Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Watendaji, kwenye Ofisi za Kituo hicho jijini Dar es salaam, Desemba 4, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwenye viwanja vya Ofisi za Kituo hicho jijini Dar es salaam, Desemba 4, 2018. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa, Faustine Kamuzora na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza, Afisa wa NEMC katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Linda Mutafungwa wakati alipotembelea Kituo hicho, Desemba 4, 2018. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Maofisa wa Kodi na Forodha wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Leonard Mapunda (wapili kulia) na Helen Haule (kulia) wakati alipotembelea Kituo hicho, Desemba 4, 2018. Kushoto ni Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Maofisa wa Kodi na Forodha wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Leonard Mapunda (kulia) na Helen Haule ( wapili kulia) wakati alipotembelea Kituo hicho, Desemba 4, 2018. Kushoto ni Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Wajumbe wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakati alipotembelea Kituo hicho jijini Dar es salaam, Desemba 4, 2018. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimalize urasimu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake. Kadhalika, ameuagiza uongozi wa TIC uweke kipaumbele cha kwanza katika kulinda rasilimali za nchi na maliasili zake ikiwemo ardhi, mazao ya uvuvi, misitu, madini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo jioni (Jumanne, Desemba 4, 2018) alipozungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa TIC na Menejimenti, jijini Dar es Salaam. “Katika kuvutia wawekezaji hasa wa nje ni lazima tuweke kipaumbe katika kulinda rasilimali zetu kama ardhi, madini fukwe ili zisiporwe kwa kisingizio cha uwekezaji.” Amesema eneo hilo linahitaji umakini na uadilifu mkubwa, hivyo ni muhimu kwa kituo hicho kuhakikisha kinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maslahi ya Taifa. Amesema ili kupata matokeo mazuri ni lazima waimarishe mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau wote sambamba na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa.
“Serikali imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025, TIC inatakiwa iongoze kwa kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.” Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa wawekezaji ambao TIC inatakiwa ivutie ni walio mahiri wenye nia thabiti ya kutufikisha huko na siyo wachuuzi au madalali. Kadhalika,Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inataka TIC iwe kioo cha nchi ambacho kitavutia wawekezaji. Amesema Serikali inataka TIC mpya ambayo itakuwa kimbilio la wawekezaji wengi wa ndani na nje, badala ya kuwa kikwazo na kusababisha wawekezaji wakija kukimbilia.
Hivyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa kituo hicho ubadilishe muundo wa kuwapokea wawekezaji, wawapokee vizuri na wawaeleze fursa za uwekezaji zilizopo. “ Pia, TIC iweke mazingira rafiki ya kuwawezesha Watanzania wengi kumiliki uchumi kwa kuanzisha miradi mipya wao wenyewe au miradi ya ubia kati ya wawekezaji.” Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kila mtumishi wa umma ni lazima afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu, uadilifu, weledi, uaminifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Waziri Mkuu amesema ni lazima wahakikishe vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma vinaepukwa na kila mtumishi.” Serikali haivumii watumishi wa aina hiyo.” Kwa upande wake,Mkurugenzi wa TIC, Geofrey Mwambe amemuomba Waziri Mkuu awasaidie kwa kuwapatia ofisi kwa kuwa eneo wanalofanyia kazi kwa sasa halitoshi. Pia amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa rasilimali watu, sasa wanahitaji watumishi 31 wakiwemo mameneja 11.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea eneo la kutolea huduma za pamoja zilizopo ndani ya Kituo hicho cha Uwekezaji Tanzania na kusema kwamba ameridhishwa na utendaji.
No comments:
Post a Comment