Tuesday, November 13, 2018

WAZIRI MKUU ASIKITISHWA WIZI KWENYE MRADI WA NSSF DEGE

*Aagiza wakurugenzi wakuu wa NSSF, AZIMIO, Kamishna TRA wakutane

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa nyumba unaojengwa kwa ubia kati Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited katika eneo la Dege Beach Kigamboni na kutamka kuwa amesikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaendelea kwenye eneo hilo.

Amewaagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio na Mkurugenzi wa Mkuu kampuni ya Azimio Housing Estate Limited, Mohammed Iqbal wakutane na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere ili wajadiliane namna ya kudhibiti wizi na kuimarisha ulinzi. 

Waziri Mkuu alitembelea eneo la mradi huo jana jioni (Jumatatu, Novemba 12, 2018) ambapo baada ya kufika katika eneo ambalo linajengwa nyumba zaidi ya 7,000 alionesha kusikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaoendelea na kutoa maagizo kwa wahusika.

“Kuna mpango gani wa ulinzi wa mali hapa, mali zinaendelea kuibiwa, tutakuja kuanza ujenzi hapa na kukuta hakuna mali hata moja. Ulinzi lazima uimarishwe pande zote mbili za mradi huu eneo la ujenzi na eneo la kuhifadhia vifaa vya ujenzi.”

Kwa upande wakeMkurugenzi Mkuu wa NSSF, Erio alimuahidi Waziri Mkuu kwamba atahakikisha wanakutana na Kamishna wa TRA na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya AZIMIO ili kujadiliana na namna ya kuimarisha ulinzi na kutatua changamoto ya wizi wa mali unaoendelea katika eneo hilo.

Mkataba kati ya NSSF na Azimio Housing Estate Limited (AHEL) ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni ya hodhi ya “Hifadhi Builders” ambapo AHEL ilikuwa na asilimia 55 na NSSF asilimia 45. Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa kwenye mradi na asilimia 35 angetakiwa kuweka fedha taslimu.

Mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba 7,460 ambapo jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani 653,436,675 ambazo kati yake ujenzi ungegharimu Dola 544,530,562 wakati gharama za ardhi zingekuwa Dola 108,906,113. Kwa fedha za Tanzania mradi pamoja na ardhi ungegharimu sh. trilioni 1.5.

Hadi kufikia Juni 2018 NSSF walishailipa kampuni ya Hifadhi Builders Dola 133,838,662.2 kama mchango wake kwenye ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na sh. bilioni 305.8 wakati kampuni ya Azimio ikitoa Dola 5,500,000 sawa na sh. Bilioni 12.6 tu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, NOVEMBA 13, 2018.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia Majengo ya  DEGE ECO- VILLAGE  mradi wa   ubia kati ya Shirika la hifadhi ya Jamii NSSF na Azimiao wa Nyumba 7,4460 zilizopo  Wilaya ya Kigamboni Dar es salaam .jana  Novemba 12/2018 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa . katikati mwenye Tai nyekundu   atembelea DEGE ECO- VILLAGE  mradi wa   ubia kati ya Shirika la hifadhi ya Jamii NSSF na Azimio wa Nyumba 7,4460 zilizopo  Wilaya ya Kigamboni Dar es salaam .kulia  ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF .Wiliam Erio na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Azimio. Mohammed Iqbal. Waziri Mkuu ametembelea mradi huo jana  Novemba 12/2018.PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa . katikati mwenye Tai nyekundu   atembelea DEGE ECO- VILLAGE  mradi wa   ubia kati ya Shirika la hifadhi ya Jamii NSSF na Azimiao wa Nyumba 7,4460 zilizopo  Wilaya ya Kigamboni Dar es salaam .kulia  ni Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF Balozi Ali Siwa.na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Azimiao. Mohammed Iqbal. Waziri Mkuu ametembelea mradi huo jana  Novemba 12/2018

No comments: