Monday, December 10, 2018

BoT YAWANOA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU HABARI ZA UCHUMI NA FEDHA

*Naibu Gavana ahimiza uwajibikaji kwa waandishi wa habari nchini

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) ,imesema imeamua kuanzisha utaratibu wa kuendesha semina kwa waandishi wa habari wa vyombo vya habari nchini kwa lengo la kukuza uandishi wa habari za uchumi na fedha.

Pia lengo la semina hiyo kwa waandishi wa habari nchini ni kuelimisha na kufafanua masuala yanayohusu majukumu na kazi za Benki Kuu , kujenga uwezo wa kutafsiri na kuchambua taarifa za uchumi na fedha, kuboresha na kudumisha uhusiano mzuri wa kikazoi kati ya vyombo vya habari na BoT.

Malengo mengine ya semina hiyo ni kupata mrejesho kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu utendaji wao wa kazi na njia bora ya kudumisha mawasiliano baina ya taasisi zao.
 
Hotuba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) upande wa Uchumi na Sera Dk. Yamungu Kayandabila ambayo imesomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Tawi la Benki Kuu Dodoma Richard Wambali amesema benki hiyo inatambua mchango wa vyombo vya habari nchini katika kuufahamisha umma wa Watazanzania na dunia
kwa ujumla.

"Mara kadhaa mmekuwa msaada mkubwa sana katika kutufikishia taarifa zetu kwa umma, na wakati mwingine baada ya kupokea mwito wa muda mfupi.Pia kupitia kazi zenu mnatuwezesha kujua ni nini wananchi wanasema au kutarajia kutoka katika taasisi zetu."Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikiendesha semina kama hii, tumeshuhudia kuimarika kwa uandishi wa habari za uchumi na fedha katika vyombo mbalimbali vya habari.Matokeo haya mema yametupa uthibitisho kwamba mafunzo tunayotoa kwa wadau wetu wakuu yana manufaa makubwa,"amesema.

Pia amesema wameshuhudia kuendelea kukua kwa ushirikiano kati ya BoT na vyombo vingi vya habari zikiwemo redio, televisheni , magazeti na mitandao ya kijamii na kwamba uhusiano huo unadhirihishwa kupitia maswali mengi na ya mara kwa mara wanayoyapata kutoka kwa mwandishi  mmoja mmoja au kupitia idara yao ya uhusiano wa umma na itifaki.

Ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili na kauni zinazoongoza tasnia ya habari kwa sababu wajibu wa wanahabari katika kuchangia maendeleo ya ustawi wa jamii ni mkubwa ambapo amesisitiza uandishi wa habari unaozingatia uwajibikaji pamoja na kuandika habari za usahihi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO)Zamaradi Kawawa ameipongeza BoT kwa kutoa mafunzo yanayohusu habari za uchumi na fedha hasa kwa kuzngatia mafunzo hayo yameendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini kuandika kwa usahihi na weledi.

Wakati huo huo waandishi wa habari waliokuwa kwenye semina hiyo wameipongeza BoT kwa kuendelea kuandaa semina hizo kwani zimekuwa zikiwajengea uwezo hasa wa kuandika habari za biashara na uchumi kwa ufasaha zaidi. Pia wamesema kutokana na semina hiyo kumekuwa na uhusiano mzuri kati ya BoT na waandishi wa vyombo vya habari nchini

Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Dodoma Bw. Richard Wambali aliyemwakilisha Dkt. Yamungu Kayandabila Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha akifungua semina ya siku tano ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu masuala ya uchumi na fedha inayofanyika kwenye ukumbi wa (BOT) jijini Dodoma. 

No comments: