenye kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetewico Limited Katrin Boehl akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari za fedha na uchumi na maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) baada ya kutembelea kampuni yake kuangalia shughuli za uzalishaji.
Meneja Msaidizi Uchumi na Takwimu wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Kanda ya Kati, Dk. Zegezege Mpemba akizungumza mbele ya Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetewico Limited Katrin Boehl() baada ya waandishi wa habari walioko kwenye mafunzo ya habari za fedha na uchumi kutembelea kampuni hiyo.

No comments: