Friday, December 14, 2018

CHAMA CHA WASANII WA KIZAZI KIPYA ZANZIBAR KUZINDUA TAMASHA LA WAZI

CHAMA Cha wasanii wa Kizazi kipya Zanzibar (ZFU) , kimeandaa tamasha la Muziki Safari ya Mapinduzi ambalo linatarajiwa kufanyika  Desemba 15 mwaka huu  kwa lengo la kuenzi fikra za Mapinduzi na kutangaza kazi mbali mbali zinazofanywa na Wasanii wa kizazi kipya nchini.

Akizungumza mapema leo mjini Unguja na waandishi wa habari Rais wa Chama hicho,Mohamed Abdallah 'Laki wa Promise' amesema Chama hicho kimeamua kufanya tamasha hilo ambalo litafanyika katika jimbo la Mpendae Uwanja wa Zantex  litasaidia kukumbusha jamii umuhimu wa fikra za mapinduzi.

Rais huyo amesema katika tamasha hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini Unguja, Abdulrahman Khatib ambapo kabla ya kuanza kwa tamasha hilo kutatanguliwa na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, uvutaji kamba na kukimbiza kuku. "Lengo kubwa ni kuchochea fikra za mapinduzi zilizofanywa na wanamapinduzi ambao wamepoteza maisha yao kwa ajili yetu ambapo kwa sasa tunaona mafanikio yake ikiwemo kuwepo kwa amani mpaka sasa hivyo ni jambo la kuwakumbusha Wanzanzibari.

kwa hiyo tutatumia vipaji vyetu vya kuimba kuwaambia jamii,"amesema Laki kuwa ni  jukumu la Chama hicho kupitia sanaa kuwahabarisha jamii umuhimu wa mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964 na kwamba lazima yalindwe kwa njia yeyote ile na kwamba kupitia tamasha hilo litasaidia kuipa jamii hisia kali za Mapinduzi hayo.  "Tamasha hili litaanza kuanzia saa 6 mchana hadi saa 12 jioni hivyo tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kwamba wasanii wengi watatoka Unguja na Pemba katika kutuimbuiza tamasha hilo na katika michezo itakayochezwa washindi watapewa zawadi mbalimbali,"ameeleza Rais huyo.

Akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja za Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo  Salum Said, amewasihi wananchi wa maeneo mbali mbali ya Mjini wa Zanzibar kuunga mkono juhudi za wasanii hao walioamua kwenda kwa jamii moja kwa moja kuonyesha vipaji vyao kupitia sanaa ya muziki. Amesema sanaa ya muziki ni moja ya kichocheo cha maendeleo ya nchi kwani inatoa ajira mbali mbali kwa vijana na makundi mengine ya kijamii, hivyo jamii inatakiwa kuacha dhana za kuamini kuwa usanii ni uhuni jambo ambalo sio kweli.

Amesema maandalizi yote ya tamasha hilo yamekamilika na kuanzia kesho wasanii wataanza kutikisa majukwaa ya burudani. Kwa upande wake Msemaji wa Chama hicho, Rashid Mustaafa 'Spaider'amesema matamasha kama hayo yanasaidia kukuza wasanii hivyo ni muhimu kuyaendeleza visiwani humu.

Amesema tamasha ya aina hiyo yanasaidia kukuza soko la muziki la hapa Zanzibar katika kufanya vizuri hivyo kwa upande mwingine yatasaidia kuibua vipaji vipya ambavyo vitakuwa ni azina kwa siku za baadae. "Tunaweza kufanya vizuri Chama kama pamoja na wasanii kwa upande mwingine hivyo tamasha ya aina haya yanasaidia sana katika ukuzaji wa vipaji,"ameeleza  Msemaji wa Chama Cha Wasanii.  

Tamasha hilo linaloanza kesho Desemba 15,mwaka huu litafikia tamati disemba 29,mwaka huu ambapo michezo mbali mbali itafanyika ikiwemo kuvuta kamba, mechi za mpira wa miguu,kufukuza kuku pamoja na Wasanii mbali mbali kutumbwiza mamia ya wananchi katika sehemu husika. Zawadi mbali mbali zitatolewa kwa washindi wa michezo hiyo na kwa mashabiki wa burudani watakaoonyesha uwezo wa kuimba na kucheza.
 RAIS wa Chama Cha Wasanii Zanzibar  Mohamed Abdalla 'Laki wa Promise' (wa pili kushoto), Msemaji wa Chama hicho Rashid Mustaafa 'Spaider'(wa kwanza kushoto),Mwenyekiti wa Tamasha Salum Said(wa kwanza kulia) wakizungumza na waandishi wa habari juu ya ufunguzi wa tamasha hilo.
BAADHI ya Waandishi wa Habari wa Vyombo vya Habari mbali mbali visiwani Zanzibar wakisikiliza maelezo ya Rais wa Chama Cha Wasanii Zanzibar Mohamed Abdallah 'Laki wa Promise' juu ya uzinduzi wa Tamasha la muziki Safari ya Mapinduzi.

No comments: