Wednesday, December 5, 2018

DC NAMTUMBO AIAGIZA TAKUKURU KUICHUNGUZA HALMASHAURI .

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Mfaume Kizigo ameiagiza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU wilayani Namtumbo kuchunguza shilingi milioni 950 zilizobadilishiwa matumizi na Halmashuri ya Namtumbo.

Kizigo aliyasema hayo hivi karibuni katika mkutano wa baraza la madiwani wilayani humo baada ya kubaini baraza la madiwani kutoridhika na taarifa ya mkaguzi wa ndani wa Halmashauri hiyo juu ya kubadilisha matumizi ya fedha shilingi milioni 950.

Taarifa ya mkaguzi wa ndani wa Halmashuri hiyo bwana John Mwingira ilidai Halmashuri hiyo imebadilisha matumizi ya fedha kiasi cha shilingi milioni 950 na kutumika kwa matumizi mengineyo tofauti na ilivyokusudiwa .

Aidha bwana Mwingira katika taarifa yake hiyo alidai kuwa fedha hiyo imetumika kwa nia njema lakini zinatakiwa kurudishwa katika shughuli iliyokusudiwa na serikali kwa kutumia mapato ya ndani ambayo kwa sasa yanasuasua.

Taarifa hiyo ilisema katika shilingi milioni 950 milioni 500 zilikuwa Ruzuku ya serikali zikiwa na lengo la kujenga Hospitali ya wilaya ambapo katika fedha hiyo milioni 200 zilibadilishwa matumizi na kumalizia zahanati saba viporo vya Halmashuri hiyo na kuanza kutumika na milioni 20 nazo zilibaki kujenga jengo moja katika Hospitali ya wilaya na milioni 156 zilipelekwa kukamilisha chumba cha upasuaji katika kituo cha afya lusewa katika mamlaka ya mji mdogo wa Lusewa.

Milioni 450 kati ya hizo milioni 950 zilipokelewa na Halmashuri hiyo kutoka bodi ya mikopo ya serikali za mitaa LGLB ambazo nazo zililenga kujenga soko zilibadilishwa matumizi na kulipia deni la vifaa vya viwandani milioni 214 zilizokopa Halmashuri hiyo na milioni 26 zilitumika kununulia mashine ya kukusanyia ushuru (POS)ishirini.

Diwani wa kata ya Hanga bwana Kassimu Ntara alidai anasikitishwa na taarifa hiyo ya kubadilishwa matumizi ya fedha kiasi cha shilingi milioni 397 zaidi ya kile kilichokubaliwa katika kamati ya fedha ,uongozi na mipango lakini pia idhini iliyotolewa na baraza la madiwani ya kutumia shilingi milioni 214 pekee.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilayani Namtumbo wameanza kuitekeleza agizo la mkuu wa wilaya huyo kuchunguza matumizi ya fedha hizo kwa kuhoji wahusika waliohusika kutoa fedha hizo na kuruhusu zitumike kinyume na malengo ya serikali.

Mwisho. picha ya kwanza DC Namtumbo na picha ya pili Diwani wa kata ya Hanga akichangia kwenye baraza hilo

No comments: