Monday, December 10, 2018

Una mpango wa kusafiri? Zingatia haya.

Una mpango wa kusafiri? Zingatia haya

Ni wakati mwingine tena wa msimu wa sikukuu za Krismasi na mapumziko ya mwisho wa mwaka. Katika kipindi hiki tunashuhudia pilikapilika za hapa na pale watu wakijiandaa namna watakavyosherehekea.

Kuna baadhi ya watu wanafikiria kusafiri nje ya mikoa waliyopo kwa ajili ya kusherehekea. Watu wengi wana kawaida ya kusafiri kurudi waliko zaliwa na kukulia ili kujumuika pamoja na ndugu na jamaa zao. Wengine hupanga kwenda kutembelea vivutio vya kutalii kwenye mikoa tofauti na walipo.

Kipindi cha nyuma kidogo usafiri wa umma ndio ulikuwa tegemezi ukilinganisha na sasa ambapo baadhi ya wasafiri wanamiliki usafiri wao binafsi. Kusafiri kwa usafiri binafsi kuna faida lukuki hususani kama mko wengi na wote mnakwenda sehemu moja. Hupunguza gharama lakini mnakuwa huru kuamua msafiri namna gani, muda wa kuondoka na kufika, kupumzika njiani nakadhalika.
Pamoja na faida lukuki za kusafiri kwa kutumia usafiri ubinafsi, yafuatayo ni masuala ya msingi kuyazingatia kabla ya kuanza safari yako. 

Jipange mapema. Kabla ya kuanza safari yako hakikisha kuwa chombo chako cha usafiri kipo kwenye hali salama. Hali ya hewa inatofautiana kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine hivyo huna budi kuhakikisha gari lako linakuwa na uwezo wa kuhimili hali yoyote itakayokutana nayo safarini. Wasiliana na fundi wako ambaye huwa analihudumia gari lako mara kwa mara ili kukusaidia katika hili. 

Pumzika vya kutosha. Miongoni mwa sababu iliyotajwa kusahaulika kuwa inachochea kutokea kwa ajali nyingi za barabarani ni madereva kutopumzika vya kutosha kabla ya safari. Hivyo basi kama dereva ambaye unatarajia kuendesha chombo cha usafiri kwa umbali mrefu hakikisha kuwa unapata muda wa kutosha kupumzika. Hii itakusaidia mwili kuwa katika hali nzuri na kupelekea umakini mkubwa barabarani. 

Kuwa makini na mwendo kasi. Hakuna haja ya kushindana kwa mwendo kasi na madereva wengine barabarani. Zingatia umbali wa kutosha baina yako na chombo kingine cha usafiri ili kuweza kuepuka ajali pindi itakapotokea. Takwimu tofauti duniani zinaonesha kuendesha gari kwa mwendo kasi kunapelekea ajali nyingi, majeruhi wengi na hata vifo zaidi. Unashauriwa kuendesha kwa kuzingatia alama za barabarani.

Epuka vishawishi. Kumekuwa na kawaida ya baadhi ya madereva kuendesha gari huku wakiwa wanazungumza na simu, kusoma au kuandika jumbe za maneno, pamoja na kuperuzi kwenye simu zao za mkononi. Kuendesha chombo cha usafiri kunahitaji umakini wako wote. Endapo kutakuwa na ulazima wa kutumia simu yako ya mkononi hakikisha unaegesha gari pembeni ya barabara ili kukidhi haja yako halafu uendelee na safari.

Endesha kwa kujihami. Barabarani kunaweza kuwa na sababu tofauti ambazo zinaweza kukuondolea umakini wako. Barabara zinaweza kuwa katika hali mbaya hivyo kupelekea kupata ajali kwa urahisi. Au kunaweza kuwepo na madereva wenye kuendesha kwa kasi kuwahi huko waendapo. Wapuuze madereva wa aina hii wala usishindane nao. Hakikisha unaweka usalama wako na wa abiria uliowabeba kwanza. 

Usiendeshe ukiwa umelewa. Kama una mpango wa kunywa pombe, achana na mpango wa kuendesha. Pombe ni miongoni mwa sababu kubwa inayopelekea ajali nyingi za barabarani. Kama una mpango wa kuendesha chombo cha usafiri hakikisha hautumii kilevi cha aina yoyote na endapo utafanya hivyo basi hakikisha unakabidhi usukani kwa mtu mwingine.
Mbali na kujiandaa mapema kwa ajili ya kusafiri, pia unashauriwa kupanga mapema masuala ya malazi. Unaweza kukamilisha mipango ya safari yako kwa kujihakikishia malazi kupitia Jumia Travel. Katika msimu huu wa sikukuu huduma ya malazi huwa na uhitaji mkubwa kutokana na watu wengi kusafiri sehemu mbalimbali. Unaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, kuepuka usumbufu wa dakika za mwisho kwa kufanya huduma zako mapema pamoja na kuwa na uhakika wa malazi huko uendako.

No comments: