Thursday, December 6, 2018

BENKI YA NMB YATOA MSAADA WA STULI NA MEZA ZA MAABARA SHULE YA SEKONDARI MWANTINI

Benki ya NMB imetoa msaada wa Stuli 32 na meza 8 za maabara zenye thamani ya Shilingi milioni tano ili kusaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi katika shule ya Sekondari Mwantini iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga. 
 

Msaada huo umekabidhiwa leo Alhamis Desemba 6,2018 na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko.

Katamba alisema msaada huo wa stuli na meza ni sehemu ya ushiriki wa benki hiyo katika maendeleo ya jamii akibainisha kuwa changamoto za sekta ya elimu nchini kwa NMB ni jambo la kipaumbele kutokana na kwamba elimu ni uti wa mgongo wa taifa lolote duniani. “NMB tulipokea maombi kuwa mnahitaji stuli na meza za maabara,tulifarijika na kuamua kuja mara moja kushirikiana nanyi ili kuwa chachu ya maendeleo ya elimu kwa watoto wetu katika shule hii”,alieleza.

“Tunatambua kuwa kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka,kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni,tutaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wetu kuhakikisha changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi”,aliongeza Katamba.

Hata hivyo alisema kwa mwaka 2018,NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu hivyo kuifanya benki ya NMB kuwa benki ya kwanza kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini.

Kwa Upande wake,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko aliishukuru benki ya NMB kwa mchango huo mkubwa katika shule ya Mwantini hali ambayo itawafanya watoto wajifunze kwa vitendo masomo ya sayansi.

“Tunawashukuru sana NMB kwa jitihada mnazofanya katika sekta ya elimu,serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto zote, ni lazima tushikirikiane tushirikiane na wadau”,alisema Mboneko.

“Wanafunzi someni kwa bidii ,epukeni vishawishi na kataeni kuolewa katika umri mdogo,someni masomo ya sayansi kwani Tanzania ya Viwanda itajengwa kama kutakuwa na wataalamu wa Sayansi”,aliongeza.

Naye Diwani wa kata ya Mwantini,Majenga Samson aliitaka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kumalizia ujenzi wa jingo la maabara katika shule hiyo pamoja kujenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike.

Hafla fupi ya makabidhiano hayo pia imehudhuriwa na Mwenyekiti wa ALAT taifa,mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Gulam Hafeez Mukadam.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko akiishukuru benki ya NMB kwa msaada wa stuli na meza za maabara katika shule ya sekondari Mwantini iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Wa pili kulia ni Diwani wa kata ya Mwantini Majenga Samson,akifuatiwa na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba na Meneja wa Benki ya NMB Manonga,Baraka Ladislaus.

Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba akizungumza wakati wa kukabidhi stuli 38 na meza 8 za maabara katika shule ya sekondari Mwantini.Alisema benki hiyo imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye elimu kwa kutoa madawati na viti na afya kutoa vitanda na magodoro pamoja na kusaidia pale majanga yanapotokea nchini.

Sehemu ya stuli na meza za maabara zilizotolewa na benki ya NMB kwa ajili ya wanafunzi katika shule ya sekondari Mwantini iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Meneja wa Benki ya NMB Manonga,Baraka Ladislaus akimkaribisha Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba ili akabidhi stuli 32 na meza 8 za maabara kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko kwa ajili ya shule ya sekondari Mwantini.
Kulia ni Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba akishikana mkono na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Jasinta Mboneko wakati wa zoezi la kukabidhi stuli 32 na meza 8 za maabara kwa ajili ya shule ya sekondari Mwantini.Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa ALAT taifa,mheshimiwa Gulam Hafeez Mukadam ambaye pia ni Mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje wakipokea moja kati ya stuli 32 kutoka benki ya NMB. Kulia ni Meneja wa Benki ya NMB Manonga,Baraka Ladislaus na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi James Katamba.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko akisalimiana na wanafunzi wa shule ya sekondari Mwantini.

Picha ya pamoja wakati wa makabidhiano ya stuli na meza za maabara katika shule ya sekondari Mwantini.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Jasinta Mboneko akiwa katika picha ya pamoja na walimu,wanafunzi,viongozi wa benki ya NMB na viongozi mbalimbali.
Picha nyingine ya pamoja.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments: