Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, anatarajiwa kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu mapinduzi ya sekta ya usafirishaji na mabadiliko ya kiuchumi katika nchi zinazoendelea, jijini Arusha.
Mkutano huo wa siku mbili (2) ulioandaliwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kushirikiana na Shirikisho la Barabara Duniani (World Road Association-PIARC), utafanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema maandalizi kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika ambapo takribani washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 25 duniani watashiriki mkutano huo.
Mkutano huo ambao lengo lake kuu ni kuangalia matokeo ya uwekekezaji katika mundombinu ya usafirishaji utajadili kwa kina mada mbalimbali zinazohusu changamoto zinazozikabili nchi zinazoendelea ikiwemo rasilimali chache za kuimarisha miundimbinu ya usafirishaji wakati huohuo kuboresha huduma nyingine za kijamii kama vile maji, afya, elimu na nishati.
"Tutajadili namna ya kuimarisha miundombinu ya kisasa ya usafiri na usafirishaji inayoendana na teknolojia inayopatikana katika nchi zinazoendelea", amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Barabara Tanzania (TARA), Bw. Joseph Haule, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo amezitaja nchi zitazoshiriki kuwa ni Bangladesh, Botswana, Canada, Jamhuri ya Czech, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Ufaransa, Ujerumani, Ghana na Japan.
Nyingine ni Kenya, Liberia, Madagaska, Msumbiji, Nepal, New Zealand, Nigeria, Rwanda, Seirra Leone, Afrika Kusini, Korea kusini, Sudan Kusini, Sri Lanka, Uturuki,Uganda, Uingereza na mwenyeji Tanzania. Kwa upande wake, Katibu mkuu wa PIARC. Bw. Patrick Mallejacq, amesema kufanyika kwa mkutano huo Tanzania kutafungua fursa za kiuchumi, kijamii na kiteknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Tanzania ilijiunga na PIARC mwaka 1992 na mwaka huu TARA imekubaliwa kuwa kamati ya kitaifa ya PIARC katika mkutano uliofanyika Yokohama nchini Japani mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2018.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akisisitiza jambo kwa wadau wa Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC), hawapo pichani, Mkutano huo unaanza kesho mjini Arusha.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC), Bw. Patrick Mallejacq, akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Barabara Tanzania (TARA) Bw. Joseph Haule, hati ya makubaliano baada ya TARA kukubaliwa kuwa mwakilishi wa PIARC nchini Tanzania, katikati ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, akishuhudia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC) utakaoanza kesho katika ukumbi wa AICC, mjini Arusha.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC), Bw. Patrick Mallejacq (kulia), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC), unaoanza kesho mjini Arusha. Katikati ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga na kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Barabara Tanzania (TARA) Bw. Joseph Haule.Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment